Header Ads

Responsive Ads Here

MADIWANI LIMENI ILI MUWE MFANO WA KUIGWA; RC NCHIMBI


1
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akizungumza na  madiwani mapema leo katika mkutano wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (Alat)-Mkoa, tawi la Singida uliofanyika katika ofisi za halmashauri ya Wilaya ya Mkalama.

2
Madiwani na wajumbe wengine wa mkutano wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (Alat)-Mkoa, tawi la Singida uliofanyika katika ofisi za halmashauri ya Wilaya ya Mkalama wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Singida.
3
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (Alat)-Mkoa, tawi la Singida James Mkwega akizungumza katika mkutano huo mapema leo.
…………………………..
Madiwani Mkoani Singida wametakiwa kulima mazao ya biashara kama vile Pamba na Korosho ambapo mazao hayo ni ya kipaumbele Mkoani hapa, ili kuonyesha faida za kilimo hicho kwa wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amewaeleza hayo madiwani mapema leo katika mkutano wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (Alat)-Mkoa, tawi la Singida uliofanyika katika ofisi za halmashauri ya Wilaya ya Mkalama.
Dkt Nchimbi amesema madiwani wanapo hamasisha kilimo cha korosho na pamba kwa vitendo hasa kwa wao kuwa na mashamba yanayoonyesha zao hilo linastawi vizuri, wananchi wengi watahamasika na kujifunza kutoka kwao.
Ameongeza kuwa mkutano huo ulenge hasa katika kuangalia namna bora ya kumtumikia mwananchi na kuangalia njia mbalimbali za kumuokoa katika umaskini ili katika kuelekea Tanzania ya Uchumi wa kati na viwanda, asiwe mtazamaji bali mshiriki mkuu.
Dkt Nchimbi amesisitiza kuwa mkutano huo utumike pia kubainisha rasilimali zilizopo Mkoani Singida pamoja na fursa ambazo zinaweza kupatikana kutokana na uwepo wa rasilimali hizo.
“Singida tunazalisha ngozi na kuiuza ikiwa ghafi hivyo faida inakuwa ndogo, tumieni mkutano huu kuangalia uwezekano wa kuanzishwa kwa kiwanda kikubwa cha ngozi, ili tuanze sasa kuuza bidhaa za ngozi pamoja na kununua ngozi kutoka mikoa mingine nchini”, ameeleza Dkt Nchimbi.
Ameongeza kuwa ili kuboresha utendaji unaolenga kumsaidia mwananchi, maafisa utumishi wanapaswa kuwasimamia watumishi ili waweze kufanya kazi kwa bidii na uadilifu huku akiwataka wawapende watumishi wao.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (Alat)-Mkoa, tawi la Singida James Mkwega amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa nasaha zake na kumuahidi kuwa mkutano huo utaweka malengo ya kuendeleza mkoa.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amewaomba wananchi wa Singida kumuombea Mbunge wa Singida Mashariki Mhe. Tundu A. Lissu aliyejeruhiwa kwa risasi nyumbani kwake Dodoma.
Dkt Nchimbi amesema Lissu ni mwanasingida mwenzetu hivyo tunatakiwa kumuombea ili arejee katika afya yake na kuweza kuendelea na majukumu yake ya kuwatumikia wana Singida na Taifa kwa ujumla.
Aidha ameongeza kuwa hakuna anayefurahishwa kwa kitendo alichofanyiwa Lissu na kuwataka wanasingida na taifa kwa ujumla kuendelea kuliombea taifa liendelee kuwa kisiwa cha amani na utulivu.

No comments