Header Ads

Responsive Ads Here

BARABARA ZA WILAYA YA TANGANYIKA NA UVINZA KUJENGWA KWA CHANGARAWE


KATE1
Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Ndugu Salehe Muhando (Wa tatu) kushoto akitoa taarifa ya Wilaya yake kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani(Katikati) wakati wa ziara yake ya kukagua miundombinu ya barabara na madaraja Mkoani Katavi.

KATE2
Meneja wa Wakala wa barabara ( TANROADS) Mkoa wa Katavi Eng. Abdon Maregesi (Wa tatu kulia) akifafanua  ramani ya mtandao wa barabara iliyopo katika Wilaya ya Tanganyika kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (Kushoto) wakati wa ziara yake ya kukagua miundombinu ya barabara na madaraja Wilayani hapo.
KATE3
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (Wa pili kulia) akipokea maelezo kutoka Meneja wa Wakala wa barabara (TANROADS) Mkoa wa Katavi Eng. Abdon Maregesi (Wa pili kulia) wakati alipotembelea kambi ya Mkandarasi anayejenga barabara ya Mpanda -Vikonge (35KM) Kwa kiwango cha lami Wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi.
KATE4
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (Kulia) akitoa maelekezo Meneja wa Wakala wa barabara (TANROADS) Mkoa wa Katavi Eng. Abdon Maregesi (Wa pili kulia) wakati alipokagua barabara ya Mpanda -Vikonge (35KM) , Ifukutwe – Mwese (Km 109) na Mwesi hadi  Mto Lugosi mpakani mwa katavi na kigoma.
KATE5
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akielekea kukagua Daraja la Lugosi ambalo ujenzi wake umekamilika, Daraja hili linaunganisha Wilaya ya Tanganyika na Uvinza.
……………………………………………………………………
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani amemtaka Meneja wa wakala wa Barabara nchini (TANRODS) mkoa wa Katavi na Tanroads mkoa wa Kigoma kushirikiana ili Kuunganisha Wilaya ya Tanganyika na Uvinza kwa Barabara za kiwango cha changarawe ili kurahisisha usafiri kwa wakazi wilaya hizo.
Naibu Waziri Ngonyani ametoa agizo hilo baada ya kukagua ujenzi wa kiwango cha lami barabara ya Mpanda -Vikonge (35KM), Ifukutwe – Mwese (Km 109) na Mwesi hadi  Mto Lugosi mpakani mwa katavi na kigoma.
“Ni wakati muafaka sasa kufungua Barabara hizi hadi ukanda wa Ziwa Tanganyika ili kurahisisha usafiri kwa wananchi kwa njia ya barabara baada ya kuwepo changamoto ya usafiri wa majini kupitia Meli ambazo kwa sasa ni chache hivyo kukamilika kwa miradi hiyo kutafanya uwepo wananchi wawe na usafiri wa uhakika,” amesema Eng. Ngonyani.
Ameongeza kuwa serikali itachukua hatua za haraka kuhakikisha wanachi wa Wilaya ya Tanganyika wanakuwa na barabara za uhakika zitakazorahisisha  usafirishaji wa mazao na hivyo kupandisha thamani ya mazao hayo kwa wananchi.
Kwa upande wake Meneja wa TANROADS Mkoa wa Katavi Eng. Abdon Maregesi amemuhakikishia Waziri Ngonyani kuwa atahakikisha barabara hizo zinafanyiwa matengezo ya mara kwa mara ili kuzifanya zipitike kwa urahisi katika vipindi vyote vya mwaka.
Kwa upande wa  huduma za mawasiliano ya simu, Eng. Ngonyani amesema Wizara yake itashirikiana na kampuni za simu zilizopo nchini pamoja na mfuko wa mawasiliano kwa wote (UCSAF) ili kuhakikisha sehemu ambazo hazina mawasiliano ya huduma za simu ya  uhakika zinapata mawasiliano.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Katavi Ngugu, Saleh Mhando amesema kukamilika kwa Barabara hizi kutafungua fursa za kibiashara na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa pande mbili za wilaya ya uvinza na Tanganyika.
“Wananchi wa Wilaya hizi hufanya shughuli za uvuvi hivyo  kuimarisha kwa barabara hizi kutarahisisha usafirishaji wa  samaki kufika katika masoko kwa wakati na hivyo kukuza kipato cha wananchi wa ukanda huu wa ziwa Tanganyika,” amesema Mhando.
Naibu Waziri Eng. Ngonyani yupo katika Ziara ya kukagua Miundombinu ya barabara, Viwanja vya Ndege, Ujenzi wa Nyumba za viongozi na Madaraja katika Mkoa wa Katavi.

No comments