Header Ads

Responsive Ads Here

CHAKUA Yaja na Mikakati Mipya ya Kusaidia Abiria


PIC 1
Mratibu na Mtendaji Mkuu wa Chama cha Kutetea Abiria (CHAKUA) Bw. Monday Likwepa akielezea changamoto zinazowakabili abiria mbele ya Waandishi wa Habari (hawapo pichani), katikati ni Mwenyejkiti wa Chama hicho Bw. Hassan Mchanjama, kulia ni Mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki na Katibu wa Marine Bw. Wilson Sylvester Damo.

PIC 2
Mwenyekiti wa Chama cha Kutetea Abiria (CHAKUA) Bw. Hassan Mchanjama akitoa ufafanuzi juu ya ukataji tiketi kwa njia ya kieletroniki kwa wasafiri alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani), wa kwanza kutoka Kushoto ni Afisa Miradi Taifa wa Chama hicho Bw. Elias Kalinga, katikati ni Mratibu Mtendaji Mkuu wa Chama hicho Bw. Monday Likwepa
……………………
Na, Neema Mathias & Thobias Robert -MAELEZO
Chama cha Kutetea Abiria (CHAKUA), kimeanzisha mikakati mbalimbali itakayotumika kukabiliana na changamoto zinazowakumba wasafiri wa majini na nchi kavu  hapa nchini.
 Hayo yamesemwa Leo Jijini Dar es Salaam na Mratibu Mtendaji wa CHAKUA Bw. Monday Likwepa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu changamoto zinazowakabili abiria na namna ya kuzikabili,  ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kila abiria anapata haki yake hasa pale anapopata tatizo akiwa safarini kwa kutumia chombo cha moto au anapokuwa akitembea kwa miguu.
 Likwepa alisema kuwa changamoto hizo ni pamoja na abira kulanguliwa wanapokata tiketi kwaajili ya safari, kuibiwa fedha, kupoteza mizigo, kulala mahali pasipostahili, kukosa huduma za matibabu na fidia wanapopata ajali pamoja na njaa ya kutwa nzima kwa kukosa huduma ya chakula na vinywaji ndani ya vyombo husika vya usafiri. 
“kutokana na changamoto hizo CHAKUA tumekuja na mikakati ya kuhakikisha kuwa abiria anayepata ajali na kusababisha ulemavu wa kudumu au kupoteza maisha anapata haki na fidia stahiki, kusimamia kesi zote mahakamani pamoja na kuelimisha abiria kujua haki na wajibu wa msafiri na msafirishaji mjini na vijijini kwani abiria wengi wameonekana kutokuwa na elimu ya kutosha jambo ambalo linapelekea kukosa haki zao za msingi,” alifafanua Likwepa.
Licha ya CHAKUA kuonyesha jitihada mbalimbali za kumtetea abiria, wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la ukosefu wa rasilimali fedha kwani kwa muda mrefu wamekuwa wakitumia fedha zao binafsi kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili abiria jambo ambalo limekuwa likiwaelemea kwani changamoto za abiria huongezeka siku hadi siku.
“Kwa mujibu wa katiba ya CHAKUA vyanzo vya mapato yake ni ada za wanachama, wadau, na wahisani. Michango hii imekua haitoshelezi kutekeleza majukumu  yao ya kila siku, hivyo ili kutekeleza majukumu yake kikamilifu CHAKUA inamwomba kila Mwanachama alipe ada zake na kila abiria anaposafiri atalazimika kulipa sh 200 ili kukiwezesha chama hicho kutekeleza majukumu yake ipasavyo,”alieleza Likwepa.
Likwepa alifafanua kuwa kupitia kupitia sh 200 ambayo itakua inalipwa na wasafiri wa mabasi na treni za mikoani itawawezesha kujenga ofisi zao katika vituo vyote vya usafiri nchini, halikadhalika fedha hizo zitatumika kuwasaidia wasafiri pale wanapopata matatizo mbalimbali, mkakati huu utaanza rasmi pale mamlaka zinazohusika na usafiri zitakaporidhia.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CHAKUA Bw. Hassan Mchanjama ameitaka Serikali  kuwalazimisha wenye mabasi ya abiria kutumia mfumo wa kielektroniki katika ukataji wa tiketi kwa wasafiri  ili kudhibiti tatizo la ukwepaji kodi ambao umekua ukifanywa na baadhi ya wamiliki wa mabasi kupitia Chama cha Wamiliki wa Mabasi (TABOA).
“TABOA wamekuwa wakipinga mfumo wa ukataji tiketi kwa njia ya kielektroniki ili kuendelea kuwalangua abiria na kukwepa kutoa mapato sahihi kwa serikali,” alieleza Mchanjama na kusisitiza,   “serikali haina budi kukifuta chama hicho kwani wengi wanaounda kikundi hicho sio wamiliki wa mabasi badala yake TABOA wameweka madalali ambao ndio wanaohudhuria vikao vya serikali.”
Aidha Mchanjama ameiomba serikali iwachunguze TABOA kwani wamekua wakitumia vyombo vya habari kupotosha na kwenda hadi kwa viongozi wa Serikali Dodoma ili kuchelewesha zoezi la abiria kukatiwa tiketi kwa mfumo wa kielektoniki, hivyo serikali haina budi kukifuta chama hicho kwani wanaongoza kwa propaganda, hujuma, fitina hata kudiriki kutoa rushwa ili kuchelewesha kuanzishwa kwa mfumo huo.
 CHAKUA kilianzishwa kwa malengo ya kutoa huduma mbalimbali kwa wasafiri wanaopata adha katika safari zao na kimesajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya usafiri wa nchi kavu na majini, Chama hiki kipo chini ya SUMATRA kwa ushirikiano mkubwa wa Jeshi la Polisi na taasisi nyingine za kiserikali na kijamii.

No comments