Header Ads

Responsive Ads Here

CHAWATA Chaiomba Serikali Kuwaondolea Kodi ya Bajaji

Na Neema Mathias – MAELEZO
Chama cha Walemavu Tanzania (CHAWATA) kimeiomba Serikali kuondoa kodi kwa bajaji (pikipiki zenye magurudumu matatu) zinazotumiwa na watu wenye ulemavu kama miguu na pia kubeba abiria ili kujipatia kipato.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa CHAWATA John Mlabu mapema leo Jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu changamoto na ajira kwa watu wenye ulemavu.
“Kupitia fursa ya kuondolewa kodi kwa vifaa vya watu wenye ulemavu tunaiomba Serikali izitambue bajaji kuwa ni moja ya nyenzo inayomsaidia mtu mwenye ulemavu na hivyo ziondolewe kodi, na Serikali iziagize kwa wingi na kuzikabidhi kwa watu wenye ulemavu kwa mkopo kupitia Umoja wa Waendesha Bajaji Dar es Salaam (UWAWABADA),” amesema Mlabu.
Ameendelea kwa kusema, kupitia UWAWABADA bajaji hizo zitatawanywa kote nchini kwa utaratibu walionao ili ziwainue kiuchumi na kuboresha maisha yao na familia zao.
Aidha Mlabu amesema, CHAWATA kinamuomba Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali yake kuangalia kundi hilo kupitia mafanikio ya watu wenye ulemavu Jijini, Dar es Salaam na kurasimisha shughuli ya uendeshaji wa bajaji kuwa ya watu wenye ulemavu pekee na wengine wasio na ulemavu waendeshe pikipiki za kawaida (Bodaboda).
“Kuendesha Bajaji ni ajira pekee ambayo haina usumbufu kwetu na imeyagusa makundi yote ya wanawake na wanaume tena rika zote, maana kwenye ujenzi wa viwanda na makampuni sisi hatuajiriwi, licha ya uwepo wa sheria Na. 9 ya 2010 ya ajira kwa walemavu inayotaka kila mahali pa kazi 3% ya watumishi wake wawe watu wenye ulemavu,” amefafanua Mlabu.
Vile vile amesema, uwepo wa chombo hicho cha magurudumu matatu kimewasaidia sana walemavu kujipatia kipato na kuwaondoa katika maisha ya kuombaomba kama ilivyokuwa hapo awali, aidha amesema kuwa wanaichangia Serikali katika kukuza uchumi wa nchi kupita kodi mbalimbali za Serikali pale wanaponunua mafuta ama vipuli vya bajaji zao.
CHAWATA kimeipongeza Serikali ya Awamu ya Tano na Rais Dkt. Magufuli kwa kujali watu wa tabaka la chini na maskini katika Taifa hili, ambapo wameshuhudia mara nyingi katika ziara zake akiwatetea wafanyabiashara wadogo (Machinga), Wakulima na Wafugaji, hivyo wanamuona Rais Magufuli kuwa ni Rais wa wanyonge.

No comments