Header Ads

Responsive Ads Here

MAKAMPUNI YA BIASHARA YATAKIWA KUHESHIMU HAKI ZA BINADAMU


IMG_1759-2
Washiriki wa Mafunzo ya  Uwezeshaji  kuhusu Biashara na Haki za Binadamu wakiwa katika picha  ya pamoja baada ya ufunguzi wa mafunzo hayo. mafunzo hayo ya siku moja yamefanyika mjini Bagamoyo na yameandaliwa   na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  kwa kushirikiana na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu kanda ya Afrika (OHCHR EARO).  Mafunzo hayo yalifunguliwa na Kaimu Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Obadia Kameya aliyeketi  katikati  kushoto kwake ni  Madame Nwanneakolam Vwede-Obahor na  kulia ni  Bi. Cecilia S. Shelly- Wakili wa Serikali Mfawidhi Mkoa wa Pwani


Na Mwandishi wetu, Bagamoyo
Makampuni ya Kimataifa na  Kitaifa yanayoendesha shughuli  za kibiashara hapa  nchi   makubwa  kwa  madogo yanatakiwa kuendesha shughuli zao kwa  kuheshimu haki za binadamu  na  kuwajibika pale yanapokiuka haki hizo.  
Hayo  yameelezwa leo  mjini  Bagamoayo na  Kaimu Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Obadia Kameya, wakati  akifungua mafunzo  ya uwezeshaji  kwa Maafisa wa  Serikali kuhusu Biashara na Haki za Binadamu.
Bw. Kameya amesema, Makampuni  ambayo yatabainika  kukiuka haki  za binadamu katika uendeshaji wa shughuli zao,  yanapashwa kuchukuliwa hatua na kwamba  mwenye wajibu huo ni Serikali ambayo ndiyo inayobeba dhamana   kwa  mujibu wa Katiba ya kuhakikisha kwamba haki za wananchi wake ndani ya mipaka yake  zinalindwa, kusimamiwa na  kutetewa.
Ni kwa sababu hiyo,  Kaimu  Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema, Maafisa wa Serikali  ambao kwa namna moja ama nyingine wanahusika na masuala ya   Biashara na Haki za Binadamu wanapashwa   kuwa na uelewa mkubwa kuhusu  Kanuni na  Miongozo inayohusu Haki za Binadamu  na  Biashara.
Akasema , suala   la  Biashara na Haki za Binadamu  limekuwa ajenda ya  ulimwengu katika miaka ya hivi  karibuni kutokana  na  kuhusishwa kwake   na haki za binadamu na ni katika  muktadha huo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu  wa Serikali  kama Mshauri  wa Serikali kuhusu  mauala ya Sheria, imeamua kwa Kushirikiana na  Kamisheni ya Haki za Binadamu  ya Umoja wa Mataifa Kanda ya Afrika (OHCHR-EARO) kuandaa  mafunzo ya kuwajenga uwezo  Maafisa wa  Serikali.
Bw. Kameya  akasisitiza zaidi kwa kueleza kwamba,  ni  muhimu sana kwa   Maafisa katika  Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  pamoja na Maafisa kutoka Wizara nyingine za Serikali na Taasisi  kuwa na  utambuzi  wa masuala ya  Biashara na  Haki za Binadamu ambayo  yaathari kwenye  sera, sheria, mikataba   na  makubaliano ya   kimataifa na katika utekelezaji wa  mipango mbalimbali  ya  Serikali na hasa katika kipindi hiki ambacho nchi imejielekeza kuwa nchi ya Viwanda. 
Naye Mwakilishi wa OHCHR EARO Madame Nwanneakolam Vwede-Obahor amesisitiza kwamba  ingawa  Maaofisa wa Serikali  wanaowajibu wa msingi kabisa wakuhakikisha kwamba wanafuatilia kwa karibu  na kuhakikisha kwamba Makapuni  ya Kibashara  yatekeleza na kuwajibika katika kuhakikisha kwamba  hayakiuki misingi na kanuni za  haki za binadamu na kwamba yajifanyia tathimini na kutoa  taarifa kama inavyotakiwa.
Wawezeshwaji wa Mafunzo hayo  wakiongozwa na  Madame  Nwanneakolam Vwede-Obahor ambaye ni Mwakilishi wa  Kamisheni   ya  Haki za Binadamu  ya Umoja wa Mataifa Kanda ya Afrika ( OHCHR-EARO) walifundisha  kuhusu  Mfumo wa Umoja wa Mataifa ulioridhiwa mwaka 2008 unaojulikana kama Zuia, Heshimu na Fidia   kuhusu Biashara na Haki za Binadamu.
Mfumo huu wa Umoja wa Mataifa una Misingi Mikuu Mitatu. Wa Kwanza ni   kuhusu wajibu wa serikali   kwa kuzingatia sheria ya Kimataifa  ya Haki  za Binadamu ya  kumlida kila mtu ndani ya mipaka yake na katika  eneo la mamlaka yake  kwa kuweka sheria madhubuti , kanuni , sera ikiwa ni pamoja na   kuzuia na kuchukua  hatua dhidi ya  ukiukwaji wa haki za binadamu  unaofanywa na  Makampuni ya Kibiashara.
Msingi wa Pili  wa mfumo huu unazitaka Kampuni za Biashara kuwajibika katika kuheshimu haki za binadamu mahali popote zinakoendesha shughuli zao  bila ya kujali ukubwa au udogo wa biashara hiyo ikiwa ni pamoja na  kutambua madhara yatokanayo na  shughuli zao na kuchukua hatua za kuzuia madhara hayo.
Msingi wa Tatu ni  utoaji wa fidia kutokana na athari za ukiukwaji wa haki za binadamu unaotokana na  shughuli za kibiashara zinazofanywa makampuni hayo. Baadhi ya athari hizo zinatajwa  kuwa ni  pamoja na uchafuzi wa mazingira,  ajali kazini, malipo au ujira duni, uhamishwaji wa kutumia nguvu na  usiozingatia sheria.
Washiriki wa Mafunzo hayo wametoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Mambo  ya Ndani, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria,  Wizara ya  Biashara na Viwanda, Tume ya Kurekebisha Sheria , Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kituo cha Uwekezaji, Nishani na Madini, na  Ofisi ya Makamu wa Rais.
IMEANDALIWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO  SERIKALINI
OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI
14/9/2017

No comments