Header Ads

Responsive Ads Here

KESI 24 ZA MAUAJI KUSIKILIZWA KATIKA KIKAO MAALUM CHA MAHAKAMA KUU-KANDA YA DODOMA


chaba
Na Mary Gwera
JUMLA ya Kesi za Mauaji 24 zimepangwa kwa ajili ya kusikilizwa kuanzia Agosti 14 hadi Agosti 25 Mwaka huu katika Kikao maalum cha kusikiliza mashauri ‘Court session’ kitakachofanyika  Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hii, Naibu Msajili Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, Mhe. Messeka John Chaba alisema kuwa mashauri manne (4) kati ya mashauri hayo 24 yamepangwa kusikilizwa ‘hearing’ huku mashauri 20 yakiwa yamepangwa kwa ajili ya usikilizwaji wa awali ‘Plea taking.’
Kufuatia maandalizi ya kikao hiki maalum Mhe. Chaba ametoa wito kwa mashahidi  muhimu ambao wametumiwa wito wa kuitwa shaurini ‘summons’ kufika Mahakamani na kutoa ushahidi wao ili haki iweze kutendeka.
Kwa upande wa Waendesha Mashtaka – Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jeshi la Polisi Mkoani Dodoma, Mhe. Chaba amewasihi kuhakikisha wanatimiza wajibu wao ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Mashahidi wote wanapatikana na kufika Mahakamani ili kuiwezesha Mahakama kusikiliza mashauri hayo na kuyatolea uamuzi kwa mujibu wa sheria.
“Miongoni mwa mashauri hayo 4 yatakayosikilizwa, mashauri 2 yalisikilizwa na Mahakama ya Rufani Tanzania na kuamuliwa yaanze upya,” alifafanua Mhe. Chaba. Aliyataja mashauri hayo kuwa ni “Crim. Sess. Case No. 52/2014 Mshtakiwa – Adrian Francis na Crim. Sess. Case No.39/2012 Mshtakiwa – Wylife Salumu@Nyendo & 2 Others.
Kikao hicho kitaendeshwa na Majaji watatu (3) wa Mahakama Kuu Dodoma, ambao ni;  Mhe Jaji M.A. Kwariko, Jaji Mfawidhi, Mhe Jaji H.H. Kalombola, na Mhe Jaji L. Mansoor.
“Matarajio yetu ni kwamba kikao hiki kitasaidia kumaliza/kuondoa mashauri ya jinai ambayo ni mlundikano.  Aidha, kikao hiki kitatoa fursa kwa washtakiwa 20 kufika Mahakamani kwa ajili ya usikilizwaji wa awali/uchukuaji wa kiri (plea taking) na huenda baadhi yao wakakiri makosa yao na kupunguza ama kuongeza idadi ya mashauri ambayo yatakuwa yameamuliwa na Mahakama Kuu kwa mwaka huu 2017,” alibainisha Mhe. Chaba.
Mahakama ya Tanzania imedhamiria kusikiliza na kutoa uamuzi kwa wakati kwa mashauri yote ya muda mrefu na yanayoendelea kufunguliwa Mahakamani ili haki ipatikane kwa wakati  na pia kurejesha imani ya jamii.

No comments