Header Ads

Responsive Ads Here

TIGO YAMKABIDHI MKUU WA TABORA KISIMA CHA MAJI SAFI SALAMA KITAKACHOWAHUDUMIA WAKAZI ZAIDI 250 WA USONGELANI


Na Tiganya Vincent
RS-TABORA
22 AGOSTI 2017
Wakazi wa Usongelani wilayani Urambo wameondokana na tatizo ya maji safi na salama baada ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri kuzindua kisima chenye uwezo wa kuhudumia watu zaidi 250.

Kisima hicho kilichochimbwa na Kampuni ya Simu za Mkononi ya TIGO kwa thamani ya shilingi milioni 18 kinauwezo wa lita 2000 za maji kwa muda wa saa moja.
Akiongea mara ya kuzindua kisima hicho jana wilayani Urambo Bw. Mwanri aliwaagiza wananchi kuhakikisha wanatunza miradi yote ya maji inayojengwa katika maeneo yao ili kuifanya iwe endelevu na iweze kutoa huduma ya maji safi na salaama kwa muda mrefu.
Bw. Mwanri aliwaambia wanakijiji wa Usongelani wasipoweka uongozi makini katika kusimamia Kisima hicho kilichojengwa watarudi katika hali yao ya awali ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji na wakati mwingine kuugua magonjwa ya tumbo kutokana  na matumzi ya maji yasiyo salama.
Aliwataka wakazi wa Kijiji hicho kuhakikisha watu wote wanachangia fedha kwa ajili ya uendeshaji na usimamizi wa kisima hicho kwani gharama iliyopendekezwa ni kidogo.
Naye Mkurugenzi wa TIGO Kanda ya Ziwa  Ally Maswanya alisema Kampuni ya Tigo itaendelea kushirikiana na Serikali katika kutatua shida mbalimbali za wananchi ikiwemo utatuzi wa uhaba wa maji.
Alisema uchimbaji wa kisima hicho chenye thamani ya shilingi milioni 18 ni sehemu ya mipango mikakati ya kampuni ya Tigo ya kuwekeza katika huduma za jamii zenye mchango mkubwa katika kuboresha afya, uchumi na hali ya maisha ya wananchi.
Alisema kuwa hadi kufikia sasa wameshachimba  na kukabidhi jumla ya visima 20 kwa vijiji mbali mbali ambapo maji yanawanufaisha  zaidi ya wananchi laki moja na themanini na saba elfu (187,000) nchini kote.
Mkurugenzi huyo aliongeza wana mipango ya kuchimba visima vingine vitakavyowafikia zaidi ya Watanzania laki tatu na nusu(350,000) kote nchini.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Urambo Angelina Kwingwa alisema uzinduzi wa Kisima hicho kimesaidia kuwatua ndoo wanawake na watoto ambao walikuwa wakitembea mwendo mrefu na wakati mwingine kukesha kutafua maji.
Alisema kuwa muda waliokuwa wakiutumia kutafuta maji watautumia katika kutafuta maji , watautumia kufanya shughuli nyingine za maendeleo.
Kwa upande wa Mkazi wa Kijiji hicho Johary Said alisema kuwa mradi huo utawasaidia kuokoa fedha nyingi ambazo walikuwa wakilazimika kutumia katika ununuzi wa maji ambapo kwa lita ishirini ya maji walilazimika kulipa shilingi 500.
Alisema kuwa mradi utawasaidia kupata lita 500 kwa kwa kiwango hicho hicho cha pesa kwa sababu lita 20 itauzwa kwa kiwango cha shilingi 20.
Johari alisema kuwa mradi huo ni ukumbozi kwao na utaimarisha afya zao kutokana na matumizi ya maji safi na salama.

No comments