Header Ads

Responsive Ads Here

RC TABORA AWAONYA WA-MADED WANAOWAWEKEA VIKWAZO MAMENEJA WA TARURA


RC1
Na Tiganya Vincent
RS-TABORA
SERIKALI Mkoa wa Tabora imewaonya Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri na Watendaji wengi kuacha mara moja kuwawekea vikwazo  Mameneja Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania(TARURA) ambavyo vinawafanya washindwe kutekeleza majukumu yao ya kuendeleza miundo mbinu ya barabara za vijijini kwa wakati na hivyo wananchi kuendelea kusafiri katika barabara mbovu.

Kauli hiyo ilitolewa jana mjini Tabora na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri  kwenye kikao kazi cha Mameneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini Tanzania(TARURA) wa mkoani humo wakati akijibu malalamiko mbalimbali yaliyatoa kwake dhidi ya watendaji wa Halmashauri kuwakwamisha.
Alisema kuwa Mkurugenzi Mtendaji yoyote atakayewakwamisha Watumishi hao ajue amewadharau viongozi wa juu waliowatuma kazi Mameneja hao ya kuwaboreshea barabara wananchi wa vijijini na kwa nafasi yake  hayuko tayari kuona hilo linatokea.
Mwanri aliongeza kuwa Wakurugenzi Wote na Watendaji wengine wanatakiwa kuhakikisha kuwa Mameneja na watumishi wengine wa TARURA wanayo maeneo ya Ofisi ya kufanyia kazi, Vyombo vya Usafiri na Madreva wa kuwapeleka maeneo ya kazi.
Alisema kuwa kitendo ambacho kimeanza kuonyeshwa na baadhi ya Watendaji wa Halmashauri kuwanyima Vyombo vya Usafiri na Madreva hawezi kukifumbia macho na atayebainika atamchukulia hatua kali.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka Watumishi wa TARURA kutojifungia Maofisini badala yake watumie muda mwingi katika kutembelea na kuzijua barabara zote zinazowahusu ili kuandaa mpango kazi wa kuziboresha.
Awali baadhi ya Mameneja hao kutoka Halmashauri za Mkoa wa Tabora walieleza kuwa baadhi ya Wakurugenzi Watendaji wamekuwa wakiwawekea vikwazo pindi wanapotekeleza majukumu yao kwa mujibu barua ya uteuzi waliyopata.
Baadhi ya vikwazo ni pamoja na kunyima magari na wanapopata magari wanang’anywa madreva wanaokuwa wamepangiwa kuwahudumia na wakati mwingine kutopangiwa maeneo ya kuendeshea shughuli zao za kiofisi.
Vikwazo vingine kushindwa kupewa taarifa ya makabidhiano kama wakurugenzi hao walivyoagizwa.
Akitoa ushauri wa uboreshaji utendaji kazi Meneja wa Wakala  wa Barabara nchini (TANROADS)  mkoani Tabora  Mhandisi Damian Ndabalinze aliwashauri Mameneja wa TARURA kuwa milango iko wazi wakihitaji msaada wasisite kuwaomba ushauri ili waweze kutekeleza kazi kwa kiwango bora na kinacholingana na fedha.
Meneja huyo wa Mkoa alisema kuwa wako tayari kuwasadia  kitaalumu wakati ambao bado hawana vifaa vya kutosha ikiwemo vile vya maabara kwa ajili ya upimaji wa udongo na uimara wa madaraja wanayokusudia kujenga ili waweze kutoa kazi nzuri.
Alisema kuwa wakati wanatekeleza majukumu yao hayo ni vema wakazingatia hifadhi za barabara ili kueepuka wananchi kujenga katika maeneo hayo.
Mhandisi Ndabalinze aliongeza kuwa wakati wanatekeleza majukumu yao kwa kuandaa mipango yao kwa kuzingatia vipaumbe katika ujenzi wa barabara.

No comments