Header Ads

Responsive Ads Here

HBUB YALAANI OFISI ZA WANASHERIA KULIPULIWA KWA BOMUTume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inapenda kutoa tamko la kulaani kitendo cha kupigwa bomu ofisi za wanasheria wa IMMMA zilizoko barabara ya Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam, kilichotokea usiku wa kuamkia Jumamosi tarehe 26 Agosti, 2017.


Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imesikitishwa na kitendo hicho ambacho kinaashiria uhalifu wenye nia ya kutisha wanasheria wasitekeleze majukumu yao ya kisheria ya kutetea wateja wao.

Tume inasisitiza kuwa dhana ya utawala bora inategemea utawala wa sheria, ambao utaathirika iwapo wanasheria watatishwa na matukio kama ya kupigwa mabomu au vitendo vinginevyo vitakavyowanyima uhuru wa kufanya kazi zao.

Tume inalitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha linakamilisha upelelezi wa tukio hilo na kuwapeleka wahusika katika vyombo vya sheria.

Aidha, Tume inautaka uongozi wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) kusitisha tangazo lao la kuwataka Mawakili kususia vikao vya Mahakama na Mabaraza kwa siku mbili kwani mgomo huo hautakuwa na maana kwa vile vyombo vya usalama vimeishaanza kufanya uchunguzi. Pia ni vyema TLS ikasitisha mgomo huo kwani utawaathiri zaidi wateja wao ambao hawahusiki na tukio la kupiga bomu.

Imetolewa na:
(SIGNED)

Bahame Tom Nyanduga
Mwenyekiti

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Agosti 28, 2017


No comments