Header Ads

Responsive Ads Here

ELIMU BILA MALIPO YAONGEZA ZAIDI YA WANAFUNZI MILIONI TATU NCHINI


A1
Na Eleuteri Mangi-MAELEZO
Idadi ya wanafunzi kwenye ngazi mbalimbali za elimu nchini inaendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na hatua ya Serikali kuendelea kutoa Elimumsingi bila malipo.

Hakika hatua hiyo ya Serikali imekuwa mkombozi kwa Watanzania wengi wa kipato cha chini na cha kati amabao wazazi au walezi wengi walishindwa kuwasomesha watoto wao kutokana na gharama za hapo awali ambazo zilikuwa kikwazo kulingana na hali zao za kiuchumi.
Sekta ya elimu ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Magufuli ambayo imedhamiria kuleta mapinduzi ya kiuchumi ili kuibadili Tanzania  kuwa  nchi  ya  uchumi  wa  kati  ifikapo  mwaka  2025.
Ili kutimiza azma hiyo, ni dhahiri elimu bila malipo itasaidia kuwaelimisha wananchi wengi waweze kuwa sehemu ya mafanikio ya nchi yao katika kujenga uchumi.
Hatua ya Serikali ya kutoa elimu bila malipo imeanza kuonesha matokeo chanya kwa mwitikio wa wazazi na walezi kuwaandikisha watoto wao katika elimu ya awali, darasa la kwanza kwa shule ya msingi na kidato cha kwanza kwa shule za sekondari.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala Za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene alipokuwa akiwasilisha Bungeni hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya ofisi hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018, alisisitiza kuwa Serikali inatoa elimumsingi bila malipo siyo Elimumsingi Bure.
Hakika dhamira ya utoaji elimu bila malipo umekuwa ndio mkombozi wa wanafunzi, wazazi pamoja na walezi, jukumu lao ni kuhakikisha watoto wenye umri wa kwenda shule wanapata fursa hiyo ambapo kwa mwaka 2017 jumla ya wanafunzi zaidi ya 3,670,000 wamejiunga na masomo katika ngazi ya elimu ya awali, elimu ya msingi na sekondari.
Kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Rais TAMISEMI, uandikishaji wa wanafunzi wa elimu ya awali imeongezeka na kufikia wanafunzi 1,345,636 ambapo idadi ya wavulana ni 664,539 na idadi ya wasichana ikiwa ni 681,097 kwa mwaka 2017 ikilinganishwa na wanafunzi 971,716 ambapo idadi ya wavulana ilikuwa ni 480,053 na idadi ya wasichana ilikuwa 491,663 mwaka 2016, ongezeko hilo ni sawa na asilimia 38.5.
Uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza kwa mwaka 2017 nao umeongezeka na kufikia wanafunzi 1,842,513 ambapo idadi ya wavulana ni 931,674 na idadi ya wasichana ni 910,839 ikilinganishwa na wanafunzi 1,896,584 mwaka 2016.
Kwa upande wa elimu sekondari, idadi ya wanafunzi nayo imeongezeka na kufanya idadi yao kuwa jumla ya wanafunzi 483,072 hadi kufikia Machi, 2017 ambao walikuwa wameandikishwa wakiwemo wasichana 244,707 na wavulana 238,365.
Idadi hiyo ya wanafunzi hao ni sawa na asilimia 86.9 ya wanafunzi ambao walikuwa wamefika shuleni kati ya wanafunzi 555,291 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu wa masomo.
Aidha, jumla ya wanafunzi wenye mahitaji maalum walioandikishwa kwa elimu ya awali ni 4,337 na darasa la kwanza hadi Machi 2017 idadi ya wanafunzi ambao wameandikishwa ilikuwa ni 6,097.
Sanjari na hilo, kwa upande wa elimu sekondari, idadi ya wanafunzi wenye mahitaji maalum wakiwemo wenye ulemavu wa viungo mbalimbali waliojiunga kidato cha kwanza imeongezeka na kufikia wanafunzi 1,117 ikilinganishwa na  wanafunzi 648  walioandikishwa Mwaka, 2016.
Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 41 ya wanafunzi wenye mahitaji maalum walioandikishwa kidato cha kwanza katika shule zinazoandikisha wanafunzi wenye mahitaji hayo.
Akionesha dhamira ya Serikali katika kutoa elimu bila malipo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa ambaye ndiye Msimamizi Mkuu wa shughuli za Serikali alipokuwasilisha Bajeti ya Ofisi yake kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 alisisiza kuwa Serikali itaendelea na mpango wa kutoa Elimumsingi bila malipo.
“Tangu utekelezaji wa mpango huu uanze, Serikali imekuwa ikipeleka wastani wa Tsh. Bilioni 18.77 kila mwezi ambapo shule za msingi 16,088 na shule za sekondari 3,602 zimenufaika na mpango huo” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Kwa mujibu wa Waraka wa Elimu Na. 5 wa mwaka 2015, unaohusu Elimumsingi bila malipo, waraka huo unampa fursa mwanafunzi kusoma na kupata elimu bila mzazi au mlezi kulipa ada wala michango ya fedha iliyokuwa inatozwa shuleni kabla ya waraka huo kutolewa.
Aidha, Waraka wa Elimu Na. 3 wa mwaka 2016 unaohusu utekelezaji wa elimumsingi bila malipo nao unatoa mwongozo wa namna ya kutekeleza mpango huo wa Elimumsingi kulingana na Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 iliyozinduliwa Februari 13, 2015 na Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Kikwete.
Kwa mujibu wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Serikali imeweka utaratibu wa elimu ya awali kuwa ya lazima  na  kutolewa  kwa  watoto  wenye  umri  kati  ya miaka  mitatu  hadi  mitano  kwa  kipindi  kisichopungua mwaka mmoja.
Zaidi ya hayo Sera hiyo pia imebanisha kuwa Serikali ndio yenye jukumu la kuweka utaratibu  wa  elimumsingi  kuwa  ya lazima  kuanzia  darasa  la  kwanza  hadi  kidato  cha  nne ambayo inatolewa kwa miaka kumi, umri wa kuanza darasa la kwanza ukiwa kati ya miaka minne hadi sita kulingana na  maendeleo  na  uwezo  wa  mtoto  kumudu  masomo katika ngazi husika.
Ili kutekeleza Sera hiyo, yapo majukumu mbalimbali ambayo yanapaswa kutekelezwa na wadau wa sekta ya elimu ili mlengwa wa elimu ambaye ni mtoto aipate na kuweza kutimiza azma yake ambayo msingi wake ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ni matarajio ya Serikali kuwa zoezi zima la utoaji elimumsingi litaendelea kuwa na ufanisi kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Taknolojia, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Ofisi za Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya, Manispaa na majiji,, Kamati/Bodi za shule za Serikali, Wakuu wa shule, walimu, wanafunzi, wazazi na viongozi pamoja na jamii katika mamlaka za vijiji na mitaa ili kufanikisha azma ya Serikali ya kutoa elimu bila malipo kwa walengwa na kwa wakati.
Ili kuhakikisha dhana ya elimumsingi bila malipo inaeleweka na kila Mtanzania, Waziri Simbachawene amewasisitiza Waheshimiwa Wabunge, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Asasi zisizo za Kiserikali, Wadau wengine wa Elimu, Wazazi na Walezi kuendelea kutoa ushirikiano na kuhakikisha uwepo wa miundombinu muhimu ya shule kwa ajili ya wanafunzi wa elimu ya awali, msingi na sekondari kwa kujitolea hata nguvu zao katika kuchangia shughuli mbalimbali zinazohusu elimu.
Shime Watanzania ni wajibu wa kila Mtanzania  kujenga misingi  bora  ya  malezi,  maadili,  ujuzi,  umahiri  na kumwezesha  kijana ambaye ni nguzo ya taifa kujitegeme kwa kuzingatia mabadiliko  yanayotokea  katika  jamii,  kisiasa,  kiuchumi, kisayansi na kiteknolojia.

No comments