Header Ads

Responsive Ads Here

RAIS DKT,MAGUFULI APONGEZWA KWA UPATANISHI


 mqdefault
Na Judith Mhina – MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, John Pombe Magufuli amepongezwa na viongozi wa Dini 170 kutoka Tanzania na Kenya katika suala zima la upatanishi.

Pongezi hizo zimetokana na kitendo cha Rais kuwapatanisha   Mkuu wa Mkoa Dar-es-Salaam, Mhe. Paul   Makonda na mmiliki wa Kituo cha Televisheni na Redio cha Clouds Bw, Ruge Mutahabwa, kuwa ni kielelezo cha kuigwa na Wakenya mara baada ya kukamilika kwa uchaguzi wao.
Akiongoza maombi hayo maalum, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maadili na Amani  kwa  Maaskofu na Maashekhe  nchini Tanzania Askofu William Mwamalanga na viongozi wa  Dini wa kutoka Kenya na Tanzania, walipiga kambi ya   kuombea uchaguzi Mkuu nchini Kenya  kwa  muda wa mwezi mmoja Bunju nje kidogo ya Jiji la Dar-es-Salaam.
Akifunga  maombi hayo na kuwaaga   viongozi wa dini na vijana kutoka Kenya   Askofu William Mwamalanga amesema; Kitendo cha Rais John Magufuli kumpatanisha Ruge Mutahabwa na   Paulo Makonda ni cha kishujaa na muhimu kuigwa na Kenya ili wapatane kwa kuwa uchaguzi umekwisha, haingii akilini kuendelea na maisha ya chuki ugomvi na malumbano ambayo yaweza kuleta utengano.
Akiwasihi kwa msisistizo washiriki kutoka Kenya  amesema; “Nendeni Kenya  mkawe wapatanishi wa kweli mwambieni Mheshimiwa Raila Odinga  na wote ambao wamekosa uongozi katika uchaguzi huo, waridhie matokeo na kujumuika kama raia wema kuijenga Kenya mpya.
Akisisitiza jambo hilo, Askofu ameomba watu wote Kenya wajipatanishe  nafsi zao na MUNGU  ili kuijenga kenya kwa ajili ya ustawi wa wakenya wote bila ubaguzi.
Katika kuthibitisha upatanishi uliofanywa na Rais Magufuli, Askofu Mwamalanga alipiga simu kwa Bw, Ruge ambaye amesema; “Nimefurahishwa sana na hatua ya Rais Magufuli ya kutupatanisha, nimepokea kwa’ furaha hakika ni kazi njema ambayo inatakiwa kuungwa mkono na jamii yote. Hakuna sababu kuishi kwa chuki zisizo na maana, naomba niwashukuru Maaskofu kwa kunipongeza”.
Naye Shekhe Abrahamani Mohamed aliyeshiriki ibada hiyo amesema; “Bw, Ruge Mutahabwa ni mtu aliyekomaa kisiasa, ana hekima, na mwenye upeo mkubwa wa fikra. Hivyo nawasihi vijana wa Tanzania na Kenya kuiga mfano huo maana haipendezi kuishi kwenye maisha ya chuki”.
Chuki ni kikwazo cha maendeleo tunaomba upatanisho wa Rais Magufuli  uendelee  kwa watu wengine wanaishi  na maisha  ya kuchukiana na sisi viongozi wa kiroho tuwe mfano wa kupatana wenyewe”. Amesema Shekhe Abrahamani.
Maombi hayo na Dua  yaliongozwa na Askofu Mwamalanga na kuhudhuriwa na vijana 400 wakristo kutoka  Vyuo vikuu vya Tanzania na wanawake 283, kutoka Kenya, na wanawake 500 kutoka  Tanzania. Aidha, kulikuwa na washiriki wake kwa waume kutoka  Marekani 3   Uingereza, 5  Malawi, 6,  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo 15, Zambia 7,  Uganda 2  na Israel 2.
Maombi hayo yalimalizika kwa kurejea kitabu cha Mathayo 5 msatari wa 9 nanukuu; “Heri wapatanishi maana hao wataitwa wana wa Mungu. Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki maana ufalme wa mbinguni ni wao”.

No comments