Header Ads

Responsive Ads Here

TPA YATOA MSAADA WA MASHUKA 900 KWA HOSPITALI ZA WILAYA YA TEMEKE


Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Felix Lyaviva (wanne kushoto) akishukuru kupokea msaada wa Mashuka 900 yenye thamani ya Tshs Milioni 10 kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko (watano kushoto)
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Felix Lyaviva (wapili kushoto) akishukuru kupokea msaada wa Mashuka 900 yenye thamani ya Tshs Milioni 10 kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Eng Deusdedit Kakoko (watatu kushoto).

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imetoa msaada wa mashuka 900 yenye thamani ya Sh. Milioni Kumi kwa Hospitali za Temeke, Mbagala Zakheim na Round zilizopo katika Wilaya ya Temeke.

Msaada huo umekabidhiwa leo na Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko kwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Felix Lyaviva ikiwa ni sehemu kutambua na kuthamini dhamira na kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. John Pombe Joseph Magufuli, ya kufikisha huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi wote na hasa wa hali ya chini.

“Menejimenti ya TPA, chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Bodi ya Wakurugenzi ya TPA, inaunga mkono kwa dhati kabisa juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano za kuhakikisha jamii inapata huduma muhimu, TPA inayo Sera ya Misaada kwa Jamii ambayo imejikita katika kusaidia jamii kwenye nyanja za Afya, Elimu na Maendeleo ya Kijamii,” amesema Mhandisi Kakoko.

Mhandisi Kakoko ameongeza kuwa pamoja na kwamba TPA kazi yake kubwa ni kuhudumia shehena mbalimbali zinazopita kwenye bandari zote nchini, lakini pia ina wajibu wa kurudisha kile inachokipata kutokana na huduma zake kwa kuisaidia jamii inayoizunguka na ndio maana imeamua kutoa msaada huo kwa Wilaya hii ya Temeke ilipo Bandari ya Dar es Salaam ambayo kiutendaji ndiyo bandari kubwa kuliko bandari zote hapa nchini.

Hivi karibuni Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alizindua rasmi kuanza kwa kazi ya maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam na mara itakapokamilika mwaka 2022 itaiwezesha bandari hiyo kuhudumia meli zenye uwezo wa kubeba kontena 8,000 kutoka kontena 2,500 za sasa na kuiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya ushindani na kuliongezea Taifa mapato. 

No comments