Header Ads

Responsive Ads Here

KIWANDA CHA NYAMA CHA MEAT KING KUZALISHA TANI 900,000 KWA MWAKA


maxresdefaultMahmoud Ahmad Arusha,

Kiwanda cha nyama cha Meat King Limited  kilichopo nje kidogo ya jiji la Arusha kinataraji kuzalisha tani 900,000 za nyama kwa mwaka mmoja huku kikipanga kukidhi mahitaji ya  soko la ndani kabla ya kuingia katika soko la jumuiya ya Afrika mashariki (EAC).
 
Akizungumza na wanahabari waliotembelea kiwanda hicho hivi karibuni  mkurugenzi mtendaji  wa kiwanda hicho Lesley De Kock amesema kuwa  wamefanikiwa kupata eneo la ukubwa wa ekari 4.5 mkabala na barabara ya Nelson Mandela ambapo  wamejenga jengo lenye ukubwa wa mita za mraba 1,216  ambapo watachakata mazao ya nyama na kufungasha sanjari na duka la jumla na rejareja .
 
 Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo alisema kwamba  awali kiwanda chao kilikuwa na uwezo wa kuzalisha tani 300,000 za nyama lakini kwa sasa wamejipanga kuzalisha kiwango hicho kwa tani 900,000 kwa mwaka ambazo zitakidhi mahitaji ya soko la ndani ya nchi.
 
Mkurugenzi huyo alisema kwamba malengo yao ni kutumia  mifugo ya ndani katika kuzalisha bidhaa za nyama  huku akisisitiza ya kwamba kipaumbele chao ni kuwatumia wafugaji mbalimbali nchini hususani wanaotoka katika maeneo ya kanda ya kazkazini.
 
“Malengo yetu ni kuzalisha bidhaa bora za nyama hapa nchini tuna mifugo ya kutosha sidhani kama tunahitaji kuleta bidhaa nyingine kutoka nje ya nchi”alisema De Kock
 
Alisema kwamba  mahitaji ya soko la ndani kwa sasa ni makubwa hivyo wamejipanga kuimarisha uzalishaji wa bidhaa zitakazokidhi soko hilo kabla ya kuhamia katika soko la nje .
 
Alisisistiza kuwa kiwanda hicho kimekuwa mkombozi wa uchumi  kwa wakazi wa Kata ya Moshono ambao  watapata fursa ya  kuuza mazao yao ya nyama kama  sungura,kondoo,nguruwe ,mbuzi na ng”ombe.
 
Kwa mujibu meneja wa kiwanda hicho Faustine Laizer  alisema kuwa kiwanda hicho kimegharimu jumla ya kiasi cha sh,4.4 bilion hadi kukamilika ambapo wamefanikiwa kutoa ajira kwa vijana  40 ambao ni wakazi wa jiji la Arusha.
 
Laizer ,alisema miongoni mwa changamoto wanazokumbana nazo ni pamoja  upandaji holela wa bei ya nyama nchini jambo ambalo linapelekea wao kushindwa kukabiliana na ushindani wa bidhaa za nyama zinazoingizwa kutoka nje ya nchi.
 
Aliongeza kuwa kumekuwa na changamoto ya wafugaji mbalimbali kuleta mifugo kiwandani kwao  isiyokuwa na ubora jambo ambalo linawafanya kutofikia malengo ya kuzalisha  bidhaa bora na kuwataka  wafugaji kuzingatia mifugo iliyo na afya bora kabla ya kuileta kiwandani hapo.

No comments