Header Ads

Responsive Ads Here

MAHAKAMA KUU PEMBA YAMPA DHAMANA MTUHUMIWA WA DAWA ZA KULEVYA


Na Masanja Mabula -Pemba ..

MAHAKAMA kuu kanda ya Pemba, chini ya Jaji Mkusa Isac Sepetu, hatimae imempa dhamana  mwanamke mwenye mtoto wa siku 21, anaetuhumiwa kukutwa na kete 3,621 zinazodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya.

Jaji Mkusa, alilazimika kuitisha jalada la kesi hiyo ghafla kwenye kizimba cha mahakama kuu, baada ya Mahakama ya Mkoa Chakechake, chini ya hakim Hussein Makame Hussein, kuwanyima dhamana watuhumiwa hao.
Mama huyo Zuhura Ahmed Ali (29) mkaazi wa Jadida na mwenzake Seif Ali Seif (30) mkaazi wa Mtemani wote wilaya ya Wete, walipandishwa mahakamani mbele ya hakimu Hussein na kuwakosesha dhamana.
Licha ya wathumumiwa hao akiwemo mwanamke huyo, kuangua kilio cha taratibu na kuiomba mahakama dhamana huku akigonga meza na kushindwa kuitoa, hatimae Jaji Mkusa baada ya kuitisha jalada la watuhumiwa, hao alimpa dhamana mwanamke huyo, kwa sababu ya kuwa na kichanga.
Jaji Mkusa Isac, alilazimika kumpa masharti ya dhamana mtuhumiwa mmoja pekee, kwa kuandikisha shilingi milioni 5, na wadhamini wawili, wenye kima kama hicho, masharti ambayo aliyatimiza.
“Zuhuru tunakupa dhamana ya shilingi milioni tano, na wadhamini wenye kima kama hicho kila mmoja, lakini mwenzako ataenda rumande hadi tarehe iliopangwa 20 mwezi huu”,alisema.
Mara baada ya watuhumiwa hao kupanda juu ya kizimba cha mahakama, Mwendesha Mashitaka kutoka Afisi ya Mkurugenzi wa mashitaka Ramadhan Suleiman Ramadhan, alidai kuwa wote kwa pamoja, Septemba 9, mwaka huu walipatikana na dawa hizo za kulevya.
Alidai kuwa, walipatikana na kete hizo 3,621 kituo cha Polisi Mkoani Pemba, majira ya saa 6: 45 mchana, mara baada ya kupekuwaliwa, wakijua kuwa hilo ni kosa.
Mwendesha mashitaka huyo, aliiambia mahakama hiyo kuwa, kufanya hivyo ni kosa, kinyume na kifungu cha 15 (1) (a) sheria no 9 ya mwaka 2009, kama ilivyofanyiwa marekebisho na kifungu cha 11 (a) cha sheria no 12 ya mwaka 2011 sheria ya Zanzibar.
Mara baada ya kusomewa mashitaka yao, watuhumiwa hao kwa pamoja, walikana kuhusika na kosa hilo na kuiomba mahakama hiyo, iwapatie dhamana ombi ambalo kwa mtuhumiwa Seif, lilipingwa na mtuhumiwa Zuhura kukubalika.
Mtuhumiwa Zuhura Ahemed Ali, aliiomba mahakama hiyo kumpa dhamana, kutokana na kuwa ananyonyesha mtoto aliejifungua siku 21 zilizopita na kuyatimiza masharti ya dhamana.
“Muheshimiwa jaji, naomba unipe dhamana, maana mimi kwanza hali yangu sio nzuri, lakini kisha nna mtoto mchanga nanyonyesha na tokea juzi ninae Polisi, na kuna mbu”,aliomba mtuhumiwa huyo.
Kwa upande wake mtuhumiwa Seif Ali Seif, aliomba dhamana hasa kutokana na kwamba, yeye hahusiki na tukio hilo, na siku tatu kamili, alikuwa kituo cha Polisi na hajapata mlo.
“Muheshimwa, kwa vile mimi sihusiki na tukio hili, naomba dhamana, maana kwanza nna njaa na hali yangu sio mzuri”,aliomba dhamana hiyo, maombi ambayo yamekataliwa mahakamani.
Baada ya maombi hayo ya dhamana Jaji Mkusa wa mahakama kuu, ndipo alipomuamuru mtuhumiwa Seif, kwenda rumande hadi Septemba 20 mwaka huu.
Aidha Jaji huyo, alisema kwa vile tayari upelelezi umeshakamilika, siku hiyo mashahidi wote waitwe na barua za wito zitolewe kwao

No comments