Header Ads

Responsive Ads Here

Wizara ya Mambo ya Nje yafanya usafi kwenye ufukwe wa Feri

Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki waadhimisha siku ya
mazingira duniani kwa kufanya usafi kwenye ufukwe wa Bahari ya Hindi
eneo la Feri jijini Dar es Salaam.  Wanaoenekana wakifanya usafi wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa
Idara ya Sera na Mipango, Bw. James Lugaganya akiwa pamoja na wafanya
kazi wengine wa Wizara.

Mkurugenzi msaidizi Idara ya Utawala na Rasilimali watu Bw. Hamid Mbegu (kushoto) naye akifanya usafi
Sehemu nyingine ya watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakijumuika kwa pamoja katika kufanya usafi kwenye ufukwe wa bahari eneo la Feri.
wakisomba taka
Sehemu nyingine ya watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakiendelea kufanya usafi
Usafi ukiendelea
Kaimu Mkurugenzi wa idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Jestas Nyamanga  akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya kumaliza zoezi la kufanya usafi kwenye ufukwe eneo la ferri

HOTUBA
YA BALOZI DKT. AZIZ P. MLIMA, KATIBU MKUU WA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA
USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI KATIKA SHUGHULI YA KUFANYA USAFI KWENYE UFUKWE
WA BAHARI YA HINDI, ENEO LA KIVUKONI (FERRY), DAR ES SALAAM
TAREHE
05 JUNI 2017
Waheshimiwa Mabalozi, Wakurugenzi na Makaimu Wakurugenzi kutoka Wizarani, Wawakilishi wa Mashirika
na Taasisi za Umoja wa Mataifa kwenye tukio hili; 
Uongozi wa Kata ya Kivukoni ukiongozwa na Mhe. Henry Massaba, Diwani wa Kata ya Kivukoni; Uongozi wa Mtaa wa Kivukoni ukiongozwa na Ndugu Gasper Makame, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa KivukoniWafanyakazi wa Wizara na Taasisi zilizo chini
ya Wizara; Wananchi wote mlioshiriki; Waandishi wa Habari; Mabibi na Mabwana.
Awali ya yote, napenda kuwasilisha salamu kutoka kwa Mhe. Waziri, Dkt. Augustine P. Mahiga (Mb.), pamoja na Mhe. Naibu Waziri, Dkt. Susan A. Kolimba (Mb.). Wanawasalimu sana na walitamani wajumuike nasi kwenye zoezi hili, ila kutokana na kubanwa na majukumu mengine ya kitaifa wameshindwa. Lakini wamefurahishwa na hiki tulichokifanya na wanatupongeza sana.
Wizara inawashukuru sana wote mliojumuika nasi kwenye tukio hili muhimu la kusafisha mazingira ya ufukwe huu tunapoadhimisha Siku ya Mazingira Duniani.
Maadhimisho haya kidunia yanafanyika nchini Canada, na kwa hapa Tanzania, yanafanyika kitaifa huko Butiama, Mkoani Mara, chini yakaulimbiu: “Hifadhi ya Mazingira: Muhimili kwa Tanzania ya Viwanda”.
Kaulimbiu hii inatukumbusha kuwa tunapoelekea kwenye Tanzania ya Viwanda na Uchumi wa Kati, hatuna budi kutunza mazingira, kwani rasilimali tunazozihitaji kutimiza azma yetu hii adhimu zinapatikana kwenye mazingira na mazingira ndiyo maisha yetu. Hivyo utajiri wetu wa kwanza ni mazingira.
Tumechagua kufanya zoezi hili la usafi kwenye ufukwe wa bahari kwa sababu tunapozungumzia
utunzaji wa mazingira, suala la utunzaji wa bahari linasahaulika. Hivyo, sisi tunaikumbusha jamii kuwa bahari nayo ni sehemu ya mazingira, ni urithi wetu, ni lazima tuitunze.
Kwa bahati, wakati sisi tunafanya zoezi hili, leo hii pia kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, huko New York, dunia inakutana kujadili namna ya kuhakikisha uhifadhi wa bahari na matumizi endelevu ya rasilimali zake, ukiwa ni Mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa kuhusu suala hili. Hivyo, ndugu wananchi wenzangu, naomba tuone umuhimu wa kutunza bahari, tunaitegemea sana kwenye uchumi wetu na maisha yetu ya kila siku, tuache kuichafua kwani ikipoteza uhai ni hasara kwetu sote.
 Mtakubaliana nami kuwa, bila kufanya zoezi hili kwa ushirikiano, tusingefanya chochote cha
msingi hapa. Basi, na hili liwe funzo wakati huu tunapotekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na Makubaliano ya Paris ambayo yote yanasisisiza uhifadhi wa mazingira. Bila ushirikiano, itakuwa vigumu kutimiza azma hiyo ya Makuibaliano ya Paris na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs). Dunia ni yetu sote, inatutunza sote, inatukirimia sote sawa sawa, basi sote tuna jukumu la kuitunza, tena kwa ushirikiano.
Kabla sijamaliza kuzungumza, napenda kutumia nafasi hii kuishukuru Ofisi ya Umoja wa Mataifa hapa nchini; Uongozi wa Manispaa ya Ilala na Kata ya Kivukoni kwa misaada yao ya hali na mali katika kufanikisha zoezi hili. Tunawashukuru sana.
Asanteni sana kwa kunisikiliza!

No comments