Header Ads

Responsive Ads Here

DKT. MABODI: CCM INAFANYA SIASA ZA USHINDANI WA SERA ZA MAENDELEO.


NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar , Abdulla Juma Saadalla “ Mabodi” amesema CCM itaendelea kufanya ushindani wa sera za maendeleo zitakazowanufaisha wananchi wa makundi yote mijini na vijijini.

Kauli hiyo ameitoa wakati akifungua Mafunzo ya Wanawake na Uongozi kwa wanachama na viongozi wa UWT Mkoa wa Mjini huko Amani Zanzibar, Dkt. Mabodi alisema wananchi wa visiwa vya Zanzibar kwa sasa wanachohitaji ni siasa za ushindani wa kisera katika kukuza kipato cha mwananchi mmoja mmoja hadi taifa kwa ujumla.

Dkt. Mabodi alisema taifa lolote linalotamani kuendelea kiuchumi ni lazima wananchi wake wakubali kwa vitendo dhana ya siasa za ustaarabu katika kudumisha amani na utulivu wa nchi ili kufanya kazi za kujiongezea kipato na kukuza uchumi wa nchi.

Aidha Naibu Katibu Mkuu huyo alisema ushindi wa CCM katika chaguzi mbali mbali za dola unatokana na nguvu za Wanawake wa UWT katika kuunga mkono harakati mbali mbali za kisiasa hadi kuhakikisha chama kinaingia madarakani.

“ kila mtu ndani ya Chama Chetu anajua na kutambua mchango wa Wanawake katika medali za kisiasa, wao ndio wamekuwa mstari wa mbele kwa kila kitu ikiwemo kujitokeza kwa wingi kupiga kura halali za kuiletea ushindi CCM.

Pia nakuahidini kwamba nitaendelea kuwa nanyi bega kwa bega kwa lengo la kuimarisha chama na jumuiza zake sambamba na kuwaletea wananchi maendeleo ya kudumu.”, alisema Dkt. Mabodi.

Kupitia Mkutano huo Dkt. Mabodi aliwasihi viongozi na watendaji wa Umoja wa Wanawake Tanzania kushuka ngazi za chini za uongozi hasa matawi na mashina kwa lengo la kuratibu changamoto zinazowakabili wananchi ili zitafutiwe ufumbuzi wa kudumu na serikali.

Aliwapongeza viongozi wa UWT waliojitolea kuanzisha mafunzo ya uongozi kwa wanawake wenzao ili wapate ujuzi wa kufanya siasa za maendeleo zitakazowajengea ujasiri wa kujenga hoja imara zinazokubalika katika ulimwengu wa siasa za ushindani.

Sambamba na hayo alimpongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Zanzibar Dkt. John Pombe Magufuli kwa juhudi zake za kulinda rasilimali za nchi hasa kuthibiti mianya ya usafirishaji wa Mchanga wa Madini unaosababisha upotevu wa fedha nyingi za umma.

Akizungumzia Uchaguzi wa ngazi ya Wadi unaoendelea hivi sasa katika Chama na Jumuiya aliagiza kwamba kamati zinazosimamia zoezi hilo zifanye kazi ya ziada ya kuhakikisha wanapatikana viongozi safi wasiokuwa na sifa za usaliti.

Mapema akizungumza katika Mkutano huo Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Mjini, Bi. Waridi Juma Othman aliahidi kuwa wanawake hao watatumia vizuri mafunzo ya uongozi katika siasa kama muongozo wa kufanya kazi za kisiasa kwa ufanisi mkubwa.

Akitoa neno la shukrani Mbunge wa Viti Maalum wanawake( MNEC), Khadija Hassan Aboud alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wanawake wa CCM ili waweze kuzitumika vizuri fursa za uongozi zinazopatikana ndani ya chama na serikali kwa ujumla.

Mafunzo hayo ya siku moja yameandaliwa na Mbunge wa Viti Maalum wanawake( MNEC), Khadija Hassan Aboud kwa kushirikiana na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mjini, Faharia Shomari Shomari Khamis.

No comments