Header Ads

Responsive Ads Here

MPIRA WETU NA THAMANI YA USAJILI WA SIMBA SC


3
Na.Samuel Samuel
Dirisha la usajili kwa vilabu vya ligi kuu, ligi daraja la kwanza na la pili umefungwa rasmi tarehe 6 August 2017 kwa wachezaji wa ndani na kwa wachezaji wa nje dirisha linafungwa kesho tarehe 15 August 2017 saa sita kamili usiku.

Vilabu 62 kati ya 64 vimekamilisha usajili wake huku viwili vikishindwa kukamilisha usajili na kushushwa daraja . Vilabu hivyo ni Pepsi ya Arusha na Bulyanhulu ya Shinyanga vilivyokuwa ligi daraja la pili.
Msimu huu wa usajili 2017-18 klabu zikiingia upya kandarasi na wachezaji waliomaliza kandarasi zao, kusajili wapya , kuwatoa na kuwapokea kwa mkopo wengine ; ni gharama za kifedha ndio zilikuwa zikitumika ili kufanikisha zoezi hilo. Kila klabu imetumia kiwango cha fedha kulingana na uwezo wao, mahitaji ya aina ya wachezaji iwatakao na malengo mama katika ligi.
Katika matumizi hayo; klabu ya Simba SC mabingwa wa kombe la Azam Sports Federation Cup linalotoa mwakilishi wa Tanzania katika michuano ya kombe la Shirikisho Afrika ( CAF ) wameibuka vinara katika fungu walilolitumia kwa usajili. Simba imetumia bilioni 1.3 kwa mgawanyo ufuatao ;
USAJILI KWA WACHEZAJI WA NDANI
Simba SC imetumia kiasi cha milioni 360 za kitanzania kusajili wachezaji wa ndani katika kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya msimu mpya wa 2017-19. Fedha hizo zilitumika kuingia kandarasi mpya kwa wachezaji waliokuwa wamemaliza mikataba yao na kusainisha wachezaji huru wapya .
DAU LA UHAMISHO
Usajili uliohusisha uhamisho wa mchezaji kutoka klabu nyingine umetumia kiasi cha shilingi milioni 100 za kitanzania .
USAJILI WA WAGENI
Katika kusajili wachezaji wa kigeni kutoka nje , klabu hiyo ya pili kwa ukongwe nchini imetumia kiasi cha shilingi milioni 453! .
Katika dirisha dogo la usajili 2016-17 fedha ambayo inaingia kwenye bajeti hii , Simba walitumia milioni 346.
Kwa ujumla bajeti hiyo inawafanya Simba SC kutumia bilioni 1.259 za kitanzania ambazo zikiainishwa na kodi mbalimbali na matumizi mengine jumla kuu inakuja bilioni 1.3 na kuwafanya vinara wa matumizi ya fedha kwa msimu huu.
Simba SC kwa mujibu wa taarifa ya muhasibu mkuu wa klabu hiyo , makusanyo ya klabu hiyo kwa mwaka ni bilioni 1.6 kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato kama ifuatavyo hapa chini.
Haki za matangazo ya Runinga ( Azam media )
Katika udhamini huu wa Azam TV Simba SC wanakusanya kiasi cha shilingi milioni 184 kwa mwaka . Dau la kawaida la milioni 123 la udhamini kwa vilabu vyote na fedha za Simba TV.
Mdhamini mkuu wa ligi kuu ( Vodacom )
Kampuni ya Vodacom ambao ni wadhamini wakuu wa ligi kuu nchini, wanatoa kiasi cha milioni 108 kwa mwaka sawa na shilingi milioni 9 kwa mwezi .
Diamond Trust Bank wadhamini shirikishi wa ligi kuu nchini wanatoa kiasi cha shilingi milioni 10 kwa mwaka .
Mdhamini mkuu wa klabu ( Sportpesa )
Udhamini huu ni mpya kwa klabu ya Simba ambao umeingiwa mwezi juni mwaka huu na unaipatia klabu hiyo milioni 990 za kitanzania kwa mwaka . Ni kandarasi ya miaka mitano.
Jumla kuu katika mapato haya ni bilioni 1.607 kwa klabu ya Simba. Hili ndio kusanyo lao kuu kwa mwaka katika bajeti yao ya 1.3 bilioni ikiwa na maana kiasi kinachobaki ni milioni 270 mpaka 300 kama faida kwa klabu. Fedha ambayo ndio inaingia katika bajeti ya maendeleo ya klabu.
Kiuchumi bajeti kuu ya klabu ya Simba kwa ujumla wake kwa mwaka katika matumizi ya kawaida tu ya klabu ni 1.5 bilioni ukiondoa mipango ya kimaendeleo katika kuipa klabu hiyo nguvu za kiuchumi.
Tuanze kuitazama Simba SC katika hii mizani na aina ya soka tulilonalo.
Hatuwezi asilani kubeza matumizi ya klabu hiyo kulingana na mfumo wa soka ulivyo hivi sasa duniani. Soka linasimama katika muhimili wa uchumi wa dunia kwa maana ya pesa. Pasipo na pesa hakuna maendeleo ya soka bali penye pesa ndipo ua la pesa linachanua vyema.
Matumizi haya tunayaona makubwa yasiyo na tija kulingana na uwekezaji wetu mbovu katika soka katika nyanja zote ila katika ulimwengu wa soka bado ni matumizi madogo sana.
Kwanza kabisa vilabu vyetu ikiwemo Simba havina mifumo bora ya kiuchumi kutanua misuli yao kiuchumi . Endapo hili lingekuwa bora hii bajeti isingekuwa habari kuu mtaani kwa sasa . Klabu kama ingekuwa na soko zuri la bidhaa zake , miundo mbinu bora ya soka na mafanikio mazuri uwanjani kwa maana ya kushinda vikombe vikubwa barani Africa au kufika mbali katika hilo ambapo mamilioni ya dola hutolewa , watu wasingehoji kwanini Simba, Yanga au Azam wanatumia kiasi hicho cha fedha.
Simba wanaweza kujitetea wamewekeza kiasi hiki kikubwa cha fedha kwakuwa baada ya misimu minne sasa ndio wamepata fursa ya kuiwakilisha nchi kimataifa hivyo wanahitaji uwekezaji mzuri katika masuala ya kiufundi kwa maana ya kusajili wachezaji wazuri ( quality players ) ili wafike mbali kwenye kombe la Shirikisho na kujichotea mamilioni ya CAF pia kushinda vikombe vya ndani.
Wadhamini wa ligi kuu Vodacom ambao wanatoa milioni 108 kwa mwaka sawa na milioni 9 kwa mwezi hawa ndio wanaweza kukufanya ushituke na bajeti ya Simba SC ya bilioni 1.3. Ni lazima wadhamini waangalie matumizi ya vilabu hivi na angalau na wao udhamini wao uwe theluthi ya matumizi yao kwa mwaka ili kuvipa nguvu kifedha ili uwekezaji mwingine nje ya uwanjani ufanyike kwa maana ya miundo mbinu bora kisoka ; viwanja vikuu na vya mazoezi.
Bajeti hii hatuwezi kuihukumu hivi sasa bali mwisho wa msimu ndio tutaweza kuwanyooshea vidole Simba SC kwanini walitumia bilioni 1.3 pasipo kufikia malengo yao ? Bajeti hii ikiishiwa kuwapa kombe la ASFC lenye thamani ya milioni 50 ni hasara kuu pia likiishia kuwapa kombe la ligi kuu lenye thamani ya milioni 84 bado ni hasara. Kufika mbali katika michuano ya kombe la Shirikisho hususani kuvuka hatua ya makundi ndio faida pekee. Kwanza watapata zaidi ya milioni 400 za CAF pia kujitangaza kimataifa na huenda wakapata faida ya kuongeza wadhamini na kuuza wachezaji. Uimara wa klabu utaongeza ushawishi kwa mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo kuingia uwanjani na kuongeza mapato kwenye gate collection pia uuzwaji wa jezi zao endapo mfumo utawekwa vizuri.
Kama taifa kabla ya kuiponda bajeti ya Simba tuwaombe viongozi wapya wa TFF wawatazame wadhamini wakuu wa ligi kwa maana ya kuongeza fedha kwenye ligi ili kuipa thamani ligi yetu. Mathalani bingwa wa ligi kuu atoke na milioni 300! pia fedha ya udhamini iongezeke kutoka 108 milioni kwa mwaka mpaka milioni 200 kwa mwaka ili vilabu viweze kushiriki kikamilifu kutokana na msuli mzuri kiuchumi. Viongozi waangalie namna ya kuongeza wadhamini kwenye ligi ili kuwasaidia Vodacom, DTB na Azam .
Bado klabu zinapokea kiasi kidogo cha haki za matangazo kulinganisha na faida mdhamini anayopata kwa kurusha matangaz ya mpira ligi kuu. 123 milioni kwa mwaka bado ni ndogo sana . Angalau apande milioni 220 kwa msimu ili vilabu vivune jasho lao kwa haki.
Tukifanya hivyo na klabu hizi zikajijenga vyema kiuchumi , hatutashangaa tena bajeti 1.3 ya usajili kwa klabu inauoingiza 1.6 bilioni kwa mwaka. Vilabu vitakuwa na pato kubwa na matumizi madogo yenye tija . Pia timu zitakuwa imara kufika mbali katika michuano ya CAF na mwisho wa siku kuwa na timu bora za taifa kwa ngazi zote.

No comments