Header Ads

Responsive Ads Here

KAZI YA UUGUZI NI NGUMU INAHITAJI USTAHAMILIVU,KUJITUMA NA KUJITOA-NAIBU SPIKA ZANZIBAR


01
Waziri wa Afya Mhmoud Thabit Kombo akizungumza na wauguzi na wakunga walioshiriki kongamano la kujadili maadili  ya kada hiyo lililofanyika Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni Mjini Zanzibar.

02
Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Mgeni Hassan Juma akifungua kongamano la Wauguzi na wakunga lililofanyika katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani Kikwajuni.
03
Baadhi ya wauguzi na wakunga walioshiriki kongamano lililojadili maadili ya fani hiyo wakifuatilia ufunguzi rasmi katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni Mjini Zanzibar
04
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wauguzi na Wakunga Zanzibar Amina Abdulkadir akizungumzia umuhimu wa  maadili  ya uuguzi na ukunga na kiapo cha wauguzi katika kongamano lililofanyika Barazaa la Wawakilishi la zamani Kikwajuni Mjini Zanzibar.
                  IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI 
……………………….
Na Maryam kidiko-maelezo Zanzibar. 
Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi  Mgeni Hassan Juma amesema kazi ya Uuguzi  ni ngumu inahitaji  ustahamilivu, kujituma na kutoa huduma  kwa uadilifu bila upendeleo kwa wagonjwa wanaofika Hospitali kutafuta matibabu
Hayo aliyasema wakati akifunguwa Kongamano la siku moja la Wauguzi na Wakunga lililojadili kuporomoka kwa maadili ya kada hiyo katika  Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Alisema vijana wanaoingia katika kada ya Uuuguzi wanapaswa  kuwa wapenzi wa kazi hiyo bila ya kupata shinikizo kutoka kwa watu wengine  na kuwa tayari kukabiliana na changamoto zinazotokea ndani ya kada hiyo.
Alisema kuwahudumia Wagojwa kwa kufuata maadili na lugha nzuri  kunamsaidia mgonjwa kupata faraja  kabla ya kufika kwa daktari  na kunapunguza malalamiko na kuipelekea Wizara  ya Afya kuonekana  inatekeleza wajibu wake kikamilifu .
Aidha alisema kilio kikubwa cha Wananchi wanaofika Hospitali na Vituo vya afya kutafuta matibabu wanalalamikia lugha chafu  wanazotolewa na baadhi ya wafanyakazi na kuitia dosari kubwa Wizara ya Afya
“Wengi wenu mnafanya kazi nzuri lakini wapo wachache wanakiuka maadili na kuidhalilisha kada hii, endeleeni kutumia lugha itakayowaridhisha wagojwa na Wananchi wanaofika katika vituo vyenu,’’ alisema Naibu Spika.
AIiishauri Wizara ya Afya kuweka utaratibu  wa kuwapongeza Wafanyakazi wanaotekeleza wajibu wao  vizuri wa kuhudumia wagojwa kwa lengo la kuwahamasisha wengine kuiga mfano wao.
Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo alikiri kupokea malalalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu vitendo wanavyofanyiwa  na amefanya uchunguzi  na kugundua  kuwa baadhi ya malalamiko hayo yanaukweli.
 Aliwataka wakunga na wauguzi kutekeleza majukumu yao kwa mujibu walivyosomeshwa na kufuata utaratibu wa kutowa huduma bora kwa wagonjwa  ili waweze kurudisha heshma ya kazi zao.
“Hivi sasa mnabahati ya kupata nafasi za masomo na mafunzo ya mara kwa mara katika kada yenu, yatumieni kuongeza ufanisi na kuondosha malalamiko kutoka kwa wananchi ,” alisisitiza Waziri wa Afya.
 Mwenyekiti wa Baraza la Wauguzi na Wakunga Amina Abdulkadir aliwahimiza wauguzi na wakunga  tufanya kazi kwa mujibu wa sheria ili kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi ambao wamejenga imani kwao katika kupata huduma bora.
“Najuwa mnafanyakazi kazi nzuri katika kutowa huduma  kwa Wananchi lakini ongezeni juhudi ili muweze kuisaidia Jamii kama mulivyokula kiapo katika kazi hii,” alieleza Mwenyekiti .
Washiriki wa Kongamano hilo walilishauri Baraza la Wauguzi na Wakunga kusimamia kikamilifu sheria na kanuni za Baraza hilo ili wafanyakazi watakaobainika kwenda kinyume na sheria wachukuliwe hatua za kinidhamu.
Kongamano hilo lililoandaliwa na Wizara ya afya lilijumuisha wakunga na wauguzi, taasisi za kiraia, viongozi wa dini, Kamisheni ya Kazi na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar..

No comments