Header Ads

Responsive Ads Here

IGP SIRRO ATOA YA MOYONI KUHUSU SHAMBULIO LA LISSU PAMOJA NA KUTEKWA WATOTO ARUSHA


 1. Ndugu zangu waandishi wa habari, kwanza kabisa napenda kutumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kutupatia afya na kutuwezesha kuwepo hapa hii leo.
 2. Aidha napenda kuwashukuru sana ninyi waandishi wa habari kwa kuitikia wito wa muda mfupi wa kufika kwenye kikao hiki. Nawashukuru kwa ushirikiano ambao mmeendelea kutupatia sisi Jeshi la Polisi na wananchi, hasa raia wema, katika kazi zetu za kupambana na uhalifu hapa nchini.
 3. Ndugu Waandishi wa habari, nimewaita hapa leo ili kuzungumzia masuala mbalimbali kama ifuatavyo:-
  1. Tukianza na ripoti ya uchimbaji wa madini ya Tanzanite na Almasi:-
Ripoti hii ilikabidhiwa jana tarehe 07/09/2017 kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam. Mhe Rais alitoa maelekezo kwa vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua kwa wahusika waliotajwa kwenye ripoti hiyo. Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine tayari limeunda kikosi kazi cha kushughulikia ripoti hiyo na tayari baadhi ya watuhumiwa wamekamatwa na wanaendelea kuhojiwa kwa lengo la kukusanya ushahidi na hatimaye wafikishwe mahakamani.
 1. Matukio ya kihalifu ambayo yamejitokeza hivi karibuni:-
Nchi yetu ni shwari licha ya kuwepo kwa matukio machache ambayo Jeshi la Polisi linaendelea kuyashughulikia. Matukio ambayo bado tunaendelea kuyakabili ni pamoja na:-
 1. Kuhusu tukio la kuuawa kwa Wyne Lotter mwanaharakati wa kupinga ujangili tarehe 16/08/2017:- Watuhumiwa wa tukio hili wamekamtwa na baadhi ya mali za marehemu zimaekamtwa pia. Upelelezi bado unaendelea ili kuhakikisha kwamba wote waliohusika wanatiwa mbaroni.
 2. Tukio la mlipuko uliotokea katika ofisi za Mawakili wa IMMA:- Mnamo tarehe 20/08/2017 kulitokea milipuko katika ofisi hizo zilizopo katika eneo la Upanga jijini Dar es Salaam. Napenda kuwajulisha kuwa upelelezi unaendelea na utakapokamilika wahusika watafikishwa mahakamani mara moja.
 3. Tukio la utekaji wa watoto lililotokea mkoani Arusha (04/09/2017) na Geita (01/09/2017) :- Jeshi la Polisi limefanikiwa kuwakamata wahusika wa matukio haya ambapo mmoja wao aliuawa wakati akijaribu kutoroka mikononi mwa Polisi. Tunaendelea na upelelezi ili kuwababini wote waliohusika katika matukio haya.
 4. Tukio la kushambuliwa kwa risasi Mhe.Tundu Lissu (MB):- Mnamo tarehe 07/09/2017 katika eneo la Area D mkoani Dodoma Mhe.Tundu Lissu (Mb) na Mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) alishambuliwa kwa risasi na watu wasiofahamika na kujeruhiwa ambapo hivi sasa anaendelea na matibabu.
Kufuatia tukio hilo, nimeunda timu ya upelelezi kutoka Makao Makuu ya Polisi ambayo ilishafika mkoani Dodoma jana kuongeza nguvu ili kuhakikisha kuwa watuhumiwa waliofanya kitendo hicho wanakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Kufuatia tukio hilo, wananchi walianza kusambaza taarifa mbalimbli kwenye mitandao ya kijamii ambazo kwanza zinaibua hofu kwa jamii; pili zinaweza kuharibu upelelezi na; tatu zinaweza kujenga chuki na mtafaruku ndani ya jamii.
Napenda kutumia fursa hii kuwataka wananchi kuacha kusambaza ujumbe, picha, video na taarifa zisizo na ukweli kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na matukio kama haya. Ni vyema wananchi wakajua kufanya vitendo hivyo ni kosa kisheria. Natoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la polisi kwa kutoa taarifa zitakazofanikisha kukamatwa watuhumiwa wote waliohusika na tukio hili.
 1. Mwisho niwashukuru raia wema wanaoendelea kutupatia taarifa ambazo zimefanikisha kukamatwa kwa wahalifu wa matukio mbalimbali na niwaombe waendelee kutupatia taarifa wanapoona viashiria vya uhalifu.

Asanteni kwa kunisikiliza

Imetolewa na:

Inspekta Jenerali wa Polisi,
Makao Makuu ya Polisi,
DAR ES SALAAM.

No comments