Header Ads

Responsive Ads Here

Mwenendo wa Serikali Katika Kupambana na Rushwa, Usimamizi wa Rasilimali na UwajibikajiKituo cha Sheria na Haki za Binadamu ni shirika lisilo la kiserikali lenye maono makuu ya kuona Jamii yenye Haki ya Usawa Tanzania. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimekuwa mstari wa mbele kuhamasisha Utawala Bora kwa Maendeleo ya Taifa letu. Katika misingi mikuu ya utawala bora “Uwajibikaji na Uwazi” ni tunu adhimu inayopaswa kuenziwa.


Ndugu Wanahabari,

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimeendelea kufuatilia kwa karibu hatua za Serikali ya Awamu ya Tano hususani katika uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali za nchi. Moja ya hatua chanya zilizochukuliwa na serikali hivi karibuni ni hatua ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuunda kamati mbili kuchunguza thamani halisi ya kiwango cha madini kilichopo kwenye makasha yenye mchanga wa madini (maarufu kama makinikia) na hatimaye kupokea taarifa zenye mapendekezo mbalimbali na kuahidi kuyafanyia kazi.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinatumia fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dk. John Pombe Magufuli, kwa maamuzi haya makubwa hususani katika sekta ya madini.

Ndugu Wanahabari,

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimekuwa mstari wa mbele kupigania matumizi sahihi ya rasimali za nchi, hususani madini. Kupitia Ripoti ya Haki za Binadamu na Biashara na tafiti mbalimbali tunazofanya katika nyakati tofauti, tumekuwa tukipigia kelele sana juu ya mambo kadhaa kiwemo; kukosekana kwa uwazi katika sekta ya madini nchini, ukwepaji wa kodi, kuwepo kwa misamaha ya kodi kwa makampuni ya uchimbaji dhahabu isiyo na tija kwa taifa, pamoja na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu maeneo ya mgodi hususani wilayani Tarime.

Ndugu Wanahabari,

Mnamo Juni, 9 mwaka 2017 Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kilitoa tamko hapa mbele yenu kupinga kusudio la Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) kuiongezea muda wa kuzalisha umeme kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kwa muda wa miezi 55. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinapongeza hatua zote zilizochukuliwa ikijumuisha hatua kubwa ya wamiliki na wa wahusika wakuu wa Kashfa ya Tegeta Escrow ambao ni zao la Kampuni hii ya IPTL kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria. 

Hatua hii sio tu inatuletea heshima kama taifa lakini pia inarudisha imani ya watanzania kwa Serikali kwamba dhana ya uwazi na uwajibikaji inawezekana. Pia inafuta dhana iliyojengeka kwa muda mrefu ya viongozi kulindana kwa maslahi binafsi na kuumiza maslahi mapana ya taifa.


Ndugu Wanahabari,

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu tuanona uwepo wa utashi wa kisiasa katika kumaliza vitendo vya rushwa vinavyodidimiza maendeleo ya Tanzania, hivyo pamoja na pongezi hizi za dhati, tunaikumbusha Serikali mambo yafuatayo:

1. Serikali kuunda Mamlaka kamili ya Madini itakayokuwa inafanya kazi ya uratibu wa shughuli zote za madini Tanzania kama zilivyo mamlaka za hifadhi ya jamii. Mamlaka hii itafanya shughuli zote za uratibu wa mikataba ya madini, kufuatilia mapato yatokanayo na madini, kuidhinisha vibali na leseni zote za madini, kuendeleza miradi mbali mbali ya uchimbaji wa madini ya vito vya thamani, kuratibu soko la madini ambapo madini yote yatauzwa hapa Tanzania ili kuweza kupata fedha za kigeni.

2. Serikali, iwachukulie hatua wale wote waliotajwa na katika ripoti za kamati zote mbili na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria kujibu tuhuma hizi nzito.
3. Serikali, iwachukulie hatua watu wote na wanufaika wa miamala ya fedha za Tegeta Escrow bila kujali nafasi zao, vyeo vyao, kazi zao na nafasi yao katika jamii. Itakumbukwa kwamba Tegeta Escrow iliwanufaisha wanasiasa ambao wana mahusiano ya moja kwa moja au ya karibu na wizara ya nishati na madini, majaji wa mahakama kuu Tanzania, viongozi wa serikali na viongozi wetu wa kiroho (Maaskofu).

4. Kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo wa ndani ili kuanzisha soko rasmi la madini yanayozalishwa na wachimbaji wadogo katika maeneo tofauti kama vile Chunya - Mbeya, Mererani - Arusha, Handeni-Tanga ili kuinua uchumi wa wananchi moja kwa moja.

5. Serikali ipige marufuku usafirishwaji wa madini kama dhabahu moja kwa moja kutoka katika viwanja vya ndege vilivyopo katika baadhi ya maeneo ya migodi. Katazo hili liendane moja kwa moja na kufungwa kwa viwanja vyote vya binafsi vilivyopo ndani ya maeneo ya migodi hii.

6. Serikali kuheshimu na kudumisha demokrasia kwani kupitia demokrasia ndipo vyama au watu wanaweza kukosoa utendaji wa serikali na kuikumbusha juu ya masuala mbalimbali na kusaidia kuimarisha serikali.

7. Serikali kuheshimu na kulinda misingi ya haki za binadamu kwani maendeleo ya kiuchumi/viawanda huambatana na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

8. BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania libadilike kuendana na kasi ya Serikali, lisiendeshe mijadala kisiasa bali kwa lugha za kibunge na kutanguliza maslahi ya nchi  mbele. 

Tumefika hapa na kashfa hizi kubwa za Rushwa zimedumu kwa miongo kadhaa
kwa sababu ya Bunge dhaifu lisiloweza kuisimamia serikali kwa dhati hususani katika mambo makubwa ya kitaifa. Zaidi kila hoja inayo wakilishwa ipewe uzito pasipo kujali itikadi za vyama ambazo zimekuwa kikwazo katika kupata muafaka kwenye mambo yenye maslahi ya taifa. Kwa mfano mapigamizi yaliyo letwa na upande wa upinzani kuhusu miswada ya dharua ya sheria za madini n.k.

9. Kuongeza ushirikiswaji na uwazi katika mambo makubwa yenye maslahi ya taifa ikiwemo kuwasilishwa bungeni kwa mikataba inayo ingiwa na serikali kwa ajili ya uchambuzi.

10. Serikali ichukue hatua katika kutatua kashfa nyingine ambazo zimechafua taswira ya nchi na kuisababishia serikali hasara. Baadhi ya kashfa hizo ni:
a) Kashfa ya ununuzi wa Rada ambayo ilidhihirika kuwepo kwa Rushwa katika manunuzi yake na kupelekea Serikali ya Uingereza kurudisha kiasi cha pesa kilichozidi nchini na kupelekwa katika sekta ya elimu kwa manunuzi ya vitabu. Wahusika katika kashfa hii wapo na hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi yao.
b) Kashfa ya inayohusisha kampuni ya Lugumi Enteprises; tunakumbusha Bunge letu tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuleta hadharani ripoti ya Kamati Ndogo ya Bunge iliyoundwa katika bunge la 10. Hii itasaidia kuweka uwazi na kama kuna viashiria vya rushwa na matumizi mabaya ya ofisi wahusika wafikishwe kwenye vyombo vya dola.

c) Kashfa ya Richmond; moja ya Kashfa kubwa za rushwa kuwahi kutokea nchini Tanzania.

Kashfa hii ilipelekea kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania mwaka 2008.

Ripoti hii ilitaja viongozi mbalimbali waliohusika kwa namna moja ama nyingine kuliingizia hasara ingawa hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa mpaka sasa. Tunaiomba serikali ilikumbuke hili katika kuenzi utawala bora unaopinga rushwa kwa vitendo.

d) Kashfa ya uwepo harufu ya Rushwa katika miradi mbalimbali inayotekelezwa na mifuko ya
hifadhi ya jamii, mathalani mradi wa NSSF Kigamboni ambao umesimama wakati
mabilioni ya shilingi yamewekezwa ikiwa ni fedha za mafao ya wananchi wa Tanzania.

Tunaomba Mh. Rais aitazame miradi yote mikubwa inayotekelezwa na mifuko hii ya hifadhi ya jamii kwa kuzingatia Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali.

e) Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu pia kinamkumbusha Mh. Rais kutazama kwa  ukaribu suala la vitalu vya uwindaji na umiliki wake, maslahi kwa taifa, mapato yatokanayo, na mustakabali wa vitalu vya uwindaji na uhifadhi wa mbuga zetu za wanyama na hifadhi zake.

Mwisho, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu tunapendekeza kuwepo kwa Katiba Mpya na bora itakayojenga taasisi imara, mifumo thabiti ya sheria na ulinzi mathubuti ya rasilimali zetu. Hii itafanya vita dhidi ya rushwa na matumizi mabaya ya rasilimali kuwa endelevu, ya kudumu, itakayotegemea uwepo wa taifa na si utayari na utashi wa kiongozi tunahitaji Katiba Mpya.Imetolewa Ijumaa Juni 22, 2017 na,

Bi. Anna Henga

Kaimu Mkurugenzi MtendajiNo comments