Header Ads

Responsive Ads Here

HATIMAYE MAHAKAMA YAKUBALI MANJI KUHOJIWA NA POLISI


Manji no ndevu
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu leo September 4, 2017, imeruhusu mfanyabiashara Yusuf Manji na wenzake wahojiwe na Jeshi la Polisi ili kukamilisha upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili.

Ruhusa hiyo imekuja baada ya upande wa mashitaka kuieleza mahakama hiyo kuwa waliomba hati ya kuwatoa washitakiwa  mahabusu ili kufanyiwa mahojiano katika kesi namba 33/2017 na kwamba polisi wakabidhiwe watuhuiwa hao.
Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shaidi alisema jana kuwa Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZCO), alimuandikia barua kuomba washitakiwa wahojiwe na kusema mahakama imekuwa ikisisitiza kesi za uhujumu uchumi zikamilishwe upelelezi ili ziweze kusikilizwa.
“Tusingeweza kukataa maombi hayo kwa sababu tutapingana na kauli yetu ya kukamilisha upelelezi. Ndio maana tumetoa hati ya kuwatoa mahabusu kwa ajili ya mahojiano. Hii sio mara ya kwanza kuwatoa washitakiwa kwa upelelezi.”
Aidha, amewataka Polisi kuzingatia haki za washtakiwa kwa kuhakikisha wana afya njema na wapate uhuru wa kuwakilishwa na Mawakili wao kwenye jambo lolote na isiwe kificho.
“Namkabidhi Koplo Dotto kama barua inavyoelekeza kwa kuwa Sajenti Mkombozi ambaye nilitakiwa kumkabidhi hayupo. Washitakiwa warudishwe muda wa kazi.”
Mbali na Manji, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Meneja Rasilimali watu wa Kampuni ya Quality Group Ltd, Deogratius Kisinda, Mtunza Stoo, Abdallah Sangey na Thobias Fwere mkazi wa Chanika wanakabiliwa na mashitaka ya uhujumu uchumi.
Awali, akiwasilisha maombi hayo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi alidai kuwa Mahakama iruhusu washitakiwa waweze kukabidhiwa kwa Polisi ili kutimiza matakwa ya upelelezi akisema kwa mujibu wa Kifungu cha 59 cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinawapa mamlaka Polisi kufanya upelelezi.
Akijibu hoja hizo, Wakili wa utetezi, Hudson Ndusyepo alidai Mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa amri kama ilivyoombwa na upande wa mashtaka kwa sababu shauri hilo halijapata hati ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) kuipa mamlaka Mahakama hiyo kusikiliza shauri hilo.
Ndusyepo alidai Mahakama hiyo imefungwa mikono ya kutoa amri dhidi ya maombi hayo akisema kifungu cha sheria kilichotajwa kinazungumzia ufanyaji wa upelelezi kwa ujumla.
Wakili Hajra Mungula alidai kuwa washitakiwa hao wako chini ya ulinzi na kwamba upande wa mashtaka uliwashitaki huku wakijua kwamba hawajakamilisha upelelezi na   wametoa hati ya kuzuia dhamana.
“Tunaomba ombi hili likataliwe na upande wa mashtaka waelekezwe kuzingatia sheria na  haki za washitakiwa.”
Hata hivyo, wakili Kishenyi alidai Mahakama imekuwa ikisisitiza kukamilisha upelelezi na kwamba wanachofanya ni sehemu ya kukamilisha upelelezi akisema washtakiwa hao wana haki ya kuwakilishwa hivyo maombi yao yakubaliwe.

No comments