Header Ads

Responsive Ads Here

MAADHIMISHO YA SIKU YA MOYO DUNIANI TAASISI YA MOYO (JKCI) KUFANYA UPIMAJI KWA WANANCHI BILA MALIPO


Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Chama cha Madaktari wa Moyo Tanzania (THF) katika kuadhimisha siku ya Moyo Duniani watafanya upimaji wa magonjwa ya Moyo bila malipo kwa wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam na mikoa jirani. Upimaji huo utaenda sambamba  na utoaji wa elimu ya lishe bora kwa afya bora ya Moyo.


Upimaji huu utafanyika katika viwanja vya Taasisi ya Moyo ambapo  wananchi watapimwa urefu, uzito, shinikizo la damu (BP), sukari na  kupewa ushauri. Kwa wale watakaokutwa na matatizo ya moyo watafanyiwa uchunguzi zaidi na kupatiwa matibabu. Kauli mbiu ya siku hii ni:  “Moyo wenye Afya”.

Katika wiki hii ya maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani tuna kambi maalum ya upasuaji  wa moyo wa bila kufungua kifua ambayo imeanza tarehe 25/09/2017  hadi tarehe 29/09/2017. Kambi hii tunaifanya kwa kushirikiana na Taasisi ya  Madaktari Afrika ya nchini Marekani.

Hadi sasa tayari tumewafanyia upasuaji wa bila kufungua kifua kwa kutumia mtambo wa Cathlab (kwa jila la kitaalam Cathertarization) wagonjwa 23, siku ya kesho tutamalizia kuwafanyia upasuaji  wagonjwa watano ili kufiokia idadi ya wagonjwa 28 tuliyolenga. Nia ya kambi hii ni kutoa huduma ya matibabu kwa wagonjwa na kubadilishana uzoefu wa kazi.

Wafanyakazi wa Taasisi hii tunahakikisha tunatoa  huduma bora zaidi za magonjwa ya moyo kwa wananchi wenye matatizo hayo. Mpango wetu ni  kutoa tiba ya moyo,  upasuaji wa moyo na elimu kwa jamii ambayo itawasaidia wananchi kuwa na ufahamu wa kutosha kuhusiana na magonjwa ya moyo ambayo ni moja ya magonjwa yasiyoambukiza na mtu anaweza kuyaepuka kwa kufuata ushauri wa kitaalam.

Tangu mwaka 2015 tumewafanyia upasuaji wa kupasua kifua, kuziba mishipa ya moyo, upasuaji wa mishipa ya moyo, upasuaji wa mishipa ya damu, kuweka vyuma ndani ya moyo,  na kuweka kifaa maalum cha kuusaidia moyo ili uweze kufanya kazi vizuri (Pacemaker) zaidi ya wagonjwa 1500.

Hatua hiyo imewezesha Serikali kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 45 fedha ambazo zingetumika kuwatibia wagonjwa wa moyo iwapo wangepelekwa njje ya nchi, hii ni sawa na asilimioa 85.

Taasisi pia inatoa huduma ya uchunguzi wa kipimo cha magonjwa ya moyo kwa watoto wachanga waliopo tumboni mwa mama zao (FETAL ECHOCARDIOGRAPHY) ili kujuwa kama wanamatatizo ya moyo au la.
Tangu kuanza kutolewa kwa huduma hii mwezi wan ne mwaka huu jumla ya kinamama wajawazito 37  wameshafanyiwa  uchunguzi wa kipimo hicho kati ya hao watoto watano walikutwa na matatizo ya moyo jambo ambalo litawawezesha   kupata matibabu mapema pindi watakapozaliwa.

Tunawaomba wananchi waadhimishe siku hii kwa kujitokeza  kwa wingi kupima afya zao hii itawasaidia kujuwa kama wanamatatizo ya moyo au la na hivyo kuanza matibabu mapema kwani asilimia kubwa ya wagonjwa tunaowapokea mioyo yao huo haiku katika hali nzuri.


Imetolewa na :

Kitengo cha Uhusiano na Masoko
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
28/09/2017

No comments