Header Ads

Responsive Ads Here

KATIBU MKUU S.NKINGA: WANACHI WA IRINGA VINARA WA MIRADI YA MAENDELEO

Na Erasto Ching’oro – WAMJJW
Mapema wiki hii, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii) Bibi Sihaba Nkinga amepongeza ari ya wananchi wa mkoa wa Iringa katika utayari wao wa kushiriki kazi za kujitolea ili kuchangia maendeleo yao na Taifa.

Bibi Nkinga alibainisha kuwa kushamiri kwa miradi ya maendeleo katika vijiji mbalimbali mkoani Iringa ni matokeo ya weledi wa wataalam wa Maendeleo ya Jamii kuweza kutumia mbinu shirikishi katika kuibua, kupanga na kutekeleza miradi hiyo kwa kushirikisha jamii ili kuwa na miradi endelevu inayomilikiwa na jamii na kusimamiwa na wataalam wa maendeleo ya jamii.
Tafiti zinaeleza kuwa asilimia 71 ya watanzania wanapenda kukaa vijiweni, hawapendi kazi. Taarifa kama hii, inapotolewa kwa kiasi kikubwa inamhusu mtaalam wa maendeleo ya jamii kutambua changamoto hii na kuwajibika kuibadilisha kuwa fursa. “Mhe. Rais wa Jamhuri ya Tanzania Mhe. Dkt. John P. Magufuli anaposema  vijana wanapenda kucheza ‘pool’ bila kufanya kazi mtaalam wa maendeleo ya jamii ujue unawajibu wa kutekeleza”, amesema Katibu Mkuu Nkunga.
Itakumbukwa kuwa kipindi cha miaka ya 1970,  mchango wa wananchi katika kazi za kujitolea ulikuwa mkubwa takribani asilimia 66 ikilinganishwa na asilimia 14 ya hivi sasa.  Hii inamaana kuwa jamii imeegemea zaidi katika kuwezeshwa na Serikali na wafadhili ilihali wananchi wakitoa mchango mdogo katika maendeleo yao.
Kwa wakati huo, mafanikio yalipatikana kutokana na ukweli kuwa maafisa maendeleo ya jamii walitumia weledi kuwahamasisha wanachi kushiriki kazi za maendeleo. Hatua hii ilichochea ushiriki wa wananachi kutumia rasilimali na nguvu zao kujiletea maendeleo yao. Katibu Mkuu Nkinga alisisitiza kurejesha ari ya kufanyakazi ili kutekeleza kikamilifu majukumu ya idara ya maendeleo ya jamii. Ikumbukwe kuwa ni Wizara inahimiza kuwafuata watu walipo na kuwashirikisha katika kujadili mahitaji, mipango yao ili kumiliki miradi hiyo kwa manufaa yao wenyewe.
Bibi Nkinga amewapongeza watendaji wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa mkoa wa Iringa, kwamba wameonesha njia na kuwataka waongeze juhudi. Aidha, amewataka wataalam wa maendeleo ya jamii katika maeneo mbalimbali kujifunza mifano bora iliyoko mkoa wa Iringa ili kurejesha ari na hamasa ya kushiriki kazi za maendeleo, msukumo ukiwa jamii kufanyakazi kwa bidii katika kujiletea maendeleo yao.
Mradi wa ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Ufyambe, kata ya Waswa, wilaya ya Iringa mkoani Iringa, ni mfano bora wa urejeshaji ari ya kazi kwa manufaa ya kijiji na Taifa. Katika utekelezaji wa mradi huu, mradi unasimamiwa na Afisa Maendeleo ya Jamii wa kata ya Wasa iliyoko wilaya ya Iringa vijijini Bw. Saidi Omari kwa kushirikiana na viongozi wa kijiji hicho. Kazi zote za utekelezaji wa mradi zinafanywa na wananchi, jambo ambalo lilimwinua Katibu mkuu Sihaba Nkinga kwenda kushirikiana nao kufanya kazi ya mikono kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo.
Zahanati ya ufyambe itakapokamilika itakuwa imegharimu shilingi milioni 60  na hadi sasa imegharimu kiasi cha shilingi 17,470,000/- ikiwa ni fedha ya wananchi na wahisani wa ndani na nje ya kijiji hicho. Zahanati hiyo itasaidia kuondoa tatizo la kutembea umbali wa kilometa zaidi ya kumi kutafuta huduma za kiafya jambo ambalo limekuwa likisababisha vifo kwa watoto na akinamama wajawazito kutokana na kutembea umbali mrefu kutafuta matibabu. 
Diwani wa Kata ya Wasa alipongeza Katibu mkuu Bibi Nkinga kwa kuonbesha utumishi uliotrukuka kwa kuwatembelea wananchi wa Ufyambe na kushirikikiana nao kufanya kazi za ujenzi ili kuokoa maisha ya wanawake na watoto. Mwenyekiti wa Ufyambe alieleza kuwa kijiji hakijawahi kutembelewa na kiongozi wa ngazi yake, hivyo Katibu Mkuu Nkinga ameandaika historia siyo tu kwa kufika hapo kijijini bali kuweza kushiriki kazi ya kuchanganya saruji, kubeba matofali, na mchango wake wa  ujenzi vimeonesha mfano katika utumishi wa jamii.  
Akiwa kijijini Afyambe, Katibu Mkuu S. Nkinga aliongozana na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii Bw. Patrick Golwike na Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa Bibi Wamoja Ayubu na Mkurugenzi wa wilaya ya Iringa Bw. Robert Masunya na maafisa wengine.

No comments