Header Ads

Responsive Ads Here

PlanRep Kuwaleta Pamoja Wananchi na Watoa huduma


1B
Mmoja wa Wawezeshaji wa Mafunzo ya Mfumo wa kielektroni ulioboreshwa ambao ni wa Kitaifa utakaosaidia kupanga bajeti, mipango na kutoa ripoti (PlanRep) yanayoendelea mjini Kigoma Bw.  Jocktan Bikombo akiwasilisha mada wakati wa mafunzo hayo.

2B
Washiriki wa mafunzo hayo kutoka Mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa wakifuatilia mafunzo hayo ya siku nane yanayoendela mjini Kigoma kupitia mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za umma (PS3) unaofadhiliwa na USAID.
3C
Sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo wakifurahia jambo wakati wa mafunzo hayo.
(Picha zote na Frank Mvungi-Maelezo Kigoma)
…………………………………………………………………
Na. Frank Mvungi-MAELEZO
Mara nyingi wananchi tumekuwa na Kasumba yakuona maboresho yanayofanywa na Serikali kwa Kushirikiana na wadau wa Maendeleo yanapaswa kuendelezwa na Kusimamiwa na Serikali peke yake ili hali sisi ndio wanufaika wa huduma hizo katika ngazi mbalimbali za kutolea huduma za jamii hasa katika sekta ya Afya na Elimu.
Nayasema haya kwa Kuzingatia kuwa sasa Serikali ya awamu ya Tano kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI na mradi wa Maboresho ya Mifumo ya Sekta za Umma wamekuja na mfumo mpya ulioboreshwa wa PlanRep utakaosaidia katika kupanga bajeti, mipango na kutoa ripoti ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kutumia Mfumo huu wa Kitaifa ambao ni wa Kisasa na umebuniwa na wataalamu wazalendo hapa nchini.
Katika kufanikisha azma ya mradi huu ulioshirikisha wadau mbalimbali wakiwemo Wizara ya Afya, TAMISEMI, Wizara ya Fedha na Mipango na wadau wengine, ni vyema tukatambua kuwa Mfumo huu unaweka msukumo katika kusimamia rasilimali zetu hasa fedha katika maeneo ya kutolea huduma kama Zahanati,Vituo vya Afya, Hosipitali na kwingineko.
Ili dhamira ya kujenga Tanzania mpya itimie kwa wakati kwa kuzingatia kuwa hicho ndicho kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Jemedari Rais Dkt. John Pombe Magufuli ni lazima kila Mtanzania atimize wajibu wake katika nafasi aliyokabidhiwa katika kuwahudumia wananchi.
Mfumo wa Kuandaa bajeti, mipango na kutoa ripoti ni wa Kielektroniki na umeboreshwa kwa kuunganisha sekta zote hali itakayoharakisha maendeleo ya wananchi na kuongeza uwazi na uwajibikaji katika hatua zote za kuwahudumia wananchi, Pia kuwezesha vipaumbele vya wananchi kuzingatiwa hali itakayopelekea wananchi wote kuwa na maisha bora.
Ni wakati sasa wananchi kutumia fursa ya kuanza kutumika kwa Mfumo huu mpya ifikapo 2018/2019  kuongeza kasi katika kufanya kazi na kutimiza wajibu ili mipango itakayopangwa itekelezwe kwa wakati badala ya kukaa na kulaumu Serikali,Kazi ndio msingi wa Maendeleo alisisitiza Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere  nyakati zote.
Kuboreshwa kwa Mifumo ni hatua kubwa iliyochukuliwa na Serikali na itasaidia kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo wananchi wanawajibika kushiriki kikamilifu katika hatua zote za utekelezaji wake.
Tumekuwa na mifumo mbalimbali ikiwemo ya kukusanya mapato,Kufanya malipo (EPIC) na ule wa kukusanya taarifa za sekta ya Afya na sasa PlanRep iliyoboreshwa itaunganisha mifumo yote na kufanya Taifa kuwa na Mfumo unaowezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kuwa wenye tija na unaoendana na thamani halisi ya fedha zilizotumika (value for money) kama inavyosisitiza Serikali ya Awamu ya Tano.
Wataalamu wetu katika maeneo ya kutolea huduma hamtakuwa na kisingizio tena pale mtakapotoa huduma duni kwani Serikali imeshaonyesha dhamira yake kuwa ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora hivyo msisitizo umewekwa katika kuangalia matokeo ya huduma zinazotolewa kwa wananchi na si vinginevyo.
Kuwepo kwa PlanRep iliyoboreshwa kunaiwezesha Serikali na wananchi kuja pamoja na kuweka vipaumbele vinavyoakisi azma yakufikia maendeleo ya kweli kwa kutumia rasilimali zilizopo hapa nchini,  Wataalam wetu wa ndani wamaeshiriki kikamilifu kujenga mfumo huu ulioboreshwa na unaowezesha Serikali kupeleka rasilimali moja kwa moja kwa wananchi ili kuchochea ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi wake.
Tutashuhudia muda mwingi ukitumika kuwahudumia wananchi katika maeneo yao na pia fedha zitakazookolewa zitatumika kufanya maboresho,awali tunatambua kuwa tulitumia fedha nyingi kuandaa bajeti na Mipango ambapo sasa mfumo huu wa kielektroniki utasaidia kwa kuwa maandalizi yote yatafanyika katika ngazi ya Kituo cha kutolea huduma,baadae kuwasilishwa kielektroniki katika Halmashuri ,Mkoa na Taifa kwa hatua Zaidi.
Mfumo wa PlanRep iliyoboreshwa umejengwa na wataalamu Wazalendo hivyo itakuwa rahisi katika kufanya maboresho pale itakapohitajika kwa kuzingatia mahitaji ya wakati husika katika Mikoa na Halmashauri zote nchini ambapo mradi wa maboresho ya Mifumo ya sekta za umma unatekelezwa, mradi unatekelezwa katika Mikoa 13, halmashauri 93 na utatumika kote nchini.

No comments