Header Ads

Responsive Ads Here

HALMASHAURI YA WILAYA TABORA YANUNUA NYUMBA ZA NHC KWA AJILI YA WATUMISHI

index
Na Tiganya Vincent-RS-Tabora     
 
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeikabidhi Halmashauri ya Wilaya ya Tabora nyumba 32 zenye thamani ya shilingi bilioni 1.8 ambazo zitalipwa kwa kipindi cha miaka saba.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya pande zote kukaa chini na kusainiana Mkataba wa kuuziana nyumba hizo bei kwa ajili makazi ya Watumishi wa Halmashauri hiyo ambao walikuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu kwa sababu ya ukosefu wa nyumba za watumishi katika eneo la ofisi yao.

Nyumba hizo zilikabidhiwa jana na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angeline Mabula (Mb),kwa niaba ya NHC katika eneo la Isikizya Wilayani Uyui.

Akizungumza kabla ya kukabidhi nyumba hizo alisema ni vema Halmashauri ya Wilaya ya Tabora ikaheshimu makubaliano ya kuuziana nyumba hizo ya kulipa kila mwezi shilingi milioni 260 kama walivyokubaliana ili fedha zitakazopatikana ziweze kusaidia katika ujenzi wa nyumba  katika meneo mengine.

Katika hatua nyingine Mhe. Mabula alizitaka Halmashauri zote za Wilaya hapa nchini zihakikishe zinapima na kupanga matumizi bora ya ardhi ili kuzuia migogoro ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara katika maeneo mbalimbali.

Alisema hatua hiyo itasaidia katika uondoaji wa migogoro ambayo imekuwa ikisababisha mapigano na itawezesha miji na vijiji kupangika vizuri.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri alisema kuwa baada ya Halmashauri hiyo kununua nyumba hizo hakutakuwepo kwa kisingizio cha mfanyakazi kuishi Tabora mjini badala yake wanatakiwa kuwepo wakati wote eneo la Isikizya.

Alisema hatua hiyo itasaidia kuipungizia mzigo Halmashauri ya Wilaya ya Tabora wa gharama zikiwemo za matumizi ya mafuta ya magari ambayo yalikuwa yakitumika kuwasifirisha watendaji kutoka Tabora Mjini hadi eneo ilipo Ofisi ya Halmashauri hiyo.

Mkuu huyo wa Mkoa alisisitiza kuwa hivi sasa hataki kuona Mfanyakazi anaishi nje ya eneo hilo kwa kisingizio cha kukosa nyumba ya kuishi.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tabora Hadija Makuwani alilishukuru Shirika la Nyumba kwa kuwauzia nyumba hizo ambazo wanapaswa kulipa deni hilo kwa kipindi cha miaka saba kwa kiwango cha shilingi milioni 260 kila mwaka.
 
Aliongeza kuwa wataheshimu mkataba waliofikia na Shirika la Nyumba wa kulipa kila mwezi ili ndani ya kipindi walichokubaliana wamalize deni.

No comments