Header Ads

Responsive Ads Here

TANZANIA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA BARAZA LA MAWAZIRI LA NCHI ZA UMOJA WA MASHARIKI NA KUSINI MWA AFRIKA KUJADILI UDHIBITI UTAKASISHAJI FEDHA HARAMU


KIKAO CHA BARAZA LA MAWAZIRI LA NCHI ZA UMOJA  WA MASHARIKI NA KUSINI MWA AFRIKA WA UDHIBITI UTAKASISHAJI  FEDHA HARAMU (ESAAMLG).
Baraza la Mawaziri kutoka Umoja wa Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika wa Udhibiti Utakasishaji Fedha Haramu “The Eastern and Southern Afrika Anti Money Laundering Group – ESAAMLG”, litakutana Tanzania tarehe 08 Septemba 2017, katika ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort, Visiwani Zanzibar.

Aidha, mkutano huo utatanguliwa na Mkutano wa Maafisa Waandamizi (Makatibu Wakuu) utakaofanyika kuanzia tarehe 02 – 06 Septemba, 2017 katika ukumbi wa Hoteli hiyo ya Zanzibar Beach Resort.
Kwa sasa Tanzania ndio Mwenyekiti  wa Umoja huo kwa kipindi cha mwaka mmoja, baada ya kupokea Uenyekiti kutoka Jamhuri ya Zimbabwe iliyomaliza muda wake mwezi Agosti, 2017, ambapo Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. PHILIP ISDOR MPANGO (MB), ambae pia ni Mwenyekiti “President of the Council” ataongoza Mkutano huo.
Katika Mkutano huo, pamoja na masuala mbali mbali yatakayojadiliwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, itatumia fursa hiyo  kuwasilisha Taarifa ya hatua iliyofikia katika utekelezaji wa Mpango wa “Financial Action Task Force” (FATF) ulioasisiwa mwaka 2009.
Mpango huo ulizitaka nchi wanachama kufanya  Tathmini ya utekelezaji wa maazimio yaliyoainishwa kwenye FATF, katika maeneo mbalimbali ya Kisheria, Kisera, Miongozo ya Kitaasisi zikiwemo  Sekta za Fedha na maeneo ya ushirikiano wa kimataifa.  Lengo ni kubaini jinsi nchi wanachama  zilivyojipanga katika kudhibiti suala la Utakasishaji Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi (Anti-money Laundering and Combating the Financing of Terrorism).
Katika mkutano huo, mbinu na mikakati mbali mbali itakayosaidia kudhibiti Utakasishaji Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi itajadiliwa, hatua ambayo italeta matokeo chanya na kuongeza kasi ya ukuaji wa Uchumi na kufikia maendeleo tarajiwa katika Nchi yetu na nchi wanachama kwa ujumla.
Tanzania ni miongoni mwa Nchi waanzilishi wa Umoja huo ulioasisiwa jijini Arusha,  mwaka 1999, Nchi nyingine ni  Uganda, Kenya, Mauritius, Namibia, Sychelles na Swaziland ambazo zilisaini makubaliano (Memorandum of Understanding – MOU). Hatua ambayo ilisababisha Makao Makuu ya Sekretariati ya Umoja huo wenye nchi wanachama (18) ambazo ni Angola, Botswana, Ethiopia, Kenya, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Rwanda, Afrika Kusini, Swaziland, Sychelles, Tanzania, Uganda, Zambia na Zimbabwe  kuwa jijini  Dar es Salaam Tanzania.
IMETOLEWA NA:
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO.

No comments