Header Ads

Responsive Ads Here

WANAOLALAMIKA KUFELI USAILI WA AJIRA SERIKALINI WANATIMIZA VIGEZO?

Na: Agness Moshi –MAELEZO.
Si jambo geni kusikia watu wakiilalamikia Serikali kufeli usaili wa ajira za serikalini kupitia Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira Katika Utumishi wa Umma,jambo ambalo limesababisha baadhi ya watu kudhani kuwa mamlaka hiyo inafanya kazi kwa upendeleo.

Sekretarieti ya ajira katika utumishi wa umma kwa niaba ya serikali inahakikisha wale wote wenye vigezo vya kupatiwa ajira katka serikali wanapata ajira kwa utaratibu maalum uliowekwa bila kumpendelea mtu.
Serikali ya awamu ya Tano chini ya Dkt.John Pombe Magufuli imefanya jitihada mbalimbali  za kuhakikisha Wanachi wake wanapata fursa za ajira ikiwa ni pamoja na kutangaza ajira zaidi ya 52,000 kwa mwaka wa fedha  2016/2017 ambapo  imekua ikitekeleza ahadi hiyo kwa kutoa vibali vya kuajiriwa watumishi mbalimbali kulingana na mahitaji.
Kwa mujibu wa Sekretarieti ya Ajira Katika Utumishi wa Umma, Vibali 239 vya ajira  viliwasilishwa kutoka Taasisi mbalimbali na Mashirika ya umma  na baadhi ya vibali hivyo vimekwishwa fanyiwa kazi ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA),Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), Wakala wa Serikali wa Mtandao(e-Ga), na Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS).
Kupitia vibali hivyo waombaji 56,815 walituma maombi yao kupitia mfumo wa uwasilishaji kwa njia ya kielektroniki ‘Recruitment Portal’ ambapo yalifanyiwa kazi na waombaji takribani 29,674 tu ndio waliokidhi vigezo vya tangazo husika na hivyo kuitwa kwenye usaili.
Kwa Takwimu hizo  tunaona  karibu nusu ya waombaji hao hawakupata nafasi hata ya kufanya usaili, jambo ambalo limekua gumzo mitaani kwani waombaji waliokosa nafasi za usaili  hudhani  sekretarieti inafanya uchaguzi kwa upendeleo kitu ambacho si sahihi kwani mamlaka hiyo inafanya kazi kwa kufauata vigezo na masharti.
Serikali inaendeshwa kwa Sheria,  Kanuni na taratibu zilizowekwa kwenye katiba ambayo haina ubaguzi kwa mwananchi yoyote katika kuleta maendeleo vivyo hivyo utoaji ajira  hauna upendeleo ukiwa na vigezo utakuchukuliwa na kufanya usaili, sikatai baadhi ya waombaji kukosa nafasi za usaili lakini je wanatimiza vigezo na masharti yanayowekwa na Taasisi husika wakati wa matangazo ya ajira hizo?
Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano na Msemaji wa Sekretarieti ya Ajira Kwa Utumishi Wa Umma Riziki Abraham amesema mchakato wakuchagua waliokidhi vigezo kwaajili ya usaili una changamoto mbalimbali ambazo zinasababishwa na waombaji wenyewe hivyo kupelekea kukosa nafasi za kufanya usaili kutokana na kutokidhi vigezo vya ajira husika.
“Waombaji wengi hawazingatii masharti wanapotuma maombi,wengine wanatoa taarifa za uongo, kweli kuna mapungufu mengi kwa waombaji  lakini kwa wale wenye sifa na wanaozingatia vigezo vya ajira husika huwa tunawaita kwa ajili ya usaili na endapo watafaulu tunawapangia kazi kwenye vituo husika kwa mujibu wa sheria”, alisema Riziki.
Aliyataja baadhi ya mapungufu ya waombaji hao ikiwa ni pamoja na kutofahamu kuandika barua za maombi ya kazi, kutothibithisha nyaraka zao hususani kwa waliosoma vyuo vya nje, kutokuambatanisha nyaraka zao za elimu, kutozingatia vigezo vilivyoainishwa ikiwemo kudanganya baadhi ya taarifa, kuandika wadhamini wachache badala ya kuandika idadi kamili.
Aliongeza kwa kusema badhi ya waombaji hao huwasilisha maombi kwa njia tofauti na ile iliyoelekezwa kwenye tangazo na hivyo kusababibisha maombi yao kutofika kwa wakati. Pia waombaji hao wamekua wakipakia taarifa ambazo si sahihi ikiwa ni pamoja na kupakia vyeti visivyokamilika kama vile “Transcipts,result slip,progress report na particial transcript”.
“Wale ambao hawazingatii maelekezo kikamilifu mara nyingi hukosa fursa za kuitwa kwenye usaili na hatimaye kusababisha malalamiko”, alisema Riziki.
Aidha Riziki amesisitiza kuwa, waombaji wajitathmini wenyewe kwanza kabla ya kutuma maombi hayo kwa kuzingatia vigezo  vilivyoanishwa kwenye tangazo husika na  endapo watatakiwa kuwasilisha picha za utambulisho ‘Passport size’ wazingatie mfumo wa kuwasilisha picha hizo,madhari iliyotumika na aina ya picha wanazotuma.
Kwa upande wake Katibu Msaadizi wa Sekretarieti ya Ajira Kwa Utumishi Wa Umma Malimi Muya ametoa rai kwa waombaji wenye changamoto zozote ikiwa ni pamoja na walemavu kuzitaja changamoto zao kwenye maombi ili endapo watapata nafasi za kufanyiwa usaili  waweze kuandaliwa mazingira rafiki.
“Ni vyema kama kuna mtu anachangamoto asisite kueleza kwenye fomu ya maombi, hii itatusaidia sisi katika kuhakikisha tunamuandalia mazingira ambayo ni rafiki kwake  na endapo atafaulu usaili itatusaidia pia kumpangia ajira sehemu ambayo itamfanya afanye kazi kwa amani”, alisema Malimi.
Hata hivyo, Malimi amesema mwitikio wa walemavu katika mchakato wa ajira bado ni mdogo na hata wanaoomba huwa hawataji changamoto zao kwa kuhofia kutopatiwa nafasi hizo jambo ambalo si sahihi kwani Sheria namba 9 ya Ajira ya mwaka 2010 inasema “Mwajiri yoyote awe taasisi za Umma au Binafsi mwenye waajiriwa kuanzia 20 na kuendelea lazima asilimia 3 ya waajiriwa hao iwe kwa ajili ya watu wenye ulemavu”.
Aidha, Serikali inawapa kipaumbele walemavu wanaojitokeza kuanzia wakati mchakato wa usajili unaanza kwa kuhakikisha wanahudumiwa kulingana na changamoto zao kama vile kuwaongezea muda wakati wa usaili, kuwatafutia wataalam wa mawasiliano na kuwaandalia mazingira rafiki kwani inatambua nafasi yao katika kuchangia maendeleo.
Ni matumaini yangu wahitimu ambao wanatarajia kuomba ajira  watazingatia vigezo na masharti yanayowekwa kwa kusoma tangazo lilitolewa badala ya kukurupuka kujaza fomu kwasababu tu wamepata matangazo hayo kupitia simu au mitandao ya kijamii ambayo kwa kiasi kikubwa inatumika katika usambazaji wa taarifa hizo.
Nawasihi waombaji watambue kuwa soko la ajira kwa sasa ni laushindani mkubwa na linahitaji mwombaji aliyejiandaa vizuri na mwenye uwezo wa kulitumikia Taifa kwa ufanisi mkubwa na weledi ili aweze kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu Ya Tano.

No comments