Header Ads

Responsive Ads Here

HALOTEL TOENI HUDUMA ZOTE ZA MAWASILIANO VIJIJINI: KAMATI YA BUNGENI YA MIUNDOMBINU


Na.1
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema J. Nchimbi (wa kwanza kushoto) akiwa ofisini kwake alipotembelewa na wajumbe wa Kamati  ya Bunge ya Miundombinu wakati wa ziara yao ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini kwenye mkoa huo

Na.2
Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Willy Quambalo (wa kwanza kulia) akisisitiza jambo kwa wataalamu wa kampuni ya simu ya Halotel wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini walipokuwa kwenye kijiji cha Kijima kilichopo Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.
Na.3
Msimamizi wa kampuni ya Halotel wa mkoa wa Mwanza na Simiyu Bwana Benedict Kishusha (wa pili kushoto) akifafanua jambo mbele ya kamati ya Bunge ya Miundombinu wakati wa ziara yao ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini kwenye kijiji cha Kijima kikichopo mkoa wa Mwanza.
Na.4
Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Abbasi Hassani Mwinyi (wa pili kushoto) akisisitiza jambo wakati wa ziara ya Kamati hiyo ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini kwenye wilaya ya Manyoni mkoani Singida kwa wataalamu wa kampuni ya Vodacom (hawapo pichani).
Na.5
Msimamizi wa kampuni ya simu ya Vodacom wa Mkoa wa Dodoma Bwana Bwana Benedict Maro akifafanua jambo mbele ya Kamati ya Bunge ya Miundombinu (hawapo pichani) wakati wa ziara yao ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini katika kijiji cha Idondandoye kilichopo wilaya ya Manyoni mkoani Singida. Aliye katikati ni Mkuu wa Idara ya Uendeshaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Bwana Albert Richard.
…………..
Kamati ya Bunge ya Miundombinu iko kwenye ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa minara ya simu, ufikishaji na upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini kwenye maeneo ya vijiji mbalimbali nchi nzima ikiwa ni moja ya jukumu la Kamati hiyo ya kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ya kujenga miundombinu ili kukuza uchumi wa taifa letu, kuchangia pato la taifa na kuiwezesha Serikali kuhudumia wananchi wake.
Hayo yameelezwa na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Emmanuel Adamson Mwkasaka wakiwa kwenye ziara yao ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasikiano vijijini kwenye  kijiji cha Kijima kilichopo wilayani Misungwi mkoani Mwanza. Mhe. Mwakasaka amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imwekeza kwenye kampuni ya simu ya Halotel ili iweze kufikisha huduma za mawasiliano vijijini a kwenye maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara ili wananchi wa vijijini waweze kutumia huduma hizo na kunufaika nazo sawa na wanachi waishio mijini.
 Naye Msimamizi wa Kampuni ya simu ya Halotel wa Mkoa wa Mwanza na Simiyu Bwana Benedict Kishusha amesema kuwa Halotel ina watumiaji wachache kwenye vijiji mbalimbali nchini ambako kampuni hiyo imejenga minara na wananchi waishio maeneo hayo wana uwezo mdogo wa kiuchumi wa kutumia huduma za mawasiliano kama vile kununua muda wa maongezi ili kufanikisha azma ya Serikali ya ufikishaji na upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini. “Halotel imekuwa ikiwapatia wananchi simu za mkononi bure bila ya kuwauzia ili waweze kuwasiliana na kutumia huduma nyingine za mawasiliano,” amesema Kishusha. Ameongeza kuwa kijiji cha Kijima kina takribani ya watu 2,000 na mnara huo umewashwa na kuanza kutumika mwezi Julai mwaka 2015.
Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Emmanuel Adamson Mwakasaka ametoa rai kwa kampuni ya simu ya Halotel kutangaza  huduma zake za kutoa na kuweka fedha pamoja na kuweka mfumo wa matumizi ya data ya 3G kwani ndizo zinawavutia wananchi. Pia ameongeza kuwa waendelee kujitangaza hasa kwenye maeneo ya vijijini walikojenga minara yao ili wananchi waweze kupata huduma za mawasiliano vijijini kama vile kutuma na kupokea fedha kwa kuwa hamna huduma za kibenki kwenye maeneo ya vijijini na wananchi wanategemea huduma hiyo kupitia kampuni ya simu ya Halotel.  Pia ameongeza kuwa Halotel waendelee kutangaza  huduma zake za kutoa na kuweka fedha pamoja na kuweka mfumo wa matumizi ya data ya 3G kwani ndizo zinawavutia wananchi.
Akizungumza kwenye  ziara hiyo iliyofanyika katika Kijiji cha Kijima wilayani Misungwi mkoani Mwanza, Mjumbe wa Kamati hiyo, Mhe. Ritha Kabati amesema kuwa wananchi wengi wanahitaji huduma ya kuweka na kutoa fedha kwani ndiyo huduma muhimu kwao. Kabati alisema wananchi wengi walioko vijijini hawatambui kama Haloteli inatoa huduma ya kutoa na kuweka fedha hivyo hutumia mitandao mingine inayopatikana huduma hiyo. “Wananchi wengi waliopo vijijini hawatambui kama kuna Halopesa wanachokijua ni M-pesa wakati huduma hii ni muhimu kwa kuwa watoto, ndugu na jamaa walioko mjini huwatumia fedha kwa njia ya simu za mkononi hivyo kukosekana kwa huduma hii kunachangia watu wasiitambue,” amesema Rita Kabati.
Pia Mjumbe wa Kamti hiyo Mhe. Mussa Ntimizi alisema serikali imetoa ruzuku kwa kampuni za simu lengo ni kueneza huduma za mawasiliano hivyo baada ya ujenzi wa minara mnatakiwa kuweka promosheni mbalimbali na matangazo ya kutosha kujitangaza. “Haloteli  mtengeneze matangazo ya kutosha ili watu waitambue kwani Serikali imeweka fedha za kutosha ili wananchi wapate huduma zote muhimu. Natambua kwamba huduma ya kuweka na kutoa fedha (Halopesa) imeanza kutoa huduma lakini ipo zaidi mjini hivyo mnapaswa kuitangaza na huku vijijini,” alisema Ntimizi. Pia amesema kama ambavyo Haloteli inafanya vizuri katika masuala ya data mijini, wanapaswa kuweka huduma hiyo vijijini kwani suala la mawasiliano limekuwa hivyo wasitegemee kuwa wanakijiji hawatumii data. “Kwa sasa wananchi wanapendelea zaidi data katika mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Instagram na WhatsApp hivyo msifikiri kwa kuwa huku ni vijijini basi hawatumii hapana, mnatakiwa muweke data nzuri kisha muangalie watumiaji wako wengi kiasi gani,” alisisitiza.
Mwanakijiji wa Kijima, Bi. Hellen Michael alisema kuwa katika kijiji hicho wanatumia zaidi mtandao wa Vodacom na kwamba wengi wanatambua huduma za M-Pesa na sio Halopesa. Alisema huduma hiyo ya kuweka na kutoa fedha kwa Haloteli imeanza miezi minne iliyopita na kwamba wanakijiji wanapenda kutumia huduma hizo zaidi. “Wananchi wanafurahia na kutumia simu ya kampuni ya Halotel bali tunaiomba itoe huduma za kuweka na kutoa pesa,” amesema Bi. Hellen Michael.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Eng. Peter Ulanga amesisitiza kuwa kampuni ya simu ya Halotel itoe huduma za data kwa wananchi waishio vijiji mbalimbali walikojenga minara na sio huduma za simu za sauti tu ili wananchi waweze kupata huduma za mawsilaino ya sauti na data kupitia kampuni hiyo kama ilivyo kwa wananchi waishio mijini.
Msimamizi wa Kampuni ya Haloteli mkoa wa Mwanza na Simiyu, Bwana Benedict Kishusha alisema kuwa mnara huo uliwashwa Julai, 2015  ambao unahudumia vitongoji 23 vya kijiji hicho. Kishusha alisema changamoto mojawapo ni watumiaji wachache wa mitandao ya simu katika kijiji hicho unaosababishwa na uwezo mdogo wa  kupata huduma za mawasiliano ikiwemo ununuaji wa vocha.  Alisema wanajitahidi kuelimisha watu kutumia mtandao huo ikiwemo kufanya matangazo mbalimbali na kuwapatia bure kadi za simu na muda wa maongezi. “Huduma ya Halopesa imezinduliwa hivi karibuni na kijiji hiki kimeanza kutumia huduma hiyo miezi mitatu iliyopita.  “Katika mnara huu wanatumia data ya 2G kwani hatuwezi kuweka 3G kwa sababu watumiaji wake ni wachache hivyo  inaongeza gharama,” alifafanua Kishusha. Pia alieleza kuwa awali,  walifunga data ya 3G  lakini kijiji hicho na vingine waliona watumiaji wa simu za mkononi za kutumia data za 3G ni wachache na mfumo wao unasoma hivyo ambapo iliwalazimu kutoa huduma hiyo na kupeleka vijiji vingine na kuacha huduma ya data ya 2G ikiendelea kufanya kazi na kutumika kwenye kijiji hicho.
Naye Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya miundombinu, Mhe. Emmanuel Mwakasaka alisisitiza kuwa ni vyema kampuni hiyo kuzingatia kutoa huduma zote ili wananchi waweze kunufaika na  mawasiliano sio tu ya kuongea. Pia alizitaka  Kampuni za simu zote zinazotumia huduma za mawasiliano kote nchini kuhakikisha zinashiriki katika kusaidia  huduma za jamii. Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Haloteli mkoa wa Mwanza, Francis Mafuru alisema wanajitahidi kutoa huduma za kijamii licha ya kwamba wananchi hao wapatao 2,000 hawatumii vocha zaidi ya shilingi 500 hali inayoongeza gharama za uendeshaj wa kampuni hiyo ya simu. “Tunaamini wateja wetu wataongezeka kwani tumejipanga vizuri kuwahudumia katika masuala ya fedha na data,” alisema Mafuru.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

No comments