Header Ads

Responsive Ads Here

YANGA MWENDO MDUNDO MSIMU WA 2017-18


YANGA
Samuel Samuel
Mabingwa wa soka Tanzania bara leo wanaingia kambini rasmi kisiwani Pemba kwa ajili ya maandalizi ya fainali ya kombe la Ngao ya jamii na mwanzo wa ligi kuu Tanzania bara inayoanza mwishoni mwa mwezi huu wa nane tarehe 27.

Tarehe 23 August 2017, Yanga watakuwa uwanja wa taifa na washindi wa kombe la FA ( ASFC ) kwenye mtanange wa kugombania Ngao ya jamii. Hii ni mechi ya ufunguzi wa ligi kuu nchini inayowakutanisha watani wa jadi baada ya misimu kama minne hivi kukutana katika Ngao ya jamii.
Yanga waliokuwa kambini Morogoro kabla ya kucheza mechi tatu za kirafiki wakipoteza moja dhidi ya Ruvu Shooting na kushinda mechi mbili dhidi ya Singida United 3-2 na Mlandege ya Zanzibar 2-0; leo wanaingia kisiwani Pemba kujifua kwa mara ya mwisho kabla ya kuanza ligi.
George Lwandamina kocha mkuu wa Yanga inaonesha msimu huu atakuwa na kipaumbele cha kutumia damu changa kikosini mwake katika kuimudu mikikimikiki ya ligi kuu Tanzania bara.
Licha ya ujio wa kiungo wa timu hiyo Pappy Tshishimbi aliyesajiliwa kutoka Mbabane Swallows kusuasua mpaka sasa ; tayari muunganiko wa kinda Maka Edward aliyetoka timu B na Rafael Daudi aliyesajiliwa toka Mbeya City unaonesha kuleta uhai katika kikosi cha wanajangwani hao.
Uwezo kisoka kwa maana ya kutimiza majukumu yake kama kiungo mkabaji , nguvu, kujiamini na uelewano mzuri na wenzake unamfanya Maka Edward kusimama kama silaha muhimu kwa Lwandamina msimu wa 2017-18.
Bado Saidi Makapu anaonekana kukosa muendelezo mzuri mbele ya Maka na asipokuwa makini kinda huyo anaweza kumpoteza katika nafasi hiyo ambayo mara nyingi mkongwe Thabani Scara Kamusoko huiweka chini ya himaya yake.
Ramadhani Kabwili kijana wa miaka 18 anaonesha kuiva vyema katikati ya miamba Youthe Rostand na Beno Kakolanya. Huyu anatarajiwa kusimama kama nguzo muhimu katika kikosi cha mzambia huyo. Kipa namba moja wa kikosi hicho Beno Kakolanya anauguza majeraha ambayo aliyapata timu ya taifa hivyo ni yeye na Rostand ndio wenye dhamana ya kulilinda lango la timu hiyo.
Msimu wa 2013-14 Simba SC waliibuka na kinda Manyika Jr akiwa na umri sawa na Ramadhani Kabwili kwa sasa lakini aliweza kusimama imara kwenye kikosi cha timu hiyo . Octoba 18 2014 aliweza kulilinda vyema lango la Simba mbele ya Yanga iliyokuwa moto wa kuotea mbali kwa sare ya 0-0 hivyo sioni shida kwa Yanga kumuamini Kabwili dhidi ya mnyama huyo tarehe 23 pia kuanza nae kwenye ligi. Ni dhahiri kambi ya Pemba benchi la ufundi litatumia muda wa kutosha kumuandaa kipa huyu.
Bado Lwandamina na jopo lake wana nafasi nzuri kutetea taji lao kwa aina ya wachezaji walionao endapo umakini na maandalizi ya kutosha yatafanyika kuanzia Pemba kuja bara.
Ibrahimu Ajibu, Donald Ngoma , Amisi Tambwe , Emanuel Martini na Obrey Chirwa si safu ya kubeza kwenye forwad line ni kiasi cha kutafuta muunganiko wao mzuri kwa mbinu na mifumo watakayo tumia . Safu hii inategemea uimara na uwezo kimbinu ya viungo nyuma yao na kwenye flanks pia wing backs.
Emanuel Martin anaetumika sana kama winga wa kulia katika mechi hizi tatu za kirafiki na mazoezini kule Morogoro anaonesha kujipanga vyema msimu huu. Lwandamina anaweza kumfanya mpishi katika pacha ya Ngoma na Tambwe kulia akisimama Yahya Akilimali au Yusufu Muhilu. Ana uwezo wa kufunga kutokea pembeni pia ans uwezo wa kuwacheza washambuliaji wa kati kutokea pembeni au kuingia kati nakufanya technical screening kwa washambuliaji wa kati kufunga.
Piusi Baswita ni ingizo jipya katika kikosi cha wanajangwani hao . Ni kiungo ambaye ana uwezo mzuri kwa maana ya kipaji halisi lakini benchi la ufundi la Yanga SC linahitajika kuitumia kambi ya Pemba kumjenga kucheza mpira kwa manufaa ya timu. Kucheza mpira wa kuamua matokeo chanya kwa timu pia kulinda mifumo yote miwili ya timu ; kujilinda na kushambulia. Bado anacheza kuonesha uwezo binafsi kwa kukaa sana na mpira na kuachia wakati tayari umbo aidha la kulinda au kushambulia limevurugika.
Pia kambi ya Pemba itumike kutafuta muunganiko mzuri eneo la ulinzi wa kati. Licha ya uimara wa kiungo cha chini bado Yanga inaonesha kusumbuliwa na jinamizi la kumkosa mbadala sahihi wa Vincent Bossou. Ni rahisi kuwaamini wakongwe Kelvin Yondani na Nadir Haroub lakini wanaonesha dhahiri kuianza magharibi ya soka lao. Usalama wa eneo hilo ni mseto tu . Ni wakati wa kuwandaa vyema Pato Ngonyani, Shaibu ‘ Ninja ‘ na Andrew Vincent kuwazunguka wakongwe hao. Nadir kusimama na Dante au Yondani kusimama na Ninja itategemea na aina ya kiungo wa chini atakayesimama na mfumo wa mwalimu.
Tayari kocha mkuu wa Dodoma FC iliyopo ligi daraja la kwanza , Jamhuri Kihwelo ‘ Julio ‘ ametanabaisha ubora wa kikosi cha Yanga kwa kusema wengi wanaipa nafasi ndogo kutetea ubingwa wake lakini kwake anawaona Yanga bado wa moto.
” kwanza hawajabadili sehemu kubwa ya kikosi chao hivyo bado wana muendelezo mzuri na pia wamesajili kulingana na mahitaji hivyo wasiwazuge kuja kinyonge msimu huu hao bado wa moto ” alisema Julio.
Kauli hiyo ya Julio haipo mbali na ukweli. Yanga endapo watampata Pappy Tshishimbi kwa wakati na akaelewana vyema na wenzake hakika watasumbua kwenye ligi. Mathalani kocha kutengeneza muunganiko wa Pappy kama mlinzi wa chini, juu Kamusoko au Rafael Daudi , Ajibu 10 na tisa kusimama Ngoma hakika wapinzani inatakiwa wajipange ukitazama bado Chirwa yupo nje ingawa anaweza pia kumtumia kama mshambuliaji wa pembeni kwenye 4-3-3 au 3-4-3.
Bado Yanga ni mwendo mdundo kwa msimu wa 2017-18.
Samuel Samuel

No comments