Header Ads

Responsive Ads Here

TCU Yajizatiti Kuimarisha Ubora Wa Elimu Vyuo Vikuu.


Na. Thobias Robert – MAELEZO
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) itaendelea kusimamia kwa umakini ubora wa elimu vyuo vikuu ili kuzalisha wasomi wenye tija kwa Taifa na kuongeza ufanisi, ubunifu, maadili pamoja na utendaji kazi uliotukuka kwa vijana wanaohitimu elimu ya vyuo vikuu nchini.

Hayo yamesema leo na Afisa Habari Mwandamizi wa TCU Edward Mkaku wakati wa mahojiano na mwandishi wa habari hii katika maonesho ya vyuo vikuu yanayoendelea katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini, Dar es Salaam.
“Kwa sasa TCU tunaratibu udahili ambao unafanywa na vyuo vikuu vyenyewe, wakishamaliza kudahili majina yataletwa kwetu, na sisi tutapitia majina yote ili kuyahakiki kama yana vigezo vyote vya kujiunga na chuo husika. Tutashirikiana na Baraza la Mitihani na tukigundua kuna mtu amechomekewa kujiunga na chuo akiwa hana vigezo tutamuondoa,” amefafanua Mkaku.
Amesema kuwa tume hiyo itatembelea vyuo vyote nchini ili kufanya ukaguzi wa jina kwa jina kwa ajili ya kujiridhisha, na kama ikitokea hakuna kasoro yoyote basi mwanafunzi ataendelea na masomo.
Mkaku aliongeza kuwa, ingawa zoezi la udahili limerudishwa vyuoni lakini bado TCU ina mamlaka ya kusimamia ubora, mwenendo, mitaala pamoja na kozi zinazotolewa vyuoni ili kukuza na kuendeleza elimu bora kwa ajili ya kuinua Taifa hasa wakati huu ambapo Taifa linaelekea katika mapinduzi ya uchumi wa viwanda.
Aidha amewataka wahitimu wawe makini katika kuzisoma kozi na kuchagua ili kusiwepo na mkanganyiko na malalamiko yanayotokana na kukosea kuchagua au kupangiwa kozi ambayo mhitimu hakuomba.
Hapo nyuma zoezi la udahili wa vyuo vikuu lilikuwa likifanywa na TCU, lakini kutokana na kuwepo kwa malalamiko mengi ya wanafunzi ya kupangiwa vyuo au kozi ambazo hawakuzichagua ama kuzipenda, mapema mwaka huu Rais Dkt. John Pombe Magufuli alisitisha zoezi la udahili  kupitia TCU na kuagiza udahili kufanyika moja kwa moja vyuoni kuanzia mwaka wa masomo wa 2017/18.

No comments