Header Ads

Responsive Ads Here

Msimshambulie Magufuli kukataza Wenye Ujauzito Warudi shuleni-Askofu


4
Na Jonas Kamaleki- MAELEZO
Katazo la Rais John Pombe Magufuli  juu wasichana wanao pata ujauzito  wakiwa shuleni kutoendelea na masomo ni sahihi kwani linalenga kurudisha maadili  na heshima kwa wanawake  hivyo hapaswi kushambuliwa kwa mitazamo hasi baadala yake  mashambulizi hayo yaelekezwe kuimarisha mikakati ya kila kijiji  wilaya na mikoa ya kumlinda  mtoto wa kike   na vitendo vya ubakaji.  

Kwa kufanya hivyo wanafunzi watapata ulinzi wa kudumu kuanzia shule za awali msingi na sekondari dhidi ya vitendo viovu.
Tamko hilo limetolewa  jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maadili,Amani na Haki za Binadamu kwa Jamii ya Madhehebu ya  Dini  zote Nchini, Askofu William Mwamalanga wakati akifunga  kongamano la siku mbili  lililoshirikisha vijana  2783 kutoka  wilaya za Tanzania Bara  ambao  ni wajumbe wa  kueneza  Maadili na Amani vijijini kupitia mpango maalumu wa kuwafikia vijana kujiepusha na maadili hatarishi ya matumizi ya dawa za kulevya na kupinga elimu ya ugaidi kwa vijana wote nchini.
Askofu Mwamanga ambaye amekuwa kwenye mtandao wa kusaidia vijana nchini kwa miaka 16 ameitaja kauli ya Rais Magufuli kuwa ni kauli ya ukombozi kwa watoto wa kike na wazazi kwani hakuna mzazi anayempeleka mtoto shuleni kwenda kupata ujauzito.
“Kumshutumu Magufuli ni kitendo cha kulea  majambazi wa umbakaji na ndoa za utotoni, hapa ni lazima Serikali iweke ulinzi  kwa wanafunzi wa kike wanaosoma shule za mbali na makazi ikiwa ni pamoja na kuwapima wasichana  wote wakati shule zinaanza kwa kila muhula  wa masomo”, alisema Askofu Mwamalanga.
 Mwenyekiti huyo amesema Rais Magufuli kwa hili yupo sahihi kwa asilimia 100 kwani  dawa ya dhambi ni kuikata kwa macho meupe na siyo vinginevyo kuanzisha mijadala kwamba  anawachukia wanawake siyo sahihi,  Magufuli ana mke  ana  watoto kama tulivyo sote  huyu ni mzazi  tena Rais  wa nchi  anayejua tabu na shida pale mtoto wa kike anapobeba mimba na kukatizwa elimu. Kauli yake ina maana  kwa wanafunzi kuzingatia elimu badala ya mapenzi,kwa watoto wa kike kuishikilia fursa ya elimu bure kwa nguvu kubwa  na wenye kusimamia ulinzi kwao kuongeza mkakati huo zaidi na si vinginevyo. 
Amewataka wakuu wa mikoa, wilaya, wakiwemo wakurugenzi wa Halmashauri za wilaya  na miji kuisimamia kauli ya Rais Magufuli kwa vitendo  kwa kuainisha maeneo hatarishi kwa wanafunzi wa kike ili wawe na ulinzi pamoja na kuanzisha ulinzi wa kuwafichua wabakaji kwa kila wilaya na kila kijiji baadala ya sasa  ambapo watendaji hao wamegeuka kuwa wapongezaji wa kauli za Rais na wengine wakianzisha ibada feki za kumuombea Rais kazi ambayo haiwahusu  kabisa  kwani kazi ya maombi na dua ni yao viongozi wa kiroho.
 Vijana hao kutoka mikoa yote ya Kanda ya Ziwa,  Mashariki,Nyanda za Juu Kusini, Magharibi  na Kanza ya Kusini, wamekiri kuwa  ubakaji  ni janga la kitaifa  kwa mikoa yote nchini jambo ambalo limefanya tatizo hilo kuanza kuzoeleka na baadhi ya wanafunzi  wasiopenda elimu kama njia ya kukwepa masomo ili waolewe, alisema Askofu Mwamalanga.
Aidha,  Askofu Mwamalanga amewaonya  baadhi ya wanasiasa na wanaharakati kuacha mchezo wa kuchezea maisha ya wanawake  baadala yake  wawe na msimamo chanya wa kumsaidia mtoto wa kike.
Kuna wanasiasa  siku za karibuni walikuwa wakitetea wanafunzi wa kike wakijifungua wawe wanarudi shuleni  siku hizi wamegeuka  na  wanatetea  marufuku ya mtoto huyo huyo kutorudi shuleni watu wa namna hii hawafai kumsaidia msichana  wa kizazi cha leo, ameonya  Askofu huyo.
Vijana kutoka wilaya za Kyela,  Ileje, Simiyu, Hai, Moshi, Songea, Liwale, Masasi, Lindi Morogoro, Dodoma, Nzega,  Morogoro, Tabora, Chunya na Mbozi wamekiri kuwa wazazi wengi kwenye wilaya hizo ndiyo kikwazo kikubwa kwa wanafunzi kupata mimba wakiwa shuleni kutokana na wazazi au  walezi hao kupokea mahari wakati mtoto akiwa shuleni, hivyo katazo la Rais Magufuli litaokoa wasichana wengi kama siyo wote.
Askofu Mwamalanga aliongeza kuwa baadhi ya vijana hao ambao ni walimu wa shule za msingi kutoka   wilaya za  Mtwara,Lindi, Tunduru, Mbinga, Makete, Ukerewe Mpanda, Kasulu,Tarime, Geita, Bukoba, Tabora, Kaliua, Momba, Dodoma Vijijini wameonya kuwa  ili kumaliza tatizo la mimba shuleni ni lazima katazo la Rais lisimamiwe na wizara ya Elimu, Halimashauri za wilaya,  madiwani na wenyeviti wa vijiji  kwa kuwashirikisha walimu na wazazi kazi ambayo ni muhimu na huko ndiko kumpongeza Rais.
Naye  Shekhe  Kassimu Rajabu amewahimiza vijana hao kwenda kuyatendea kazi yote waliyojifunza kwenye kongamano hilo la aina yake ambalo limewashirikisha vijana wa dini mbali mbali nchini.
“Twendeni tukawe wajumbe mkoani mwetu ili kuibadilisha jamii ya vijana kutoka kwenye uhalifu mbalimbali ukiwemo ugaidi ambao unawanyemelea sana vijina na kuashiria uvunjifu wa amani”, alisema Shekhe Rajabu
Hivi karibuni akizindua Barabara ya Bagamoyo- Msata, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alipiga marufuku wanafunzi wa kike kurudi shuleni baada ya kupata ujauzito. Kauli ya Mhe. Rais imeungwa mkono na watu wenye maadili na kupingwa na wanaharakati hasa asasi za kiraia.

No comments