Header Ads

Responsive Ads Here

MAKAMU WA RAIS, MHE.HASSAN KUZINDUA MAKUMBUSHO MAPYA YA OLDUVAI NA ONESHO LA CHIMBUKO LA MWANADAMU TAREHE 03 OKTOBA, 2017 MKOANI ARUSHA


Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na waandishi wa habari jana mkoani Morogoro kuhusu uzinduzi wa Makumbusho Mapya ya Olduvai na Onesho la Chimbuko la Mwanadamu ambayo yatazinduliwa tarehe 03 Oktoba, 2017 na Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika eneo la Olduvai wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha. 
 Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na waandishi wa habari jana mkoani Morogoro kuhusu uzinduzi wa Makumbusho Mapya ya Olduvai na Onesho la Chimbuko la Mwanadamu ambayo yatazinduliwa tarehe 03 Oktoba, 2017 na Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika eneo la Olduvai wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha. (Picha na Hamza Temba – WMU)

Morogoro, Septemba 28, 2017
……………………………………………………………….
Serikali ya Tanzania kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa
kushirikiana na Umoja wa Ulaya imekamilisha ujenzi wa Makumbusho mapya ya Olduvai
ambayo yanaonesha 
Chimbuko
la Binadamu (The Cradle of Humankind)
katika Bara la Afrika.
Makumbusho hayo mapya pamoja na Onesho la Chimbuko la Binadamu, yatafunguliwa
rasmi na  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan tarehe 03 Oktoba,
2017 katika eneo la Olduvai, ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.
Onesho hilo ni matokeo ya utafiti wa muda mrefu uliofanyika katika Bonde
la Olduvai na Laetoli katika Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha. Wananchi,
viongozi mbalimbali wa kitaifa na Mabalozi wanatarajiwa kuhudhuria kwenye hafla
hiyo.
Idadi kubwa ya vioneshwa
katika Makumbusho hiyo, vilipatikana katika bonde la Olduvai na Laetoli nchini Tanzania
kupitia utafiti wa kisayansi wa muda mrefu na vilikuwa vimehifadhiwa katika Makumbusho
ya Taifa, Jijini Dar es Salaam. Vioneshwa hivi ni pamoja na masalia ya
zamadamu, zana za mawe na masalia ya wanyama walioishi takribani miaka milioni 4
iliyopita.
Makumbusho hayo yamepangwa
kuonesha sehemu kuu nne zinazowiana.  Sehemu
ya kwanza inahusu ushahidi wa nyayo
za zamadamu zilizongunduliwa huko Laetoli mwaka 1978 na mtafiti Dr. Mary D.
Leakey.  Nyayo hizi ziliachwa na zamadamu
anayeiitwa Australopithecus afarensis na
ndio ushaidi usiopingika wa zamadamu kutembea wima kwa miguu miwili takribani
miaka milioni 3.6 iliyopita.
Sehemu ya pili inahusu
hadithi ya kusisimua ya kuwa binadamu (Genus
Homo); ambapo kutakuwa na masalia ya
zamadamu wanaoitwa Zinjanthropus au Paranthropus boisei na Homo habilis, zana za mawe za mwanzo zilizotumika
(Oldowan) katika kujipatia chakula na
ushahidi wa kale wa ulaji wa nyama katika historia ya mabadiliko ya binadamu,
takribani miaka million 2 iliyopita.
Sehemu ya tatu inahusu maisha ya jamii ya Homo erectus.  Jamii hii ilikuwa
inafanana zaidi na
binadamu wa sasa kuliko jamii zilizotangulia. Kutakuwa na masalia zamadamu Homo erectus, zana za mawe (Acheulian) na ushahidi wa ulaji wa
wanyama wakubwa kama vile Nyati na tembo katika historia ya mabadiliko ya
binadamu, takribani miaka million 1.7 iliyopita.
Sehemu ya nne
inaonesha kipindi cha mwanzo cha
binadamu wa sasa (Homo sapiens)
walioanza kutokea hapa Afrika miaka laki 2 iliyopita. Sehemu hii pia itaonesha
mila na utamaduni wa makabila mbalimbali kama vile Wahadzabe, wamasai na
Datoga.  Kutakuwa na mavazi ya asili ya
jamii hizo, zana za kuwinda na vifaa mbalimbali wanavyovitumia katika maisha
yao ya kila siku.
Wizara ya Maliasili na Utalii inawakaribisha wananchi wote kuhudhuria
ufunguzi huo ambapo watapata pia fursa ya kutembelea vivutio vingine vilivyopo
ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro ili kujifunza na kufurahia urithi huu wa asili
na kiutamaduni wa Taifa letu.
Imetolewa na;


Prof. Jumanne Maghembe
Waziri wa Maliasili na Utalii

No comments