Header Ads

Responsive Ads Here

HakiElimu wazinduwa Kampeni kuhamasisha Elimu ya Mtoto

Mkurugenzi Mtendaji HakiElimu, John Kalage (katikati) akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari kuhusiana na uzinduzi wa kampeni maalumu ya kuhamasisha ufanikishaji wa elimu ya mtoto wa kike. Hafla hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Tafakari wa HakiElimu uliopo ofisi za taasisi hiyo leo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Meneja wa Programu ya Ujenzi wa Vuguvugu la Harakati ya Kumkomboa Mwanamke kutoka TGNP Mtandao, Grace Kisetu na Mkurugenzi, CAMFED-Tanzania, Lydia Wilbard (kulia) wakiwa katika mkutano huo.

Mkurugenzi Mtendaji HakiElimu, John Kalage (wa kwanza kushoto) akisisitiza jambo kwa wanahabari (hawapo pichani) katika uzinduzi wa kampeni maalumu ya kuhamasisha ufanikishaji wa elimu ya mtoto wa kike. Hafla hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Tafakari wa HakiElimu uliopo ofisi za taasisi hiyo leo jijini Dar es Salaam. Kutoka kulia ni Meneja Idara ya Habari na Utetezi HakiEli, Elisante Kitulo na Mkurugenzi, CAMFED-Tanzania, Lydia Wilbard wakiwa katika mkutano huo.

TAASISI ya HakiElimu leo kwa kushirikiana na asasi wadau wengine watetezi masuala anuai ya kijamii wamezinduwa kampeni maalumu ya kuhamasisha ufanikishaji wa elimu ya mtoto wa kike, huku ikiiomba Serikali kupitia wizara husika kukamilisha mchakato wa kumruhusu mtoto wa kike aliyepata ujauzito aendelee na masomo baada ya kadhia hiyo. Hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo imefanyika leo katika Ofisi za HakiElimu jijini Dar es Salaam. Hii apa taarifa nzima ya Mkurugenzi Mtendaji, HakiElimu, John Kalage akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari leo katika uzinduzi huo:- 

  TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI Utangulizi Ndugu Wanahabari; HakiElimu leo tunazindua kampeni maalumu ya kuhamasisha ufanikishaji wa elimu ya mtoto wa kike. Kampeni hii inatokana na ongezeko kubwa la changamoto za kimazingira, kiutamaduni, kiuchumi na za kimazoea ambazo zimekuwa zikirudisha nyuma sana haki ya upatikanaji wa elimu bora kwa mtoto wa kike nchini Tanzania. Katika Kampeni hii tunawataka wadau wote kutenga muda wa kutafakari na hatimae kuchukua hatua stahiki za kuboresha elimu ya mtoto wa kike hapa nchini. 

Elimu ya mtoto wa kike inahitaji tafakuri ya zaidi kutokana na kuwa na mahitaji maalumu ya ziada na hatari zinazowakabili watoto wa kike na kupelekea kukosekana usawa kati yao na watoto wa kiume katika kupata elimu. 

 Ndugu Wanahabari; Azimio la Incheon la Mwaka 2015 limesisitiza kuwepo na usawa na elimu jumuishi katika mfumo wa elimu kwa nchi zilizoliridhia. Uwepo wa usawa na elimu jumuishi kunalenga kuyawezesha makundi yote hasa wasichana, walemavu na watoto toka familia maskini kupata elimu bora na hatimaye kutimiza ndoto zao. 

 Lakini kumekuwepo na taarifa nyingi za unyanyasaji ambazo kwa kiwango kikubwa mwathirika amekuwa ni mtoto wa kike. Athari za unyanyasaji huu ni kubwa na zinahitaji juhudi za pamoja ili kuweza kumkwamua mtoto wa kike katika hatari ya kukosa haki yake ya kupata elimu bora na kufikia ndoto zake kama mwanadamu na kama raia yeyote mwingine wa Tanzania. . Hivyo, kwa kutambua hili, suala la ulinzi wa mtoto, hususani mtoto wa kike na wale wenye mahitaji maalumu, ni suala ambalo HakiElimu imelipa kipaumbele katika Mpango Mkakati wake Mpya wa Mwaka 2017-2021.  
Mkurugenzi Mtendaji HakiElimu, John Kalage (katikati) akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari kuhusiana na uzinduzi wa kampeni maalumu ya kuhamasisha ufanikishaji wa elimu ya mtoto wa kike. Hafla hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Tafakari wa HakiElimu uliopo ofisi za taasisi hiyo leo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Meneja wa Programu ya Ujenzi wa Vuguvugu la Harakati ya Kumkomboa Mwanamke kutoka TGNP Mtandao, Grace Kisetu na Mkurugenzi, CAMFED-Tanzania, Lydia Wilbard (kulia) wakiwa katika mkutano huo.

Hali halisi ya Elimu ya Mtoto wa Kike Ndugu wanahabari; kampeni hii inachagizwa na ukweli kuwa, elimu ya mtoto wa kike ina changamoto mbalimbali, ambazo hazina budi kutatuliwa ili kuwawezesha watoto wa kike kuwa shuleni na kupata elimu bora itakayowawezesha kutimiza ndoto zao hasa katika kuendeleza maisha yao na Taifa kwa ujumla. Kuna sababu mbalimbali zinazowafanya watoto wengi wa kike kuacha shule kila mwaka. Kwa mfano mwaka 2015 jumla ya watoto wa kike 69,067 wa shule za msingi na sekondari waliacha shule kwa sababu mbalimbali zikiwemo mimba utoro na vifo.  
  Meneja wa Programu ya Ujenzi wa Vuguvugu la Harakati ya Kumkomboa Mwanamke kutoka TGNP Mtandao, Grace Kisetu (katikati) akizungumza jambo kwenye uzinduzi wa kampeni maalumu ya kuhamasisha ufanikishaji wa elimu ya mtoto wa kike. Kulia ni Mratibu wa Ubora HakiElimu, Robert Mihayo na Mkurugenzi Mtendaji HakiElimu, John Kalage.

Baadhi ya changamoto nyingine za elimu ya mtoto wa kike ni kama zifuatazo; • Hali ya uandikishaji na upatikanaji wa fursa za kuwa shuleni. Japo hali ya uwiano wa uandikishaji kati ya wavulana na wasichana ni 1:1 katika ngazi ya elimu msingi, hali ni tofauti katika elimu ya kidato cha tano na sita. Idadi ya wasichana walio kidato cha tano na sita bado ni ndogo ikilinganishwa na wavulana, ambapo uwiano ni1:2. Hii ikimaanisha kuwa idadi ya wavulana ni mara mbili zaidi ya wasichana. Idadi ndogo ya wasichana inasababishwa na ufaulu mdogo wa wasichana kulingana na wavulana na hivyo kufanya asilimia ya wasichana wanaoingia kidato cha tano kuwa ndogo pia. Kwa miaka mitano mfululizo asilimia ya wasichana wanaoingia kidato cha tano imekuwa ni asilimia kati ya 5-6 ya waliofanya mtihani tofauti na wavulana ambao ni asilimia kati ya 12-13 kwa wastani. • Mazingira ya kujifunzia na kufundishia; kwa kiwango kikubwa, mazingira ya kujifunza na kufundishia bado si rafiki kwa mtoto wa kike. Kwa mujibu wa takwimu za BEST (Basic Education Statistics) za mwaka 2016, kuna upungufu mkubwa sana wa matundu ya vyoo ambapo wasichanaa 52 wanalazimika kutumia tundu moja la choo badala ya wasichana 20 kutumia tundu moja la choo. Ukosefu wa maji pia bado ni tatizo kwani asilimia 43.6 ya shule za msingi na asilimia 54.4 ya shule za sekondari tu ndiyo zina huduma ya maji. Hali ya ukosefu wa vyoo na ukosefu wa maji katika shule, inahatarisha afya zao na kuwaweka katika hatari ya kupata magonjwa yanayohusiana na uchafu. • Kutoshughulikiwa kwa changamoto za kimaumbile: Ni wazi kuwa kwa sababu ya maumbile ya kibaiolojia, mtoto wa kike ana mahitaji zaidi ya mtoto wa kiume. Hata hivyo kutokana na sababu za kukosa vifaa kama taulo za kike kwa ajili ya kuwasaidia katika siku zao, watoto wengi wa kike hushindwa kuhudhuria shule na kuamua kukaa nyumbani hadi siku zinapoisha. Utafiti wa SNV wa mwaka 2015 umeonesha kuwa asilimia 25 tu wa wasichana waliohusishwa katika utafiti ndio hupata vifaa. Utafiti umebaini kuwa njia mbadala kwa wasichana wasiopata vifaa ni kuamua kukaa nyumbani kati ya siku 4-5 ili kujisitiri na kukwepa aibu. Takwimu za utafiti wa SNV na uchambuzi wa HakiElimu kwa kutumia takwimu za BEST takribani wasichana 700,000 hadi 750,000 wa darasa la sita na saba hupoteza siku 40-50 kati ya siku 290 za mwaka wa masomo. Hii hufanya watoto wa kike kukosa vipindi vya kujifunza mada mbalimbali hivyo kuwaathiri kimasomona katika mitihani ya kitaifa. • Unyanyasaji wa Kijinsia-Ripoti ya Human Rights Watch ya mwaka 2017 yenye kichwa cha habari “I had a Dream to Finish School” imebainisha changamoto lukuki za unyanyasaji wa kijinsia kwa mtoto wa kike kama vile walimu kuwataka wanafunzi wa kike kimapenzi na kuwatishia kuwaadhibu wanapokataa kufanya mapenzi na walimu, na pia unyanyasaji wa wanafunzi wa kike mashuleni. Ripoti imebainisha madhara wanayopata watoto wa kike kwa kufanyiwa unyanyasaji na jinsi unavyowaathiri kisaikolojia na kuwafanya washindwe kuzingatia elimu yao wawapo shuleni. • Ukosefu wa Mabweni na changamoto za umbali: Uhaba wa mabweni, na changamoto za usafiri huwaathiri pia watoto wa kike hasa katika elimu ya sekondari. Shule nyingi za kata ziko mbali na makazi. Ripoti ya Human Rights Watch ya 2017 imebainisha kuwa changamoto za usafiri huwafanya wasichana kulazimika kufanya mapenzi na madereva wa magari au pikipiki ili kupata urahisi wa kusafiri kila siku kwenda shuleni, na matokeo yake hupata ujauzito na kufukuzwa shule. Pia wasichana huacha shule kwa sababu ya umbali na wengine hushindwa kutulia na kujifunza ipasavyo kwa sababu ya uchovu unaosababishwa na kutembea kwa umbali mrefu kila asubuhi na jioni. Aidha, kukosekana kwa mabweni na umbali wa shule huwafanya watoto wa kike kuwa katika hatari za kubakwa.(Human Rights Watch 2017).  
Baadhi ya wanahabari wakiwa katika uzinduzi wa kampeni maalumu ya kuhamasisha ufanikishaji wa elimu ya mtoto wa kike.
Baadhi ya wanahabari wakiwa katika uzinduzi wa kampeni maalumu ya kuhamasisha ufanikishaji wa elimu ya mtoto wa kike. Tunawezaje Kufanikisha Elimu ya Mtoto wa Kike • Serikali ihakikishe inatekeleza kwa vitendo wajibu wake wa kuhakikisha watoto wote wanapata elimu bila ubaguzi wa aina yoyote, ikiwemo kutatua changamoto za mazingira ya kujifunzia na kufundishia na kufanikisha kuwepo kwa elimu jumuishi katika elimumsingi. Kuna haja ya kuboresha miundombinu mbalimbali ya shule hasa vyoo, mifumo ya maji na kujenga mabweni katika shule, hususani za kata, ili watoto wa kike wawe katika mabweni. Hii itapunguza athari mbalimbali wanazokumbana nazo wakati wa kwenda na kutoka shuleni.Njia ya kufanikisha hili, ni kwa serikali kuongeza bajeti ya maendeleo kwenye elimumsingi ili kuwezesha uboreshaji wa miundombinu mashuleni. • 

Tunatambua kuwa serikali imekuwa katika mchakato wa kuandaa miongozo ya namna ya kuwarejesha shuleni watoto wa kike waliopata ujauzito na kujifungua. Mwaka 2015 pekee watoto wa kike takribani 3,690 wa shule za msingi na sekondari Tanzania walipata ujauzito, na kufukuzwa shule na hivyo kukatisha ndoto zao za mafanikio ya kupata elimu katika maisha yao. Kwa kuwa kupata elimu ni haki ya msingi kwa kila Mtanzania, serikali haina budi kuharakisha upitiaji na upitishwaji wa miongozo ili watoto wa kike waliojifungua warejee shuleni na kuendelea na masomo. Hoja ya msingi ya kuwarejesha watoto wa kike waliopata mimba inatokana na ukweli kuwa baadhi ya watoto wa kike hupata mimba kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao ikiwemo kubakwa au kudanganywa kutokana na shida wanazokumbana nazo katika mfumo wa elimu. 

Lazima tuelewe kuwa changamoto nyingi zinazosababisha watoto wa kike kupata mimba zinatokana na changamoto za mfumo wa elimu yetu. • 

Kutoa elimu kwa umma na watoto wa kike jinsi ya kumlinda mtoto wa kike dhidi vya vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na athari za vitendo vya ngono zembe. Jambo hili linaweza kufanikiwa zaidi kwa kuwahusisha zaidi viongozi wa serikali za mitaa, makundi ya utetezi wa watoto wa kike au elimu, asasi za kiraia na wanafunzi wenyewe. 

Mtoto wa kike akijengewa uelewa hata wa kutoa taarifa kwa vitendo vya unyanyasaji dhidi yake itasaidia kuwabaini na kuchukua hatua madhubuti dhidi ya wanyanyasaji. Pia itamwezesha mtoto wa kike kufahamu madhara ya kufanya ngono katika umri mdogo/akiwa shuleni na matokeo yake. Aidha, 

Jamii itambue kuwa kufanya mapenzi na watoto ni UBAKAJI na hivyo ni kosa kisheria kwa mujibu wa sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo waache vitendo vya kuwarubuni watoto wadogo na kuwashawishi kufanya nao mapenzi. Hitimisho HakiElimu inaamini kuwa elimu ni haki ya kila mtoto wakiwemo wasichana waliopata mimba. Mimba haiondoi haki ya kupata elimu kwa kuwa licha ya kuwa na mimba bado ni mtoto. 

Kuwafukuza watoto hao shuleni ni kuwanyanyasa wao na watoto watakaozaliwa ambao hawana makosa. Kama tulivyoonesha awali, baadhi ya watoto wamepata mimba kwa kulazimishwa kufanya ngono au kubakwa. Elimu ndiyo njia nzuri ya kuwakomboa wanawake na wasichana katika jamii, hasa wale walioathirika na mimba. Ndiyo maana HakiElimu inatetea wasichana hao wapate fursa ya kupata elimu na watiwe moyo ili waweze kuendelea na masomo baada ya kujifungua. Kama alivyosema Mwalimu Nyerere,― ‘Kwa watu masikini kama sisi, elimu inatakiwa kuwa chombo cha ukombozi’. Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto (UNCRC) pia unasisitiza watoto wote - wakiwemo waliopata mimba - wana haki ya kupata elimu bila kubaguliwa. John Kalage Mkurugenzi Mtendaji - HakiElimu

No comments