Header Ads

Responsive Ads Here

RC NDIKILO-WAWEKEZAJI NENDENI MKAWEKEZE KIBITI/RUFIJI HALI SASA SHWARI


IMG_20170830_100038
Mkuu wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo , akizungumza na wawekezaji na viongozi mbalimbali wa serikali na wawakilishi kutoka taasisi zinazoshughulikia masuala ya uwekezaji na ujenzi wa viwanda,katika mkutano aliofanyika katika ukumbi wa mkuu wa mkoa hu.
Picha na Mwamvua Mwinyi


Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
MWENYEKITI wa ulinzi na usalama mkoani Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo amewataka wawekezaji wenye dhamira ya kuwekeza wilayani Kibiti,Rufiji na Mkuranga waende kuwekeza na waondoe hofu kwani kwasasa hali ni shwari.
Aidha amewasihi baadhi ya wananchi na viongozi mbalimbali waliohama wilayani humo kwa kuogopa hali ya sintofahamu iliyokuwepo warejee kuendelea na shughuli zao.
Akizungumza katika  mkutano uliojumuisha wawekezaji wa mkoani Pwani,wakuu wa wilaya,wakurugenzi, wawakilishi kutoka Tanesco,Dawasco na taasisi mbalimbali ,mhandisi Ndikilo aliwahakikishia wawekezaji hao ulinzi na usalama wa mali zao.
Alieleza kuwa ,hivi karibuni kulikuwa na hofu na shaka kwa baadhi ya wawekezaji na wananchi kwa hali ya usalama wao hasa katika wilaya ya Rufiji na Kibiti.
Mhandisi Ndikilo,alibainisha ,wanashukuru mambo ya kiuhalifu na mauaji yaliyokuwa yameshamiri yamepungua kama sio kuisha hivyo kila mmoja aendelee na majukumu yake ya kumuinua kiuchumi.
Alisema kwamba,vyombo vya dola vimefanikiwa kupambana na vitendo vya mauaji vilivyokuwa vikitishia usalama wa watu .
“Askari na vijana wetu pamoja  na kuanzishwa kanda maalum wapo vizuri na wana ari ya kudhibiti vitendo vyote vinavyoashiria uvunjifu wa amani”
“Nichukue nafasi hii kutoa uthibitisho baada ya IGP kueleza hali ya Kibiti hivi karibuni kuwa ni salama,”
“Nami nasisitiza kama mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama mkoa vyombo vya dola vimefanikiwa kudhibiti waliokuwa wanaua ovyo,hivyo wananchi walioondoka warudi “alisema mhandisi Ndikilo. .
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo ambae pia ni mkuu wa mkoa wa Pwani,mkoa upo shwari chini ya usimamizi wa makamanda wawili waliopo ambao ni wa kanda maalum Rufiji Onesmo Lyanga na kamanda wa jeshi la polisi mkoani hapo Jonathan Shanna.
Alisema kama hakuna amani na utulivu adhma ya kuwa ukanda wa viwanda na uwekezaji haitoweza kufanikiwa.
Nae kamanda wa kanada maalumu Rufiji,kamishna msaidizi mwandamizi Onesmo Lyanga,alisema wananchi wanapaswa waelewe kilichopigwa marufuku ni kutumia usafiri wa pikipiki saa 12 jioni.
Usafiri huo hauruhusiwi kuanzia muda huo na sio watu kuacha kuendelea na shughuli zao za kibiashara ama kutembea.
Kamanda Lyanga ,alieleza anashangaa kuona na kusikia baadhi ya watu wakisema wananchi wamekatazwa kutembea saa 12 jioni jambo ambalo sio la kweli kilichokatazwa kwa muda huo ni pikipiki.
Alisema wanaendelea kushirikiana na wananchi vizuri na amewaomba endapo kuna jambo ama viasharia vya kiuhalifu wasisitize kutoa taarifa polisi.
Kamanda Lyanga,aliwatoa hofu watu wote wanaofanya shughuli zao kwenye wilaya hizo kutokuwa na wasiwasi ,ulinzi umeimarishwa .

Matukio mbalimbali ya mauaji na kiuhalifu yanadaiwa yalianza mwaka 2015  katika wilaya hizo,ambapo yamepoteza viongozi mbalimbali wakiwemo wa vijiji,vitongoji na askari polisi kadhaa,na sasa kuonekana matukio hayo kukoma.

No comments