Header Ads

Responsive Ads Here

TAARIFA KUTOKA JESHI LA POLISI MKOANI MBEYA


TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA KWA VYOMBO VYA HABARI “PRESS RELEASE” TAREHE 28.07.2017.


Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu.
Mafanikio yaliyopatikana kutokana na misako/doria ni kama ifuatavyo:-
KUKAMATWA KWA WAHAMIAJI HARAMU RAIA WA ETHIOPIA.

Mnamo tarehe 27.07.2017 majira ya saa 16:30 jioni, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya likiwa katika msako/doria huko katika Kijiji na Kata ya Lupa, Tarafa ya Kipembawe, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya lilifanikiwa kuwakamata watu wawili raia wa Ethiopia wakiwa wameingia nchini bila kibali.
Wahamiaji hao haramu walifahamika kwa majina ya 1. TATIOS TOQKSO [30] na 2. MITEKU ESUMO [20]. Wahamiaji hao walikamatwa wakiwa wanasafirishwa kwenye Gari yenye namba za usajili T. 810 AQY aina ya Scania Basi lililokuwa likitokea Tabora kuelekea Mbeya ambalo lilikuwa likiendeshwa na dereva aitwaye ABDUL SUDENI [43] Mburush na Kondakta aitwaye IBRAHIM BAKARI [28] wote wakazi wa Tabora.
Watuhumiwa wote wahamiaji haramu wawili raia wa Ethiopia na wasafirishaji wawili kwa pamoja wanashikiliwa na Polisi. Upelelezi unaendelea
KUKAMATWA KWA WAHAMIAJI HARAMU RAIA WA ETHIOPIA.

Mnamo tarehe 28.07.2017 majira ya saa 03:30 usiku wa kuamkia leo, Jeshi la Polisi likiwa katika Msako/Doria huko Check-Point Igawa iliyopo Tarafa ya Rujewa, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya, lilifanikiwa kuwakamata Waethiopia watano (5) kwa kosa la kuingia nchini bila kibali.
Wahamiaji hao haramu ni walitambulika kwa majina ya 1. BIRAMU DEISSE [25] 2. TAPAGI JOBORO [23] 3. BIRHUN ASHOZU [35] 4. TILANU MIFKUUN [23] na 5. ZARYUN JILIMWA [32] wote raia wa Ethiopia.
Wahamiaji hao haramu walikuwa wanasafirishwa kwa miguu na Mtanzania ambaye alifahamika kwa jina la RASHID NDIDI [20] Mkazi wa Dodoma ambaye ndiye alikuwa mwenyeji wao na walikuwa wakisafiri porini. Upelelezi unaendelea.

KUPATIKANA NA NYARA ZA SERIKALI.

Mnamo tarehe 27.07.2017 majira ya saa 16:00 jioni, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na askari wa TANAPA walifanya msako huko katika Pori la hifadhi ya Taifa la Ruaha lililopo Kijiji na Kàta ya Nyamlala, Tarafa ya Rujewa, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya, walifanikiwa kukamata Pikipiki 06 ambazo wahusika wake walikimbia na kuzitelekeza.
Kati ya Pikipiki hizo, mbili zilikuwa hazina plate namba na nyingine zilikuwa na za usajili MC 386 BHW aina ya Kinglion, MC T.799 CTW aina ya T-Better, MC 755 ADJ, T.461 BZE. Aidha Pikipiki hizo baada ya kukaguliwa zilikutwa na Nyara za Serikali ambazo ni Ngozi moja ya Simba na vipande 15 vya meno ya Tembo. Upelelezi na ufuatiliaji unaendelea ili kuwabaini na kuwakamata wahusika wa tukio hili.


WITO:

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishina wa Polisi MOHAMMED R. MPINGA anatoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za mtu/watu wanaowatilia mashaka popote iwe ni kwenye vyombo vya usafiri au hata katika makazi yao, kutoa taarifa katika vyombo vya ulinzi na usalama  kwa ajili ya ufuatiliaji na uchunguzi zaidi. Aidha anatoa rai kwa madereva na wamiliki wa vyombo vya usafiri kuchukua tahadhari pindi wanaposafirisha abiria na kutoa taarifa mapema kwani wapo baadhi ni wahamiaji haramu.
                                              Imesainiwa na:
 [MOHAMMED R. MPINGA – DCP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA

No comments