Header Ads

Responsive Ads Here

HOSPITALI ZOTE ZA WILAYA NCHINI ZIJENGE JENGO LA KUTOLEA TIBA YA DHARURA: UMMY MWALIMU

003

Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu, ametoa agizo kuwa Hospitali zote za Wilaya nchini ziwe na jengo maalumu la kuhudumia wagonjwa wenye dharura.

Mhe. Waziri ametoa agizo hilojana Tarehe 25 Septemba, 2017 mjini Bagamoyo, alipokuwa katika sherehe za uwekaji jiwe la msingi ujenzi wa wodi ya wazazi na jengo la kuhudumia wagonjwa wa dharura ‘emergency care unit’ katika Hospitali ya Wilaya Bagamoyo.
Naagiza Wakurugenzi wote wa Halmashauri nchini, wajenge majengo ya kupokelea na kuhudumia wagonjwa wenye dharura yaani ili kuongeza wigo wa kuokoa maisha ya wagonjwa mahututi wanaohitaji huduma ya haraka na dharura, nitumie fursa hii kuagiza kuwa ifikapo Tarehe 30 June, 2018 majengo hayo yawe yamejengwa kwenye kila hospitali ya Wilaya nchini”. Amesema Mh. Waziri.        
Mhe. Waziri wa Afya, Bi. Ummy Mwalimu alikuwa mgeni rasmi katika uwekaji mawe ya msingi Majengo mawili yenye ghorofa moja yanayojengwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Kiislamu ya Dhi Nureyninayofanya kazi nchini, ambapo yatakapokamilika wafadhili hao pia wataweka vifaa vikiwemo vitanda na vifaa tiba kabla ya kuyakabidhi kwa matumizi.
Ujenzi huo unakadiriwa kugharimu jumla ya Shilingi Mil.316,819,710.00 kwa jengo la wazazi na Shilingi Mil. 178, 489,977.46 kwa jengo la tiba za dharura.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Alhaji Majid Mwanga amewashukuru wafadhili hao taasisi ya Kiislamu ya Dhi Nureyn kwa kuendelea kushirikiana na Serikali kwani katika Halmashauri ya Bagamoyo.
Tunaishukuru sana Taasisi hii kwakuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na Serikali kuiletea jamii maendeleo na kutatua changamoto mbalimbali hivyo kuipunguzia Serikali mzigo.Taasisi hii imekuwa ikifadhili miradi mbalimbali ya kijamii, ikiwemo miradi ya maji kwa kuchimba visima virefu 23 na vifupi 15 vyenye thamani ya Shilingi Milioni 614 na sasa wamefadhili mradi huo wa ujenzi wa wodi ya wazazi na jengo la kuhudumia wagonjwa wa dharura katika Hospitali ya Wilaya Bagamoyo”.Aliongeza Mhe. Mwanga
Wakati huo huo, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo Mh. Dkt. Shukuru Kawambwa akatumia fursa hiyo kuiomba Serikali kupitia Mhe. Waziri Ummy Mwalimu, kutoa msamaha wa kodi kwa vifaa tiba vitakavyoletwa na wafadhili hao kutoka nje ya nchi ili vitumike kwenye majengo hayo pindi yatakapokamilika,ili wafadhili hao waweze kuitumia fedha hiyo kununua vifaa tiba vingi zaidi.
Mhe. Kawambwa pia akaishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuipatia Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kiasi cha Shilingi Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Afya Kerege kwani Halmashauri hiyo haikuwa na kituo cha Afya na pia akamshuru Mhe. Waziri kuridhia kituo hicho cha Afya kujengwa katika kata ya Kerege kulingana na mahitaji badala ya kujengwa katika Kata ya Dunda kama ilivyokuwa imepangwa hapo awali.
Mganga Mkuu Wilaya ya Bagamoyo Bi. Sylivia Mamkwe akitoa taarifa yake ya utekelezaji kwa Mhe.Waziri amesema huduma ya Mama na mtoto Kiwilaya imeimarika na vifo vya akina Mama wakati wa kujifungua pia vimepungua kutoka akina mama 11 Mwaka 2015 hadi akina Mama 8 Mwaka 2016.
Hivyo ujenzi wa wodi hiyo mpya ya wakina Mama itasaidia uboreshaji wa utoaji huduma ya mama na mtoto katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo.
Imetolewa na,
KITENGO CHA TEHAMA
HALMASHAURI YA WILAYA
BAGAMOYO.

No comments