Header Ads

Responsive Ads Here

RC TABORA WOTE LAZIMA WAJIOROSHE KWA VIONGOZI WA MITAA


TAB1
Na Tiganya Vincent

Viongozi wa Serikali za mitaa na vitongoji wametakiwa kuhakikisha kuwa wageni wote wanaoingia mkoani Tabora wanafahamika na kuwaorodhesha katika vitabu vyao kabla ya kuendelea na shughuli nyingine zilizowaleta ili kuepuka kupokea watu ambao wanaweza kuwa wamekusudi la kuja kushirikiana na baadhi ya wenyeji kuendesha vitendo vya kihalifu ikiwa ni pamoja na ujambazi.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri jana wilayani Tabora wakati akifunga mafunzo wa vijana  wa Jeshi la Kujenga Taifa Opereshi Magufuli katika Kikosi  cha Jeshi cha 823 JKT Msange.

Alisema kuwa lengo la kufanya hivyo ni kutaka kumjua kila mgeni anayeingia na kutoka kwa ajili ya kuondoa vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na wageni kwa kushirikiana na wenyeji wasio na moyo wa uzalendo na nchi yao na kuwasababishia maumivu watu wengine wanakuwa katika kujiletea maendeleo kwa njia halali.

Bw. Mwanri alisisitiza kuwa mara kiongozi wa Mtaa au Kitongoji akiona mgeni ambaye hafahamiki ni vema kuomba utambulisho wake kutoka kwake na mwenyeji wake ikiwa ni pamoja na  shughuli iliyomleta mkoani Tabora na siku atakazokaa mkoani humo.

Alisema kuwa kusipokuwepo na utaratibu wa kuwafatilia wageni wote wanaoingia kila siku na kutoka Mkoani humo kuna uwezekano wa kukaa na majambazi ambayo yanakuja kufanya uhalifu kisha wanaondoka na baada ya muda warudi tena.

Mkuu huyo wa Mkoa alitoa wito kwa wananchi watakaowapokea wageni kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya mkoa huu kutoa taarifa kwa viongozi wao wa mtaa au kitongoji  bila kuficha utambulisho wao halisi ili wasije wakaingia katika matatizo endapo uhalifu utatokea katika maeneo yao.

Alisema kuwa mwenyeji yoyote anayekataa kutoa taarifa za uwepo wa mgeni kwake atachukuliwa kuwa nia mbaya na jamii inayomzuka na iwapo uhalifu utatokea yeye ndiye atakuwa wa kwanza kusaidia vyombo vya dola.

 “Kwa Mkoa huu nawaagiza watendaji wote kuanzia ngani ya mtaa, kitongoji na kijiji muhakikishe kuwa hakuna mtu kuishi hapa kama ajapitia katika Ofisi zenu …hatua hii itatusaidia kujua wageni wanaoingia na kutoka mkoani mwetu” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.

“Tayarisheni utaratibu wa kuwaorodhesha wageni wote ikiwa ni pamoja na kujua mwenyeji wake, alikotoka alikuwa anafanyakazi gani, hapa mkoani Tabora amekuja kufanya nini na atakuwepo kwa siku ngapi ili ikitokea shida tuweze kumpata kirahisi” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema katika kuwabaini wenyeji wanaoshiriki katika vitendo vya kihalifu ikiwemo kuwahifadhi majambazi  wataendesha zoezi la kupiga kura za siri na mtu atakayepata kura nyingi atashughulikiwa na vyombo vya dola.

Alisema kuwa mtuhumiwa lazima apate kura kuanzia sabini na kuendelea na ndipo atachukuliwa kwa ajili ya mahojiano kwa nini awe yeye na sio mwingine au aeleze kuwa aliishije na wenzake.

Awali Mkurugenzi wa Utumishi katika Jeshi la Kujenga Taifa Luteni Kanali Julius Kiyungi aliwasihi wahitimu wa mafunzo ya awali katika Kikosi cha Jeshi cha 823 JKT Msange kutotumia mafunzo yao vibaya kwa kuwapinga raia wema  kwa kuwa wao ni sehemu ya jamii ya watoto wa wakulima na wafanyakazi ambao wanahitaji ulinzi kutoka kwao.

Aliongeza kuwa ni vema wakatumia mafunzo waliyoyapata katika kipindi hicho cha miezi sita kushirikiana na Mamlaka husika zilizopo katika maeneo yao kufichua  watu waovu, wasaliti na wasioitakia mema nchi ya Tanzania.

Akisoma risala ya wahitimu wenzake 870 wa mafunzo ya awali Fred Mashauri alitoa wito kwa vijana wengine kuomba kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili waweze kufundisha jinsi ya kuwa wazalendo na walinzi wazuri wa jamii yao na  Taifa lao kwa ujumla.

Katika mafunzo hayo jumla ya wasichana 264 na wavulana 606 wametunukiwa vyeti vya kumaliza mafunzo ya awali kabla ya kwenda katika Kambi mbalimbali ili kujifunza stadi za maisha na ujarisiamali.

No comments