Header Ads

Responsive Ads Here

UKUSANYAJI KODI KIELEKTRONIKI KUONGEZA PATO LA TAIFA


12
Na Jonas Kamaleki
Kati ya mambo ambayo yamekuwa yakimuumiza kichwa Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli ni ukusanyaji wa kodi hivyo juhudi za makusudi zimefanyika ili kutimiza azma hii.

Serikali ya Awamu ya Tano imetekeleza ahadi yake kwa wananchi ya kuongeza pato la Taifa kwa kukusanya kodi. Azma hii imetekelezwa kwa vitendo kwani mwanzoni  mwa utawala wa Rais Magufuli mapato yatokanayo na kodi yameongezeka kutoka takriban bilioni mia nane hadi kufikia trilioni 1.3 kwa mwezi.
Hivi karibuni, Rais Magufuli amezindua Mfumo Mpya wa Ukusanyaji kodi kwa njia ya Kielektroniki (Electronic Revenue Collection System (e-RCS), mfumo ambao unatarajiwa kuongeza mapato kwa kiwango kikubwa.
Akizindua Mfumo huo, Rais Magufuli alitoa agizo kwa makampuni ya simu na kusema, “Nimepata taarifa kuwa hadi sasa Kampuni za simu za TTCL, Hallotel na Smart ndizo pekee zilizojisajili katika mfumo huu, sasa natoa wito kwa makampuni mengine na mabenki yahakikishe yanasajisajili kabla ya mwezi Desemba mwaka huu”.
Ili kuwezesha mfumo huo kufanya kazi, makampuni yote ya simu, mabenki na yale yanayofanya miamala kwa njia ya kielektroniki yanapaswa kujisajili katika Kituo cha Taifa cha Kuhifadhia Taarifa (Data Centre) ambacho kina uwezo wakuona kila muamala unaofanyika na kufanya ukokotozi wa kodi inayostahili kulipwa.
Mfumo huu kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kichere, ni sehemu ya mchakato wa ukusanyaji wa mapato unaojumuisha mifumo mbalimbali iliyowekwa pamoja kuweza kufanya ukadiriaji, tathmini na ukokotozi wa kodi kutoka kwenye miamala mbalimbali inayofanyika kielektroniki.
Ni Mfumo ambao unahusisha moduli tisa zinazofanyakazi mwanzo hadi mwisho kuhakikisha kodi inakusanywa, inakadiriwa na kupelekwa moja kwa moja kwenye akaunti za Mamlaka ya Mapato Tanzania na Bodi ya Mapato Zanzibar ambazo zipo Benki Kuu. Amezitaja moduli hizo kuwa ni : moduli ya kukusanya taarifa, kutunza taarifa, kuhakiki taarifa na kushirikisha mifumo. Moduli nyingine ni ya kuzuia udanganyifu, ya kukusanya kodi, ya kutoa ripoti, ya usalama wa miundombinu na moduli ya kutoa taarifa kwa kinachotokea. 
Bwana Kichere anaeleza kuwa imekuwepo mifumo mingine ya kukusanya mapato kielektroniki ambayo imeonyesha kuwa na mianya ya kukwepa kodi. Kuhusu mifumo mingine Kamishna Mkuu anasema baadhi ya mifumo ambayo imeanzishwa na inatekelezwa kuanzia kipindi cha mwaka 2012  ni kama ifuatavyo:
Electronic Cargo Tracking System (ECTS). Mwaka 2012 Mamlaka ya Mapato Tanzania iliunda mfumo kufuatilia mizigo ipitayo katika bandari ya Dar es Salaam kuelekea nchi  jirani. Mfumo huu umesaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa tatizo la ukwepaji wa kodi kwa mizigo iliyokusudiwa kupelekwa nchi jirani
Mfumo wa Kielektroniki wa ulipaji Kodi (Revenue Gateway System) ulianzishwa mwaka 2013 na unawasiliana na Benki Kuu pamoja na benki za kibiashara hivyo unamuwezesha mlipakodi kufanya malipo ya kodi mbalimbali kupitia benki au kwa kutumia simu ya kiganjani akiwa mahali popote na hivyo kuondoa usumbufu kwa mlipakodi. Pia mfumo huu unawezesha upatikanaji wa taarifa sahihi za mapato ya Serikali kwa wakati.
Mfumo wa kielektroniki wa Forodha yaani Tanzania Customs Integrated System (TANCIS). Mfumo huu ulianzishwa mwaka 2014 na unatumika kuthaminisha mizigo na kukadiria kodi ili kodi sitahiki ilipwe pamoja na kuratibu shughuli za uondoshwaji mizigo maeneo ya forodha. Mifumo hii yote imewezesha kuongeza mapato kutoka wastani wa shilingi trilioni 3.4 mwaka 2013/14 hadi trilioni 5.2 kwa mwaka 2015/16.
Bwana Kichere anafafanua kuwa Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) imegundua kwamba kuna mianya ya kimfumo inayoikosesha serikali mapato kutoka kwa walipakodi mbalimbali.
Changamoto ni kubwa zaidi kwenye huduma zitolewazo kwa mifumo ya kielektoniki ya makampuni ya simu (Mobile Network Operators) ambapo wahusika hutoa huduma na kupata mapato yao mara moja, wakati ambapo kodi (kodi yaongezeko la thamani – VAT na ushuru wa bidhaa – (Excise Duty) inayopaswa kulipwa kwa serikali inategemea mawasilisho ya makadirio kutoka kwa makampuni husika. Hali hiyo, husababisha baadhi ya makampuni kutumia mwanya huo kuipunja serikali kodi stahiki.
Ili kukabiliana na changamoto hizi, TRA na ZRB kwa kushirikiana na taasisi nyingine za serikali zimeunda mfumo utakaowezesha kutathmini, kukusanya na kuhasibu kodi kwa njia ya kielektoniki moja kwa moja bila kuathiriwa na utashi wa mtu (without human intervention). 
Ndoto ya Rais Magufuli ya kubuni vyanzo vingine vya ukusanyaji mapato inaanza kutimia baada ya bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka 2017/18 kuanisha vyanzo hivyo.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango akiwasilisha makadrio ya bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha unaoanza Julai 1, 2017 anasema, “Serikali itatoza Kodi ya Majengo kwa nyumba zote kwa viwango vitakavyopangwa na Waziri na Fedha na Mipango. Nyumba ambazo hazijafanyiwa uthamini zitatozwa kwa kiwango maalum (flat rate) cha shilingi elfu kumi (10,000) kwa nyumba na shilingi elfu hamsini (50,000) kwa nyumba za ghorofa kwa kila ghorofa.
“Serikali itawatambua rasmi wafanyabiashara wadogo wadogo wasio rasmi na wanaofanyia biashara katika maeneo yasiyo rasmi mfano mama lishe, wauzaji mitumba wadogo, wauza mazao ya kilimo wadogo kama mboga mboga, ndizi, matunda, na kadhalika kwa kuwapatia vitambulisho maalum vya kazi wanazozifanya”, alisema Dkt. Mpango.
Katika kutekeleza suala la ukusanyaji wa mapato kielektroniki, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imezindua Mfumo wa kukusanya kodi ya pango la ardhi kwa njia ya kielektroniki. Mfumo huu umeonyesha kuwa ni bora katika kuongeza ukusanyaji wa mapato.
Kwa Mfumo huo, mlipaji kodi hahitaji kwenda Wizarani au kituo cha malipo kulipa kodi bali anaweza kufanya hivyo akiwa mahali popote kwa kutumia simu yake ya mkononi kwa kupitia menyu kuu ya Taifa ambayo ni *152*00#. Njia hii itamwondelea mlipaji usumbufu ikiwemo kupoteza muda mwingi kutoka napokaa na kufika Wizarani kwa ajili ya kulipia kodi.
Mkuu wa Kitengo cha Kodi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Denis Masami ansema kuwa katika kipindi kifupi tangu mfumo huo uanze kutumika, mapato yameongezeka kwa shilingi milioni 9 ndani ya siku tano. Hii ni kutoka bilioni 2 hadi bilioni 2.9 kwa siku tano. Mwenendo huu wa ongezeko unaonyesha kuwa kwa mwezi hadi kwa mwaka mapato yataongezeka kwa kiwango kikubwa.
Naye Mkurugenzi wa Mifumo ya Kifedha wa Wizara ya Fedha na Mipango anasema kuwa kwa kutumia mfumo huo mtu atatumiwa ujumbe wa majibu kuonyesha kiasi cha fedha alicholipia ambao utahesabika kama risti.
Hakika mifumo hii ikisimamiwa barabara, ni dhahiri kuwa changamoto za kibajeti zitapungua. Kulipa kodi ni suala la msingi na ndiyo maana kwenye nukuu za Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuhusu kodi zinasema, “Serikali ya wala rushwa haiwezi kukusanya kodi”. Mwalimu alisisitiza ukusanyaji wa kodi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi zikiwemo huduma za kijamii kama vile; elimu, afya, maji safi na salama na miundombinu.

No comments