Header Ads

Responsive Ads Here

PEMBA:SERIKALI WILAYA YA WETE KUCHUKUA HATUA KALI DHIDI YA WANANCHI WALIOJENGA NYUMBA KWENYE MASHAMBA YA SERIKALI BILA KUFUATA UTARATIBU


Na Masanja Mabula -Pemba .
 
SERIKALI Wilaya ya Wete imesema itachukua hatua kali dhidi ya wananchi waliojenga nyumba kwenye mashamba ya serikali  bila ya kufuata utaratibu ikiwa ni pamoja na kuvunjiwa nyumba zao .
 
Shehia ambazo zimetajwa kukithiri vitendo hivyo ni pamoja na Finya, Kinyasini pamoja na Ukunjwi.
 
Akizungumza ofisini kwake Wete Mkuu wa Wilaya hiyo  Rashid Hadid Rashid amesema  katika kutekeleza agizo hilo , Serikali haitakuwa na muhali na mwananchi ambaye atabainika kujenga nyumba sehemu za maeneo ya kilimo bila ya kufauata taratibu.

Amesema tayari wanaendelea kuwasiliana na masheha kuyafuatilia  na kuyatambua mashamba yote ya Serikali ili iwe rahisi kuweza kuwafahamu wananchi waliojenga katika maeneo yasiyoruhusiwa.

“Tumeandaa utaratibu wa kuyakagua mashamba yote ya Serikali na kwamba tukibaini mwananchi kajenga nyumba bila ya kufuata taratibu hatutasita kumvunjia jengo lake “alieleza.

Aliongeza kwamba “Tayari tumeshusha agizo kwa masheha kuyatambua mashamba yote ya Serikali pamoja na maeneo ya Kilimo yaliyojengwa nyumba za kuishi kinyume na taratibu za kisheria “alisisitiza.

Aidha Mkuu huyo wa Wilaya amezidi kueleza kwamba wananchi ambao wameuziwa mashamba ya Serikali wajihesabu wamepoteza kwani mashamba hayo ni mali ya Serikali na hayauzwi .

Naye Sheha wa shehia ya Kinyasini Raiya Amour Othman amesema katika shehia hiyo wameibuka wananchi wanaojiita madalali wa kuuza mashamba na asilimia kubwa ya ardhi zinazouzwa ni mashamba ya eka .

Amesema Serikali ya Shehia imechukua hatua za makusudi kuwaelimisha wananchi kujiepusha na matapeli hao wanaouza mashamba ya Serikali kwani hawana mamlaka ya uwezo wa kuuza mashamba hayo.

No comments