Header Ads

Responsive Ads Here

WIZARA YA AFYA YAVUKA LENGO LA CHANJO NA KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA.

ngu5
(Jovina Bujulu- MAELEZO)
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto kupitia Mpango wa Taifa wa Chanjo imevuka lengo la kutoa chanjo na kuimarisha huduma nyingine za afya nchini. Huduma hizo ni pamoja na  udhibiti  magonjwa  ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza, magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele,huduma ya afya ya uzazi na mtoto, lishe, pamoja na utoaji wa elimu ya afya kwa umma.

Waziri mwenye dhamana na wizara hiyo Mhe. Ummy Mwalimu amebainisha hayo hivi karibuni alipokuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na  matumizi ya wizara hiyo kwa kipindi cha Mwaka wa Fedha 2017/18 mjini Dodoma.
Aliendelea kusema  kuwa wizara yake imehakikisha kuwepo kwa chanjo za kutosha  ambapo  jumla ya shilingi bilioni 18 zimetumika kununua na kusambaza chanjo kwa watoto na makundi mengine katika mikoa na Halmashauri zote nchini.
“Utoaji wa huduma za uhakika wa chanjo umewezesha nchi yetu kuwa miongoni mwa nchi zilizofanya vizuri kwa kipindi cha mwaka 2016, ambapo tumeweza kuvuka lengo kwa kufikia kiwango cha chanjo cha asilimia 97” alisema Ummy.
Aidha, Wizara imenunua magari tisa (09) kwa ajili ya kusambaza chanjo na majokofu 317 ya kutunzia  chanjo hizo kwenye vituo vya huduma za afya nchini.
Katika kuhakikisha kuwa huduma kwa wananchi inaboresha, Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele imeendelea  kugawa dawa za kingatiba. Dawa hizo ni pamoja na za matende, mabusha, usubi, trakoma, kichocho na minyoo katika Halmashauri 71 zenye maambukizi ya magonjwa hayo.
Huduma hiyo iliwezesha wananchi milioni 14.3  kufikiwa na wagonjwa 805 katika Halmashauri za Temeke na Ilala, jijini Dar es salaam na watu 100 kutoka mkoa wa Mwanza  walifanyiwa upasuaji wa mabusha na matende bila malipo.
Wizara pia imeendelea na mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria kwa kusambaza dawa za kutibu na vipimo vya kupima (MRDT) katika mikoa 26 ya Tanzania Bara, dozi za dawa mseto na vitepe vya MRDT vya shiilingi milioni18 zimenunuliwa na kusambazwa katika vituo vya afya.
Katika kuhakikisha ugonjwa wa malaria unatokomezwa, wizara imeendelea  kuhamasisha matumizi ya kipimo cha MRDT  na kunyunyiza dawa ya ukoka katika mikoa ya  Kanda ya Ziwa ya Kgera, Mwanza, Mara na Geita ambayo ina maambukizi makubwa ya malaria na kugawa vyandarua milioni 2.6 vyenye viuatilifu katika Halmashauri ya Kilombero  mkoani Morogoro na Halmashauri zote za jijini Dar es salaam.
Akizungumzia hali ya ugonjwa wa kifua kikuu, Waziri Ummy alisema kuwa kwa sasa huduma za matibabu ya ugonjwa huo zimeimarishwa na kusogezwa karibu na wananchi kutoka hospitali moja ya Kibong’oto hadi kufikia vituo 18. Huduma za maabara pia zimeboreshwa kwa kuimarisha maabara za Kandaya-Mbeya, Bugando-Mwanza, hospitali ya rufaa mkoa wa Dodoma na Kibong’oto mkoani Kilimanjaro.
Kuhusu hali ya ugonjwa wa UKIMWI nchini , Wazii Ummy alisema kuwa wizara  yake imeendelea kutoa ushauri nasaha na kuwahimiza wananchi kupima mara kwa mara ili kujua hali ya afya zao ambapo kwa kipindi cha mwaka 2016 jumla ya watu milioni 7.4 walipata ushauri nasaha na kupima VVU.
Katika kupambana na magonjwa yasiyoambukiza, waziri alisema kuwa wizara yake imeandaa Mkakati wa Kitaifa wa kupambana na magonjwa hayo wa mwaka 2016-2020 ambao ulizinduliwa Dodoma mwaka 2016.
Mkakati huu unafuatia ongezeko kubwa la magonjwa hayo ambayo ni kisukari, shinikizo la damu na magonjwa ya moyo. Ili wananchi waweze kukabiliana na magonjwa hayo, wizara imeanzisha kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi, kupima afya mara kwa mara na kuzingatia ulaji wa chakula unaofaa.
Katika kipindi cha mwaka jana , huduma ya afya ya uzazi na mtoto imeimarishwa kwa kuandaa Mpango Mkakati wa miaka mitano wa 2016-2020  unaolenga kuboresha afya ya uzazi, watoto na vijana na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi hadi kufikia 292 kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo 2020.  Kwa sasa vifo hivyo ni 556  kwa kila vifo hai 100,000.
“Katika kutekeleza mkakati huo, wizara imezingatia maeneo makuu matatu ambayo ni hududma ya uzazi wa mpango, huduma wakati wa ujauzito na huduma wakati wa kujifungua”. Alisema waziri Ummy.`
Akizungumzia upatikanaji wa huduma ya uzazi wa mpango Waziri Ummy alisema wizara yake imefanya jitihada za kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa watu wote wanaostahili ambapo kwa kipindi cha July mwaka 2016 na Machi 2017, jumla ya watu 357,244 wamefanikiwa kupita huduma kupitia hospitali za mikoa na watu  2,509,280 walifanikiwa kupata huduma hiyo kupitia vituo vya afya.
Aidha, Waziri alitoa wito kwa wakina mama wajawazito kuhudhuria kliniki angalau mara nne katika kipindi cha ujauzito na kuzuia vifo vitakanavyo na uzazi vinavyoepukika, lengo la Serikali ni kufikisha asilimia 70 ya wanawake wajawazito kuhudhuria kliniki na kupata huduma ifikapo 2020 ili kunusuru maisha ya mama na mtoto.

No comments