Header Ads

Responsive Ads Here

DC THOMAS AWATAKA WAZAZI KUWALEA WATOTO KATIKA MAADILI MEMA ILI KUEPUSHA KUJIINGIZA KWENYE VITENDO VIOVU


Na Maryam Kidiko –Maelezo Zanzibar.    
MKUU wa Wilaya ya Mjini Marina Jowel Thomas aliwataka  Wazazi  kuongeza juhudi ya kuwalea watoto wao katika maadili mazuri yatakayowaepusha   kutumbukia katika vitendo vibaya.

Hayo aliyasema katika sherehe za uzinduzi wa shehia mpya ya Kwamtumwajeni, Baraza la vijana  la shehia na kumtambulisha rasmin Sheha wa shehia hiyo Rajab Ngauchwa  zilizofanyika katika Jimbo la Magomeni.
Alisema Vijana wengi wamekuwa wakijihusisha  na vitendo viovu katika jamii jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo yao sambamba na kujijengea mfumo mbaya wa maisha yao.
Aidha aliwaomaba vijana waliojiunga na baraza la  shehiya ya Kwamtumwajeni kuchukuwa juhudi ya kuwaelimisha vijana wenzao  ndani ya shehia yao na shehia nyengine kujiunga na mabaraza ya vijana.
Aliwaeleza vijana  kuwa wanayofursa kubwa ya kujiunga katika mabaraza hayo kwani hakuna ubaguzi  kitu muhimu ni  kufuata sheria na taratibu zilizowekwa.
Mkuu wa Wilaya aliwahakikishia vijana hao kuwa Ofisi yake  ipo tayari kushirikiana nao  katika kutafuta maendeleo kwa kuanzisha  miradi mbali mbali itayoweza kuwasaidia katika kujikwamuwa na maisha.
“Wilaya yangu ipo pamoja na nyinyi hivyo ninawasihi vijana msikubali kuingizwa katika vitendo viovu vitavyosababisha kuharibikiwa katika maisha yenu na kupoteza muelekeo mzima wa maisha,”alisema Marina.
Muwakilishi wa Jimbo la Magomeni Rashid Makame  Shamsi aliahidi kuwa yupo tayari kushirikiana pamoja na vijana nakuweza kuzitatuwa chanagamoto zinazowakabili katika shughuli zao.
Aliwataka vijana wa Jimbo la Magomeni kuweza kuzitumia fursa zinazotolewa na viongozi wao za  kujifunza ujasiria mali kwani wataweza kujisaidia katika maisha yao na kupunguza idadi ya vijana wasio na ajira.
Muwakilishi  Shamsi alisema Vijana wengi wamekuwa wakijihusisha na vitendo vibaya katika jamii jambo linalorudisha nyuma usalama wao huku ukizingatia kuwa  vijana wa leo ndio nguvu kazi ya taifa lijalo katika Nchi yetu.
Sambamba na hayo aliwaomba vijana kushirikiana pamoja ili kuweza kufanya kazi za maendeleo katika jimbo la magomeni na kujikwamuwa katika mfumo mbaya wa maisha ambao unaowakabili vijana.
Katika sherehe hiyo Muwakilishi Shamsi alimkabidhi vitendea kazi vya Ofisi Sheha wa shehia ya Kwamtumwajeni na kumuahidi kushirikiana nae ili kuhakikisha anatekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Akitowa shukurani, Sheha Rajab Ngauchwa alisema yupo tayari   kushirikiana na Wananchi wote wa shehia yake bila ya kubaguwa ili kuweza kuharakisha maendeleo kwa pamoja.
Aliwataka Wananchi kufuata sheria zilizowekwa katika nchi ili kuepuka matatizo madogo madogo yanayoweza kujitokeza na kuwasihi kuendeleza hali ya usalama na amani katika jimbo hilo na jamii kwa jumla.
Alisema kuna umuhimu mkubwa wa kulinda  na kuhifadhi mazingira yanayowazunguka kwa kufanya usafi ili kujiepusha kutokea  maradhi mbali mbali ya mripuko.
Akisoma risala ya shehia hiyo, Mjumbe wa Baraza la Vijana Khadija Mgasho Mussa alisema katika shehia yao wamefanikiwa kuunda kikundi cha utunzaji wa mazingira, kuondoa vigenge vya vijana wanaohatarisha usalama wa wananchi na mali zao pamoja na kudhibiti uingiaji wa wageni kiholela.
Alimueleza Mkuu wa Wilaya kuwa shehia hiyo inakabiliwa na changamoto mbali mbali zikiwemo kukosa sehemu ya kuwekea taka, vifaa vya kufanyia usafi wa mazingira, pamoja na kukosa ofisi kwa ajili ya  Baraza la vijana na vitendea kazi.
                    
     IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR.

No comments