Header Ads

Responsive Ads Here

TANZANIA SIYO LANGO LA KUPITISHIA DAWA ZA KULEVYA-MAJALIWA


PMO_6460
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akivuka lango kuu linalotenganisha Malawi na Tanzania katika mpaka wa nchi mbili hizi eneo la Kasumulu wilayani Kyela Julai 29, 2017.  Kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla.

PMO_6474
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa kwenye eneo la mpaka wa  Tanzania na Malawi  katika eneo la Kasumulu wilayani Kyela Julai 29, 2017. Kushoto ni Naibu Spika, Dkt Tulia Ackson Mwansasu  na kulia kwa Waziri Mkuu ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla.
PMO_6497
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wananchi wa kata ya  Njisi wilayani Kyela wakati alipowasili kwenye uwanja wa michezo kuhutubia mkutano wa hadhara Julai 29, 2017.
PMO_6508
Waziri Mkuu, kasim Majaliwa akihutuia mkutano wa hadhara kwenye  uwanja wa kata ya  Njisi katiak eneo la   Kasumulu lililopo kwenye mpaka wa Tanzania na Malawi ktika wilaya ya Kyela Julai 29, 2017.
………………………………….
*Aagiza kuimarishwa kwa ukaguzi wa watu, magari na mizigo mipakani
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania siyo lango la kupitishia dawa za kulevya kwenda nchi za nje hivyo ameagiza ulinzi uimarishwe katika mipaka yote.
Amesema kunatabia ya baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu kutumia Tanzania kama njia ya kupitisha dawa za kulevya kwa ajili ya kupeleka nchi za  Afrika ya Kusini, Malawi na Zambia.
Alitoa kauli hiyo jana jioni (Jumamosi, Julai 29, 2017) alipozungumza na watumishi wa kituo cha forodha cha Kasumulu kilicho katika mpaka wa Tanzania na Malawi wilayani Kyela.
Waziri Mkuu alisema ili kuhakikisha jambo hilo linadhibitiwa ni vema ukaguzi wa watu wanaopita kwenye maeneo hayo pamoja na mizigo ukaimarishwa.
“Endeleeni kufanya upekuzi wa kina wa magari, watu na mizigo yote yote katika mipaka yetu. Tanzania siyo lango la kupitishia dawa za kulevya na Serikali haitakubaliana na jambo hilo.”
Pia aliwataka viongozi hao kuhakikisha biashara zote za magendo zinazifanyika mipakani, zikiwemo za kubadilisha fedha zinadhibitiwa kwa kuwa zinaikosesha Serikali mapato.
Alisema ni vema yakawepo maduka ya kubadilishia fedha katika maeneo hayo ili kudhibiti biashara hiyo ambayo kwa sasa inafanywa kimagendo huku Serikali ikikosa kodi.
“Biashara za magendo zidhibitiwe katika maeneo haya na yaanzishwe maduka ya kubadilishia fedha ili biashara hiyo ifanyike kihalali. Pia imarisheni vyanzo vya mapato.”
Pia Waziri Mkuu aliwataka Maofisa wa Uhamiaji katika mikoa hiyo ya mipakani kuhakikisha wanadhibiti uingiaji holela wa raia wa kigeni kwa lengo la kuimarisha ulinzi nchini.
Waziri Mkuu alisema katika baadhi ya maeneo kwa sasa zimeanza kuonekana silaha ambazo hapo awali hazikuwepo na ndizo zinazosadikiwa kutumika katika matukio ya kihalifu.
Awali, Bw. Taniel Magwaza ambaye ni Afisa Mfawidhi wa Uhamiaji alisema watahakikisha wanafanya kazi kwa weledi katika kupambana na biashara za magendo kwenye mpaka huo.
Alisema mbali na kupambana na biashara za magendo pia watadhibiti uingiaji wa wahamiaji haramu kwa kushirikiana na watumishi idara zote waliopo katika mpaka huo wa Kasumulu.
Bw. Magwaza alisema katika doria zilizofanywa mwaka 2016/2017 jumla ya wahamiaji haramu 87 walikamatwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Alisema wahamiaji hao walitokea nchi za Malawi (30), Ethiopia (47), Burundi (6) Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) (4), ambapo baadhi walirudishwa makwao na wengine walifungwa katika Gereza la mkoa wa Mbeya.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JULAI 30, 2017

No comments