Header Ads

Responsive Ads Here

TIC Yawainua Wajasiriamali Wadogo


Geoffrey-Mwambe
Na Georgina Misama
Serikali kupitia Kituo Cha Uwekezaji Tanzania (TIC) inaratibu mpango wa kuwawezesha wawekezaji wadogo kukua kibiashara.

Akiongea hivi karibuni katika kipindi cha TUNATEKELEZA kinachorushwa na TBC1, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Geoffrey Mwambe alisema kwamba katika kutekeleza mpango huo Shirika limeingia makubaliano na Shirika la Biashara na Maendeleo Duniani (UN-UNCTAD) kutoa mafunzo kwa wajasiriamali.
“TIC inatoa mafunzo kwa wajasiriamali wetu wadogo na kuwaunganisha na wawekezaji kutoka nje ya nchi ili waweze kutoa huduma bora na kufaidika na uwekezaji”, alisema Mwambe.
Awamu ya kwanza ya mafunzo hayo TIC imeshirikiana na Benki ya Posta (TPB) ambapo walitoa mafunzo kwa baadhi ya wajasiriamali na kuwaunganisha na wawekezaji wa NAKUMAT Supermarket ili waweze kukuza biashara zao.
Mwambe alieleza kuwa mafunzo hayo ya wajasiriamali yanalenga kuwajengea uwezo wa namna ya kutambua mikataba, kutafuta masoko na kutengeneza bidhaa zenye ubora unaotakiwa.
Akizungumzia fursa za uwekezaji kwa Watanzania, Mwambe alisema kuwa wazawa wamepewa upendeleo ambapo kiwango cha chini cha mtaji wa kuwekeza ni dola laki 1 tofauti na wawekezaji wa nje ambao kiwango chao ni dola laki 5.
Vilevile TIC imejipanga vema kuhakikisha wawekezaji wa kutosha wanapatikana katika sekta ya viwanda hasa vitakavyotumia bidhaa za kilimo ili kupanua wigo wa soko kwa wakulima wa ndani.
Aidha Mwambe ametoa wito kwa wawekezaji wageni na wazawa kutumia fursa za kuwekeza zilizopo kwenye maeneo mbalimbali kote nchini.
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kilianzishwa mwaka 1997 kwa lengo la kutambua fursa za uwekezaji, kuratibu na kuhamasisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
TIC inashughulika na maeneo yote ya uwekezaji isipokuwa Sekta ya Madini, Sekta ya Uchimbaji na Utafutaji wa Petroli na bidhaa zake pamoja na Kemikali zenye athari mbaya kwa binadamu.

No comments