Header Ads

Responsive Ads Here

RC TABORA VIONGOZI WA DINI TUSAIDIE KUDHIBITI NDOA ZA UTOTONI


images
Na Tiganya Vincent, IGUNGA
 
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri amewaomba viongozi wa dini kuhakiki taarifa za binti kabla ya kufungisha ndoa ili kuona kama kweli umri wake unastahili kuanza maisha ya ndoa.
 
Bw. Mwanri alitoa wito huo jana wilayani Igunga wakati wa kongamano la Kwaya mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania linaloendelea katika eneo la Hospitali ya Rufaa ya Nkinga.
 
Alisema kuwa lengo la kuhakiki ni kutaka kukomesha mimba na ndoa za utoto ambazo zimezidi katika Mkoa wa Tabora na kurudisha nyuma maendeleo ya wasichana wengi.
 
Mkuu huyo wa Mkoa aliongeza kuwa tatizo hilo limekuwa gumu wakati mwingine wazazi wa binti wamekuwa wakishirikiana na upande wa mtu aliyempa mimba mtoto wao kwa kuficha ushahidi na kufanya kesi zinapelekwa Mahakama kufutwa.
 
Aliwaomba viongozi hao wa kihoro kabla ya kufungisha ndoa wakafanya mahojiano na binti anayekwenda kuandikisha ndoa na mwenzie ili kubaini umri wake halisi na kama unastahili kufungishwa ndoa.
 
Bw. Mwanri alisema kuwa tatizo la mimba za utotoni limerudisha nyuma maendeleo ya mabinti wengi kwa sababu wengi wao hawamalizi shule.
 
Alisisitiza kuwa kama jamii nzima na viongozi kama hawatashirikiana katika kukabiliana na tatizo hilo Mkoa wa Tabora utaendelea kuwa nyuma kwa sababu watoto wa kike wasipoelimishwa sawa na wanaume hakutakuwepo na maendeleo.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka watu wazima waache watoto wa kike wasome kwani kufanya hivyo ni sawa na kuwekeza ili waje wawafae wakati wa uzee.
 
Mkoa wa Tabora ni miongoni mwa mikoa inayoongoza hapa nchini kwa mimba ya utotoni
 
Kongamano hilo la Kwaya ambalo linawashiriki kutoka Tanzania, Kenya na Uganda limeandaliwa na Kanisa la FPTC na linalizika Jumapili hii.

No comments