Header Ads

Responsive Ads Here

Coastal Union haina kinyongo na Njombe Mji


imagesZipo taarifa zinazosambaa kuhusiana na uongozi wa klabu ya Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’ kudaiwa kuwazuia wachezaji wake watatu kushiriki Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara baada ya kufuzu majaribio katika Klabu ya Njombe Mji kutoka mkoani Njombe.
Wachezaji hao ambao ni Behewa Sembwana, Hatibu J. Hatibu na Mustafa Said, wapo katika sintofahamu kutokana na kukosa barua za kuwaruhusu kuondoka Coastal Union baada ya viongozi wa Njombe Mji kushindwa kujitokeza kwa ajili ya mazungumzo ya kuvunja mkataba.
Hata hivyo, kati ya wachezaji watatu wawili walikua na mkataba na Coastal Union ambao ni Behewa Sembwana na Hatibu J. Hatibu ambapo mkataba wao ulitakiwa kuisha Agosti 4, 2017 lakini Njombe Mji waliwasajili Julai 4, 2017 bila kufanya mazungumzo yoyote, na hata mwenyekiti wa Coastal Union, Bwana Steven Mnguto kuwandikia barua viongozi wa Njombe Mji wafuate taratibu hakuna kiongozi aliyejitokeza kufanya hivyo.
Aidha, kuhusu mchezaji Mustafa Said, Coastal Union inakiri haina mkataba naye lakini kwa kuwa aliletwa na mtu (jina linahifadhiwa) ambaye alitaka alelewe na klabu kupata uzoefu, amewaeleza viongozi wa Coastal Union kutomwachia hadi viongozi wa Njombe Mji watakapofanya mazungumzo naye. Hivyo, sisi tunasubiri ruhusa kutoka kwake.
Kwa mujibu wa viongozi wa Coastal Union, masharti ya kuvunja mkataba waliyopewa viongozi wa Njombe Mji ni kulipa gharama walizoelezwa ambazo hata hivyo hawajatimiza.
Coastal Union ni klabu iliyoasisiwa siku nyingi na kuna vipaji vingi vilipita katika klabu hii, hivyo haiwezi kwa namna yoyote ile kutaka kumkosesha mchezaji kufanikiwa katika safari yake kisoka.
Msisitizo tunaoutoa ambao tunaamini klabu yoyote inayojitambua ingefanya kama tunavyofanya, tunaomba klabu za soka kufuata utaratibu wa kuomba barua za wachezaji ili vijana wetu washiriki Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara ambayo ni ndoto ya wachezaji wengi nchini.

No comments