Header Ads

Responsive Ads Here

WANAWAKE WANAOJIFUNGULIA NYUMBANI NA NJIANI WATOZWA FAINI YA SHILINGI 50,000/-

   

BAADHI ya wanawake wa kata ya Lyangalile wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa wamelalamikia kitendo cha kutozwa fedha kiasi cha shilingi 50,000 ikiwa ni adhabu kutokana na kujifungua katika maeneo ambayo siyo salama na hakuna huduma za uzazi salama.

Wanawake hao walitoa malalamiko yao kwa Katibu wa CCM mkoa wa Rukwa Mwanamasudi Msafiri Ibrahim Pazi alipokuwa katika kata hiyo akifanya ziara ya kukagua maendeleo ya chaguzi za ndani ya chama hicho na kusikiliza changamoto walizonazo wakazi wa kata hiyo.

Wanawake hao walisema wamekuwa wakitozwa fedha hizo na watendaji wa afya pindi wanapofika katika vituo vya uzazi salama kwa lengo la kupata matibabu.

Mmoja wa wanawake hao aliyejitambulisha kwa jina la Marystella Kaputa mkazi wa kata hiyo alisema wanaumia sana kwa kitendo cha kutozwa fedha hizo kama faini kutokana na kutojifungulia katika eneo ambalo halitoi huduma za uzazi salama kama majumbani na njiani wanapokuwa wanapelekwa kujifungua.

Alisema inawezekana nia ni njema ili kuwaadhibu wanawake ambao hawaendi kujifungua katika vituo vya huduma za uzazi salama lakini adhabu hiyo imekuwa ni kubwa sana hasa ikizingatiwa kuwa sio wote wanaofanya hivyo kwa maksudi bali wengine wanajikuta inawatokea kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ni pamoja na usafiri, maandalizi duni sambamba na ndugu zao kutofanya maamuzi wakati uchungu unapo waanza.

Naye Adelina Severino mkazi wa kata hiyo alisema kitendo wanachofanyiwa wanawake hao sio sawa bali kinachotakiwa ni watendaji wa afya kuendelea kutoa elimu ili wanawake waone umuhimu wa kwenda kujifungulia katika maeneo yanayotoa huduma za uzazi salama kama zahanati, vituo vya afya na hospitali ili kuepuka changamoto zinazoweza kuwakuta wakati wakijifungua katika maeneo hayo.

Kwa upande wake Sekunde Nanyumbu mkazi wa kata hiyo alisema wakati mwingine wanawake wanakutwa na hali hiyo kutokana na ndugu wa karibu kama mume, wakwe na wengine wenye maamuzi katika ukoo kutowaruhusu ama kufanya maamuzi ya haraka ili wafike katika maeneo yanayotoa huduma za uzazi salama.

Aliongeza kuwa katika kata hiyo wanategemea zahanati iliyopo katika kijiji cha Katonto ambapo baadhi yao wanaishi umbali wa kilometa nne mpaka kuifikia zahanati hiyo hali ambayo imekuwa ikichangia wanawake kujifungua katika maeneo ambayo siyo salama kwao.

Hata hivyo katibu huyo wa CCM mkoa wa Rukwa alilaani kitendo hicho na kuahidi malalamiko yao kuyafikisha kwa watendaji wa afya ngazi ya mkoa ili yashughurikiwe na kukomeshwa kabisa kwani mpaka sasa Sera ya afya ni huduma bure kwa wakina mama wajawazito kitendo cha kuwa toza faini siyo sawa.


Kaimu mganga Mkuu wa mkoa wa Rukwa Emmanuel Mtika alikiri kuwepo kwa malalamiko hayo na kusema kuwa wanaopaswa kupewa adhabu ni wanawake wanaojifungulia nyumbani na si wale wanao jifungulia njiani lakini pia tume imeundwa kwa lengo la kuchunguza malalamiko hayo ili hatua ziweze kuchukuliwa kwani ni kosa kuwatoza faini hiyo ya shilingi 50,000 ambayo ni kubwa.

No comments