Header Ads

Responsive Ads Here

TUWASA YATUMIA ZAIDI MILIONI 100 KUFANYA MAJI YAWE SAFI NA SALAMA KWA SABABU YA UPUNGUFU KATIKA BWAWA LA IGOMBE.

 

Na Tiganya Vincent
RS-Tabora
25 August 2017
BAADA ya maji katika Bwawa la Igombe kupungua kwa mita 400 kutoka katika kingo zake hadi yalipo maji hivi sasa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Tabora Mjini (TUWASA) inatumia kiasi cha milioni 103 kwa mwezi kwa ajili ya dawa za kusafishia matope na uuaji wadudu kwenye maji ili yaweze kutumiwa na wateja wao.

Kauli hiyo imetolewa jana mjini Tabora na Meneja wa Biashara wa TUWASA Bernard Biswalo wakati wa ziara ya waandishi wa habari walipotembelea Bwawa hilo kujionea hali halisi ya maji na uharibifu uliopelekea upungufu wa maji katika eneo hilo.
Alisema kuwa kiasi hicho fedha kinazidi za awali ambapo walikuwa wakitumia shilingi milioni 50 kununulia dawa za usafishaji na milioni 8 kwa ajili dawa uuaji wa wadudu katika maji ili yawe safi na salama.
Biswalo aliongeza kuwa matumizi hayo ni nje ya gharama za umeme kwa ajili uzalishaji wa maji ambazo zinaanzia milioni 75 hadi 90 kwa mwezi.
Alisema kuwa licha ya msimu uliopita kuwa na upungufu wa mvua , tatizo kubwa lililosababisha upungufu wa maji ni baadhi ya watu wanaondesha  shughuli za kilimo za mazao mbalimbali ikiwemo mboga mboga pembezoni mwake na ulimaji wa zao la mpunga katika njia za maji na kuyazuia yasiingie ndani yake.
Biswalo alisema upungufu huo umesababisha kina cha maji kupungua kutoka kiwango kilichotakiwa cha futi 5 badala yake sasa hivi sasa kuwa chini ya futi 2 na hivyo kubaki tope.
Alisisitiza kuwa uwepo wa tope jingi umesababisha ugumu kwa Mamlaka hiyo kutoa huduma hiyo kwa wingi kwa wateja wake na  gharama za uzalishaji wa maji kwa ajili ya wakazi wa Manispaa ya Tabora.
“Upunguaji wa maji katika Bwawa la Igombe umesababishia Mamlaka yetu ugumu wa kutoa huduma ya maji kwa wananchi kama walivyokuwa wamezoea… hata maji tunayotoa hivi sasa yanatoka  katika mazingira magumu na kwa kutumia gharama kubwa kuliko maji yanavyokuwa mengi bwawani”alisema Meneja huyo.
“Hivi tunalazimika kutoa maji kwa gharama kubwa ili maji yawe safi na salama ili wananchi waweze kuyatumia bila kupata matatizo yanayotokana na maji” alisema Biswalo.
Aliongeza kuwa kwa hali ilivyo hivi sasa hakuna jinsi wakazi wa Manispaa ya Tabora watakavyoweza kuepuka mgawo wa maji na kuongeza kuwa Mamlaka inachofanya hivi sasa ni kuchukua maji kidogo dogo na kuyatibu ili yaweze kutumika kuwasaidia wateja wao.
Aliwaomba wakazi wa Manispaa ya Tabora kuwa wavumilivu wakati wakisubiri msimu wa mvua kati ya Mwezi Oktoba au Novemba ambapo tatizo la mgawo wa maji linaweza kuondoa au kupungua.
Aidha Biswalo alisisitiza kuwa jiitihada za makusudi wadau wote zinahitajika ili kuepusha tatizo hilo la upungufu wa maji katika Bwawa la Igombe kuendelea kwa wakupamba na watu wote wanaoendesha kilimo katika chanzo hicho na njia za kuingizia maji.
Alisema kuwa wakati wakazi wa Manispaa ya Tabora wakisubiri mradi wa maji ya Ziwa Victoria ni vema viongozi wa vijiji hadi mkoani wakashirikiana katika kukabiliana na wavamizi ya maeneo ya Bwawa.

No comments