Header Ads

Responsive Ads Here

Waziri Mwakyembe Awapongeza Vijana walioshiriki Mashindano Nchini Uganda


F0
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akisisitiza jambo wakati wa hafla fupi ya kuwapokea wanamichezo wanafunzi waliotoka kushiriki mashindano ya Shule za Sekondari za Jumuiya ya Afrika Mashariki (FEASSA) leo Jijini Dar es Salaam. Katikati ni Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Bw. Mohamed Kiganja na Mratibu wa Michezo Shule ya Sekondari Makongo Kapteni Abdul Mbaruka Tika.

F1
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akimpongeza mmoja wa mwanamichezo aliyeibuka mshindi wa tatu katika riadha  kwenye mashindano ya FEASSA, Winfrida Makenji wakati wa hafla fupi ya kuwapokea wanamichezo hao waliotoka kushiriki mashindano ya Shule za Sekondari za Jumuiya ya Afrika Mashariki (FEASSA) leo Jijini Dar es Salaam.
F2
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akipokea bendera ya taifa kutoka kwa Kapteni wa timu ya wanafunzi wa Sekondari za Tanzania walioshiriki mashindano ya michezo kwa Shule za Sekondari za Jumuiya ya Afrika Mashariki (FEASSA) katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Jijini Dar es Salaam leo.
F3
Mkuu wa Msafara wa timu ya wanafunzi wa Sekondari za Tanzania walioshiriki mashindano ya michezo kwa Shule za Sekondari za Jumuiya ya Afrika Mashariki (FEASSA) Mwl. Vitalis Shija akielezea jambo mbele ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (wapili kushoto) wakati wa hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Jijini Dar es Salaam leo. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Bw. Alex Nkenyenge na Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT). Mohamed Kiganja.
Picha na: Frank Shija – MAELEZO.
………………………..
Na Thobias Robert- MAELEZO
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amewapongeza vijana walioshiriki mashindano ya Shirikisho la Michezo Afrika Mashariki (FEASSSA) yaliyofanyika mwaka huu katika Mji wa Gulu Nchini Uganda.
Pongezi hizo amezitoa leo Jijini Dar es Salaam wakati akikabidhiwa bendera ya Taifa na vijana hao mbele ya Waandishi wa  Habari mara baada ya kurejea kutoka kwenye mashindano hayo ambayo hushirikisha timu za Shule za Sekondari za jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Nataka kuwadhitibishia Watanzania kwamba tutaenzi daima michezo ya UMITASHIMITA na UMISETA maana vipaji ndiyo vinapoanzia, niwapongeze sana vijana kwa kushinda medali nawatie moyo muendelee ili muweze kushiriki katika mashindano ya kimataifa yakiwemo Olimpiki, maana nyninyi ndiyo warithi wa Simbu na wanariadha wengine waliowahi kufanya vyema hapa nchini,” alisema Dkt. Mwakyembe.
Aidha Dkt. Mwakyembe amewaasa vijana hao wasithubutu kutumia njia zisizo halali ili kushinda, bali wajitume katika mazoezi na wawe na nidhamu ya hali ya juu kwani michezo ni ajira ya uhakika kwa vijana wengi sio tu Tanzania bali hata katika mataifa yote ulimwenguni.
“Tusisikie kabisa kelele za kwamba, unaweza ukafanya hiki au ukatumia njia za mkato, hakuna mchawi wa michezo zaidi ya mazoezi kwani huwezi kupata ushindi kwa kupitia njia za kishirikina, haiwezekani kwani hizo ni hadithi tu za abunuwasi njia pekee ni mzaoezi,” alisisitiza Dkt. Mwakyembe.
Vilevile Dkt. Mwakyembe amesema kuwa serikali imejipanga mwaka ujao itaongeza idadi ya washiriki katika mashindano yatakayofanyika Rwanda na amewasisitiza vijana pamoja na walimu wa michezo mashuleni kuendelea kuwalea vijana na kuibua vijana wengi ili kukabiliana na na tatizo la upungufu wa ajira kwani michezo imekuwa ajira ya uhakika duniani.
Kwa upande wake, Vitalis Shija Mkuu wa Msafara wa timu ya vijana iliyoshiriki mashindano hayo amesema kuwa, Tanzania ilikuwa na wanamichezo 73, katika michezo yote iliyoshiriki ikiwemo, Mpira wa miguu, kurusha vitu vizito pamoja na Riadha.
Katika michezo hiyo Tanzania imepata medali 10, kwa upande wa riadha na mchezo wa kupokazana vijiti na kushika nafasi ya tatu, lakini pia imeshika nafasi ya tatu kwa upande wa mashindano ya mpira wa miguu kwa wasichana na kuishia hatua ya robo fainali kwa upande wa timu ya wavulana.
Aidha katika medali 10 Mwanafunziu Winfrida Mkenji kutoka Shule ya Sekondari Makongo alipata medali nne, kwa upande wa riadha na mchezo wa kupokezana vijiti Mita 100, Kefleni Simon medali 1, Jane Maiga medali 2, Mary Emily medali 2, kwa upande wa mita 100 na mita 400 katika mchezo wa kupokezana vijiti pamoja na Sarah Joel medali 1 katika mchezo huohuo kwa mita 400.
“Katika mashindano hayo kuna ada ya ushiriki kwa kila nchi pia kila mshiriki anapaswa kulipiwa dola 7 kwa siku 10 kwahiyo unapopeleka idadi kubwa ya wanafunzi gharama zinaongezeka hivyo nikushukuru Waziri na Baraza la Michezo kwa kutuwezesha kuisafirisha timu na kushiriki michezo kwa siku zote,” alifafanua Bw. Shija.
Katika mashindano hayo vijana waliowakilisha nchi walitoka katika Shule za Alliance mkoani Mwanza, Simiyu katika Shule ya Sekondari Mwashilole, Dar es Salaam katika Shule ya Sekondari ya Makongo, Pwani katika Shule ya Lord Baden, Tabora katika Shule ya Sekondari Ulaya pamoja na Mkoa wa Morogoro Sekondari ya Treefarms.
Mashindano haya yamekuwa yakifanyika kila mwaka katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afika Mashariki na mwaka huu yamefanyika katika mji wa Gulu Uganda, kwa udhamini wa kampuni ya Brokeside ambapo Uganda ilikuwa na washiriki 1045, Kenya 840, Rwanda 650, Burundi 380, Sudani Kusini 150 na Tanzania washiriki 73.

No comments