Header Ads

Responsive Ads Here

FAMILIA YAGOMA KUMZIKA ANAYEDAIWA KUUAWA MGODINI GGM


Maeneo ya mgodi wa dhahabu wa Geita (GGM)Shughuli zikiendelea za uchimbaji madini ya dhahabu.
 Shimo ambalo limekwisha kuchimbwa
Familia ya
kijana Shija Charles mwenye umri wa miaka 25 imegoma kumzika ndugu yao
huyo  wanayedai kuwa amefariki baada ya
kupigwa na walinzi wa mgodi wa dhahabu wa GGM na kutaka uchunguzi wa kina
ufanyike.
Tukio la
kuuawa kwa kijana huyo limetokea juzi Majira ya saa moja usiku wakati akiwa na
wenzake wawili walipoingia kwenye mgodi huo kwa madai ya kwenda kuchukua Mawe
ambayo yanajulikana kwa jina la Magwangala.
Vijana
walionusurika kwenye tukio hilo Filipo Enock na Shija Mashemba wamesema
waliingia kwenye eneo la mgodi kwenye eneo la Piti na wakati wanateremka kwenye
maeneo ya barabara ya mgodi walikutana na walinzi  na kwamba mwenzao alikamatwa wakati
wakikimbia .
Mwenyekiti
wa Mtaa wa Elimu kata ya Nyankumbu alikokuwa akiishi kijana aliyeuawa Bw Hassan
Mshora Malima amesema baada ya kupata taarifa za kifo hicho walifika kwenye
chumba cha kuhifadhia maiti kwenye Hospitali ya Mkoa wa Geita na kukuta mwili
wa marehemu ukiwa na majeraha ya kupigwa.
Msemaji wa
Familia ya kijana huyo Bw Kazimili Malole amesema hawako tayari kuchukua mwili
huo kwa ajili ya maziko hadi watakapopata ukweli wa kifo chake.
“Sisi  kama familia hatupo tayari kuchukua mwili wa
marehemu hadi pale uchunguzi utakapo fanyika kujua ndugu yetu ni kipi ambacho
kimepelekea kuondoa uhai wake na tunaomba serikali itusaidie kwa swala hili
tupate haki zetu za msingi”Alisema Kazimilia.
Meneja
mahusiano ya jamii wa Mgodi huo Bw Manase Ndoroma amekanusha taarifa za kupigwa
kwa kijana huyo hadi kufariki na kwamba alianguka kwenye shimo mgodini na
kwamba viongozi wa jadi waliitwa kushuhudia tukio hilo.
“Mgodini
ndani kuna mashimo ambayo huwa tunachimba na kuyaacha wazi watu wamekuwa
wakiingia kinyemela kwenye maeneo hayo ambayo ni hatarishi kwa maisha yao na
mwisho wa siku wengi huanguka na kupoteza maisha kutokana na maeneo hayo kuwa
na mwamba mkali,na sisi tumekwisha kusema kama kuna mwananchi anahitaji kuja
mgodini kwa ajili ya kuona shughuli za uchimbaji  ni vyema wakafuata utaratibu kuliko kuingia
kinyemela kwani kuna maeneo ambayo ni hatarishi”Alisema Manase.
Hata hivyo
Kamanda wa Polisi mkoani Geita  Mponjoli
Mwabulambo  alipotafutwa kwa njia ya simu
amesema hayupo ofisini kwa muda huo na yupo kwenye oparesheni na anatarajia
kufika jioni ofisini kwake.
IMEANDALIWA NA MADUKA ONLINE

No comments