Header Ads

Responsive Ads Here

MATIC ANAPOTUKUMBUSHA YA MOURINHO KWA JUAN MATA

 

20842267_1398541580252719_5369876815506404144_n
ABDUL DUNIA
“SIJUI nimekuja kutoka wapi, mara ya mwisho nilipozungumza na Mourinho aliniambia kuwa nina umuhimu ndani ya klabu hii. Huwezi kumlazimisha mtu kuamua atakalo.
“Nina uhakika kuwa ameamua kile alichohitaji kukiamua, kila mtu anahitaji kuniona katika chaguo la kwanza, lakini haiwezekani. Ameamua kile alichotaka.

“Lazima uwajue watu kabla ya kuwatafsiri, nimemuelewa Mourinho, nimechagua uamuzi uliokuwa sahihi, acha nikapambane kwengine ambapo naweza kupata heshima ninayostahili,” alisema Juan Mata wakati akijiandaa kwenda Manchester United miaka minne iliyopita.
Kilichotoka ndani ya kinywa cha Mata kila mtu alikielewa. Hakuna asiyemuelewa Mata kwa kile alichokizungumza.
Ni wachezaji wachache kama Mata duniani wanaoweza kutoa la moyoni kwa timu yake ya zamani wakati akijiandaa kwenda katika timu nyingine. Wengi huficha ukweli na kujifanya hawajatendewa mabaya na makocha wao.
Huondoka wakiwa na tabasamu wakionyesha kuwapenda na kuwatukuza makocha na wamiliki wa klabu zao za zamani kana kwamba walilelewa katika maisha bora na heshima ya hali ya juu. Kumbe huondoka kama watumwa ingawa walicheza kwa hali na mali katika timu zao.
Wapo ambao huondoka katika ukimya na mara nyingine kushindwa kutoa kauli ya kijasiri kama aliyoitoa Mata. Mara nyingine hushindwa hata kupambania heshima yao kwa kukataa kusema ukweli katika vyombo vya habari kwa kuwaogopa wamiliki na makocha wao. Hawa huitwa waoga. Tuachane na hilo.
Wiki mbili zilizopita klabu ya Manchester United ilimsajili kiungo mkabaji wa Chelsea, Nemanja Matic kwa ada ya pauni milioni 40. Usajili wa Matic ni sawa na ule wa Mata alivyotoka Chelsea kwenda United kwa ada ya pauni milioni 37.
Mata katika ubora wake hakuthaminika katika kikosi cha Jose Mourinho licha ya kuisaidia Chelsea kutwaa taji la ligi ya mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich anakosaje heshima katika kikosi hicho.
Mata hatomsahau Roberto Di Mateo wakati akimtumikia Chelsea, alipata kila kitu katika kikosi hicho.
Mourinho aliuponda moyo wa Mata kama Matic alivyopondwa na Conte. Matic aliyeisaidia Chelsea katika michezo muhimu ikiwemo ule wa ligi kuu England dhidi ya Tottenham Hortspur unamuachaje kirahisi hivyo.
Paundi milioni 40 si kitu kwa Chelsea. Si kitu kwa Matic na bilionea Roman Abramovic. Uwezo wa Matic ni zaidi ya fedha hizo. Tusijihadae na Bakayoko kwa kumuacha Matic aende zake.
Nalikumbuka bao lake la mita 35 kutoka katika lango la Chelsea kwenda kwa Spurs. Shuti kali alilopiga wala halikutarajiwa. Matic ana ubora wa hali ya juu katika soka.
Ile mechi iliisha kwa matokeo ya 4-2. Matic bado alikuwa ni muhimu katika kikosi cha Chelsea. Hakuna anayekataa hilo. Ubora wake wa kukaba na kushambulia ndio uliomvutia Mourinho kumnunua kwa mara ya pili akitokea Benfica ya Ureno. Huyu ndio Nemanja Matic, mwanaume aliyetimia katika dimba la kati.
Matic ni mwanaume tena haswa, ambaye akiwa dimbani hapendi masihara. Aina yake ya upole na kupooza mipira imekuwa ikimfanya Conte kukasirika lakini nina uhakika mkubwa kuwa Conte naye anajisuta kwa kumuacha Matic.
Uzembe alioufanya Conte kwa Matic ni sawa na ule alioufanya kwa Diego Costa na kumuamini zaidi Alvaro Morata kuwa ndio Didier Drogba mpya wa Stamford Bridge. Uzembe alioufanya Conte kwa Matic hautofautiani na ule wa Mourinho kwa Mata vwakati ule yupo Chelsea.
Matic ni muhimu katikati. Hakika atawasaidia sana Manchester United. Uwepo wa Paul Pogba, Ander Herera na Nemanja Matic kati utamfanya Romelu Lukaku kutawala orodha ya wafungaji katika ligi kuu ya England labda atake mwenyewe kutowaongoza.
Matic ni sawa na mwiba. Kwa hakika Matic ana uwezo wa kumsaidia Lukaku. Anaweza kuisaidia Manchester United. Ana uwezo wa kumfanya Mourinho kuwa ‘Special One’ kama alivyokuwa akiwa na FC Porto, Inter Milan, Chelsea na Real Madrid. Conte hakika atajuta kumuacha Matic. Asijidanganye na Bakayoko mmoja ambaye bado ‘wakuja’ ndani ya Chelsea.

No comments